27.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

Mwalyanzi amwaga wino Simba

IMG-20150524-WA0026NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

KLABU ya Simba imejibu mapigo ya wapinzani wao wa jadi, Yanga, baada ya kumnasa aliyekuwa kiungo wa Mbeya City, Peter Mwalyanzi na kumpa mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo msimu ujao.
Jana Simba iliangukia pua kwenye mbio za kumnasa winga Deus Kaseke, aliyekuwa amemaliza mkataba wake Mbeya City kama Mwalyanzi, baada ya Yanga kumuwahi na kumsajili.
Wakati Simba ikiinasa saini ya Mwalyanzi, imefanikiwa kuzizidi kete Azam FC na Yanga ambazo awali zilionyesha nia ya kuhitaji huduma yake msimu ujao.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, alisema tayari wameshamalizana na kiungo huyo, huku akitamba wanatarajia kuendelea kukifanyia marekebisho kikosi chao kadiri inavyohitajika.
“Tuna imani kubwa na mchezaji huyu kwenye kikosi chetu na tunaamini ataisaidia timu ipasavyo kulingana na uwezo wao, tumemsajili kulingana na maelekezo ya kocha Goran Kopunovic na tutafanya usajili kulingana na mahitaji yake,” alisema.
MTANZANIA limebaini ya kuwa Mwalyanzi, aliyetua jijini Dar es Salaam jana asubuhi kwa usafiri wa ndege akitokea Mbeya, amesaini mkataba kwa dau la Sh milioni 30, nyumba ya kuishi pamoja na mshahara wa Sh milioni 1.5 kwa mwezi.

Mwalyanzi anena
Kwa upande wake, Mwalyanzi aliliambia gazeti hili kuwa sasa mashabiki wa timu hiyo wasubiri kuona mambo mazuri kutoka kwake, kwani alitamani kuchezea Simba na hatimaye amepata nafasi hiyo.

“Niliipenda Simba kwa sababu ina wachezaji vijana na wao pia walionyesha nia ya kunihitaji, tofauti na Yanga ambao pia walikuwa wakinitaka, hivyo nikaona nisaini kwa hao walioonyesha kunihitaji zaidi na nawataka mashabiki wakae tayari na wategemee mazuri kutoka kwangu,” alisema.

Simba imepanga kuacha wachezaji 10 kwenye kikosi chao kilichocheza Ligi Kuu msimu uliopita, watatu wakiwa ni wachezaji wa kigeni ambao tayari wameshajulikana, wakiwa ni Danny Sserunkuma, Joseph Owino na Simon Sserunkuma, huku wachezaji saba hadi sasa wakiwa hawajafahamika.

Wekundu hao wamepanga kuimarisha kikosi chao ili watwae ubingwa wa Ligi Kuu msimu ujao na kuondoa ukame wa miaka mitatu wa kutotwaa ubingwa na kutoshiriki michuano ya kimataifa.

Wakati huo huo, muda wowote kuanzia leo Simba inatarajia kuingia mkataba na beki Kenny Ally, aliyekuwa akichezea Mbeya City, ambaye ameshatumiwa tiketi ya ndege na uongozi wa wekundu hao ili kutua Dar es Salaam na kusaini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles