24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 20, 2024

Contact us: [email protected]

KAONJE: PANYA NI MTAMU ZAIDI YA KUKU, SAMAKI

Na FLORENCE SANAWA-MTWARA


ULAJI wa panya umekuwa ukiwashangaza wengi huku wengine wakistaajabu juu ya ulaji wa mbwa, konokono, vyura, kenge na chatu.

Viumbe hivi huliwa katika maeneo mengi duniani na hata kwa baadhi ya makabila nchini huvitumia kama kitoweo hali ambayo hufanya wengine kustaajabu pale wanapoona makabila hayo yakila.

Kwa Mkoa wa Mtwara baadhi ya watu wamekuwa wakila panya, vyura na kenge. Utegaji na uuzaji wa panya umekuwa ukiwanufaisha watu wengi katika Kijiji cha Chikoweti, Kitongoji cha Mbuyuni wilayani Masasi mkoani Mtwara.

Kijiji hicho kilichoko Kaskazini mwa mji wa Masasi kinakaliwa zaidi na watu wa kabila la Kimakua ambao wamekuwa na historia ya kutumia panya katika maisha yao ya kila siku kama kitoweo muhimu katika mlo.

 

KWANINI PANYA?

“Ukiangalia kihistoria, uhaba wa samaki ndio ulitufanya tuanze kutega panya kama kitoweo, wanatusaidia kwa kuwa hawana msimu.

“Panya anayeliwa huwa ni mweupe yaani ana manyoya meupe, wengi hudhani kuwa panya anayeliwa ni yule wa majumbani lakini yule hapaswi kuliwa kwa kuwa anakula vitu vingi huenda akawa na sumu mwilini,” anasema Edgar Mpupua ambaye ni maarufu kwa uwindaji, utengenezaji wa mitego na uuzaji wa panya.

Naye Petro Kaonje mkazi wa Kijiji cha Chikoweti anasema ladha ya panya ni tofauti na nyama alizowahi kula ndio maana haachi kula kitoweo hicho.

“Unajua unaweza kumuangalia ukamdharau lakini panya ni mtamu, sisi tunaoishi huku hatuna mabwawa wala mito ndio maana panya wanalika kutokana na uhaba wa samaki kijijini kwetu.

“Sisi Wamakuwa, Wayao na Wamakonde tunapenda kula panya, hii ni asili yetu huwezi kuikana kwa kuona aibu.

“Mbona wenzetu Wachina wanakula hadi mende lakini wanafurahia tu maisha, panya ni kitoweo  na ambacho kinapendwa,” anasema Kaonje na kuongeza:

“Panya wanaoliwa sisi tunawafahamu na wasioliwa hatuhangaiki nao, tunapomkamata tunamchoma kisha tunakula na wali ama ugali ile ni mboga nzuri.

Naye Samwel Mbaga anasema yeye si panya tu, bali pia anakula kenge, vyura na wanyama wengine ambao humpa burudani zaidi.

Anasema ulaji wa kenge umekuwa ukimpa burudani zaidi kutokana na kazi kubwa ya kumpa panya hivyo kuwa rahisi kwake kumpata kenge.

Kwa upande wake Martha Mkuti anasema ulaji wa panya ni wa mazoea kutokana na kutokuwa na kitoweo mbadala katika maeneo wanayoishi.

“Ni kweli ladha ya panya ni kama samaki ndio maana tunaridhika kula, wapo watu wanaunga kwa nazi, ni watamu mno na wengine hupenda kula chukuchuku (kuweka chumvi bila kuchanganya na kitu kingine).

“Raha ya panya unakula kila kitu hadi mifupa, ni wanyama shambani lakini nyumbani ni mboga. Mara nyingi tunapenda kula baada ya kumchoma halafu ndio unaiunga,” anasema Mkuti.

Samwel Minjale Mkazi wa Kijiji Chikoweti, anasema katika maisha yake amejifunza kula vyakula vingi lakini amevutiwa zaidi kula panya kitoweo ambacho ni rahisi kupatikana.

“Mimi namfahamu kwa kumla na si kwa kumsikia, huwezi kumfananisha na samaki kwani ana mafuta ya pekee na hutumii nguvu kumuandaa.

“Huwezi kumfananisha na kiumbe mwingine wala kuku, yaani panya ukishamkamata unamchoma na ana mafuta ya kujitegemea ila unaongeza chumvi tu,” anasema Minjale.

 

MITEGO

Mzee Mpupua ambaye anajishughulisha kutengeneza mitego ya panya,  anasema kazi hiyo ameifanya kwa zaidi ya miaka 36.

“Nilianza kutengeneza mitego mwaka 1982 na maisha yangu kwa kiasi kikubwa naendesha kwa biashara hii,” anasema.

Anasema uuzaji wa panya umeshamiri katika miaka ya hivi karibuni baada ya wategaji kuongezeka hali iliyosababisha kupandisha bei ya mitego.

“Awali nilikuwa nauza mtego kwa Sh 100 baadae ikapanda hadi Sh 200, hivi sasa nauza mitatu kwa Sh 1,000 na tunaofanya biashara hii siku hizi ni wengi.

“Mara nyingi huwa tunakwenda porini tunawavuna panya kisha tunawakausha kwa moto na kuwauza kwa mafungu. Nimekuwa nikimaliza mipango midogo midogo ya kifamilia kwa kuuza panya na mambo yamekuwa yakienda sawa,” anasema Mpupua.

 

SOKO LA PANYA

Soko kubwa la panya liko katika maeneo ya Mtandi, Migongo, Mwimbaka, Mbarika na Kanyimbi ambako ndiko kuna wateja wengi wa kitoweo hicho.

Kitoweo hicho huuzwa kwa mafungu ya panya watano kwa Sh 500 na fungu lingine ambalo huwa na panya wanane ambao ni wakubwa huuzwa Sh 1,000.

Anasema kwa siku wanaweza kuvuna zaidi ya panya 2,000.

Hata hivyo, Mpupua anasema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika utegeji wa kitoweo hicho na hivyo wakati mwingine kuhatarisha maisha yao.

“Tunapata shida kwa sababu wengi wetu tunatembea bila kuvaa viatu, hata wanaovaa wamekuwa wakitumia viatu ambavyo haviwazuii kujikinga na wanyama hatari kama nyoka na wengineo,” anasema Mpupua.

 

MTAALAMU WA LISHE

Ofisa Lishe Mkoa wa Mtwara, Herieth Kipuyo, anasema ulaji wa nyama una faida kubwa kwenye mwili wa binadamu.

“Unajua panya yupo kwenye kundi la vyakula vyenye protini, yupo katika kundi la nyama kati ya makundi matano ya vyakula. Makundi haya yana umuhimu ndani ya mwili wa binadamu kwa kuujenga ili uweze kufanya kazi vizuri.

“Lakini siwezi kusema moja kwa moja kwamba nyama ya panya ni muhimu kwa kiasi gani au ina madhara kiasi gani,” anasema Kipuyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles