24 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Tuzo za TAFA zatolewa, Ray ashangaa

FARAJA MASINDE
LICHA ya Shirikisho la Filamu nchini (TAFF) kufanikiwa kutoa tuzo za kwanza za TAFA, mwigizaji maarufu, Vicent Kigosi ‘Ray’, ameonyesha kutoridhishwa na uandaaji wa tuzo hizo.
Tuzo hizo zilitolewa juzi usiku katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam, huku Ray akikosekana katika kipengele hata kimoja kati ya vilivyoshindanishwa.
Ray aliingia ukumbini hapo akiongozana na msichana wakiwa wamechelewa, ingawa walikuwa makini kufuatilia utoaji wa tuzo hizo.
Hata hivyo, kabla tuzo mbili za mwisho hazijatolewa, wawili hao waliinuka katika viti walivyokaa wakaondoka zao, huku wakionyesha kutokuridhishwa na zoezi hili.
Katika mazungumzo na baadhi ya waandishi wa habari, vipengele vilivyoonekana kumkera Ray na wahudhuriaji wengine ni cha Best AC kilichokuwa kikihusu mtu, kampuni au taasisi iliyotoa mchango mkubwa kwenye filamu.
“Sasa Best AC ndiyo tuzo gani hii?’’ aliuliza Ray na kuendelea; “Mbona kuna majina mengi ya kuita tuzo, lugha yenyewe iliyotumika ni Kiingereza, mtu anaelewa kweli hiki kipengele bila ufafanuzi,” alilalama Ray, huku akiondoka ukumbini hapo.
Ray aliongeza: “Tuzo ni nzuri, ingawa sipo kwenye kipengele chochote kwa kuwa Watanzania ndio wameamua, nakubaliana na maamuzi,’’ alieleza.
Katika hatua nyingine, mwongozaji wa filamu, John Kallage, ndiye aliyeibuka kinara baada ya kuibuka na tuzo mbili, ikiwemo ya mwongozaji bora na filamu bora, kupitia filamu yake ya ‘Network’.
Filamu hiyo ya ‘Network’ ilizimwaga filamu ilizoshindanishwa nazo ya ‘Kitoga’, ‘Mdundiko’, ‘Shikamoo Mzee’, ‘Samaki Mchangani’, ‘Dogo Masai’ na ‘I love you Mwanza’.
Tuzo ya mtunzi bora ilikwenda kwa Irene Sanga, wakati tuzo ya msanii bora wa kike msaidizi ikienda kwa Grace Mapunda na kwa mwanamume ilinyakuliwa na Tino Muya.
King Majuto alinyakua tuzo ya mchekeshaji bora, wakati tuzo ya msanii bora wa kike ikichukuliwa na Irene Paul, huku msanii bora wa kiume akiibuka Brian Ibrick.
Tuzo ya msanii aliyetumia muda mwingi kwenye sanaa ilinyakuliwa na Bakari Mbelemba ‘Mzee Jangala’, huku kipindi bora cha filamu kikiwa ‘Take One’ cha Clouds TV.
Tuzo nyingine ni ya aliyetoa mchango kwenye filamu ambayo imeelekezwa kwa Steven Kanumba ‘marehemu’, huku kipengele cha sera bora kikikosa washiriki.
Rais Jakaya Kikwete naye alitunukiwa tuzo ya nishani ya heshima kutokana na mchango wake wa kusaidia sanaa ya filamu kipindi chote cha utawala wake.
Hata hivyo, mgeni rasmi katika hafla hiyo ya utoaji tuzo, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Fenella Mukangara, aliahidi kusaidia tasnia ya filamu hata kama hatakuwa waziri kwa miaka ijayo.
Akifafanua kuhusu tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa kwa waandaaji wa tuzo hizo, Rais wa Shirikisho la Filamu nchini, Simon Mwakifamba, alisema wanastahili pongezi kwa kuwa hawakuwa na wadhamini wakubwa, lakini wameweza kuendesha zoezi hilo kwa mafanikio.
“Changamoto lazima ziwepo, kwa kuwa ndiyo tunaanza, tunaomba Watanzania watuunge mkono ili mashindano haya yafike mbali, kwa kuwa kwa sasa tunatumia fedha zetu wenyewe na misaada midogo kutoka kwa washirika wetu, kwa hili la lugha tumelazimika kutumia Kiingereza kwa kuwa tumeshindwa kupata fasili ya neno la Kiswahili, lakini pia kulikuwa na wageni mbalimbali, imesaidia kujitangaza na kuongeza ufahamu,’’ aliendelea.
Msimu huu ni msimu wa tuzo mbalimbali ambapo Tuzo za Watu zimetolewa na washindi mbalimbali kupatikana, sasa tuzo za TAFA, pia tutarajie tuzo za Kili na tuzo za ZIFF ambazo hufanyika visiwani Zanzibar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles