28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Kaseke avuna mil 88/- Yanga

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA winga wa Mbeya City, Deus Kaseke, amevuna takribani Sh milioni 88 kwenye mkataba wa miaka miwili aliousaini jana kujiunga na mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), timu ya Yanga.

Kaseke anaondoka Mbeya City kama mchezaji huru, kutokana na kumaliza mkataba ndani ya timu hiyo, ambayo haijavuna chochote kwenye usajili wa winga huyo kwenda Yanga.

Kiasi hicho cha fedha kinatokana na dau la Sh milioni 40 lililomwezesha kusaini, sambamba na mshahara wa Sh milioni 2 atakaolipwa kila mwezi kwa miezi yote 24 (sawa na Sh milioni 48).

Habari za uhakika zilizolifikia MTANZANIA jana kutoka kwa mtu wa karibu wa winga huyo, zimeeleza kuwa mbali na kitita hicho, Kaseke pia amepewa nyumba ya kuishi pamoja na gari jipya aina ya GX 100.

Yanga yatumia umafia

Klabu ya Yanga iliizidi kete Simba hadi kunasa saini ya winga huyo mwenye kasi na krosi za uhakika, inadaiwa. Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, alikuwa tayari kumpa fedha taslimu Sh milioni 35 na mshahara wa Sh milioni 2.5 kwa mwezi ili asaini.

“Yanga walimuwahi Uwanja wa Ndege usiku jana (juzi) na kumficha hotelini (Valley View Hotel) hadi walipomalizana naye asubuhi (jana), lakini Hanspope naye alileta ofa hiyo, lakini Yanga waliweka ulinzi hotelini asitoke hadi aliposaini,” kilieleza chanzo hicho.

Kiliongeza kuwa viongozi wa Simba ndio wamefanya uzembe hadi akashindwa kusaini, kwani walikuwa wakichukulia mambo kirahisi tokea msimu uliopita walipoanza mbio za kumnasa.

CAF yamvuta Kaseke

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kaseke alisema mbali na maslahi, jambo jingine kubwa lililomfanya kujiunga na Yanga ni kutokana na timu hiyo kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.

“Michuano ya Afrika imechangia mimi kwenda Yanga, kwani nataka kujiuza na kupata timu nje ya nchi kupitia michuano hiyo, lakini maslahi pia yamechangia,” alisema.

Kaseke alisema mashabiki wa Yanga watarajie makubwa kutoka kwake, huku akiwaomba wamuunge mkono ili kuipa mafanikio timu hiyo.

“Pia nataka kuwashukuru viongozi na mashabiki wa Mbeya City, kwani wao ndio wamenifanya mimi kuwa hapa, naomba waniombee Mungu nifanikiwe zaidi, siwezi kuwasahau daima,” alisema.

Mbali na Yanga kukamilisha usajili wa Kaseke, pia inadaiwa wapo katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa winga Haroun Chanongo, aliyekuwa akichezea Stand United kwa mkopo akitokea Simba msimu uliopita.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles