20.9 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

DUNIA YAENDELEA KUPOTEZA VIUMBE HAI ADIMU

JOSEPH HIZA Na MTANDAO


RIPOTI tano mpya zilizozinduliwa katika Mkutano Mkuu wa Viumbe Hai wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Colombia zimetahadharisha juu ya hali mbaya inayovikabili baadhi ya viumbe hai duniani.

Lakini pia ilikuja na mapendekezo ya namna ya kupambana na changamoto hiyo inayokabili aina ya mimea na wanyama wa mwituni na baharini walio hatarini kutoweka.

Wajumbe katika Mkutano Mkuu wa Kimataifa juu ya viumbe hai mjini Medellín, Colombia wameshtuka baada ya kutolewa kwa ushahidi mpya juu ya hali ya viumbe hai duniani.

Wajumbe 750 kutoka nchi 115 walikutana katika kikao cha sita cha Jukwaa la Kisayansi na Sera Baina ya Serikali la Huduma za Viumbe Hai na Mfumo wa Ekolojia (IPBES) mwezi uliopita.

Jukwaa hilo lilipewa kazi na Umoja wa Mataifa mwaka 2012 kutoa ushahidi bora zaidi ili kuwezesha kufanyika uamuzi bora wa sera juu ya namna ya kulinda mazingira katika wakati ambapo dunia inaendelea kukabiliwa na shinikizo kubwa la mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti hizo tano, ambazo zilitayarishwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na wataalamu wa kimataifa wapatao 550, zinatoa tathmini ya kikanda juu ya viumbe hai barani Afrika, Amerika Kaskazini na Amerika Kusini, Asia Pasifiki, Ulaya na Asia ya Kati. Ripoti ya tano inatoa tathmini juu ya hali ya uharibifu wa ardhi duniani kote.

Ripoti hizo zinahitimisha kuwa kwa upande wa Amerika, viumbe hai vya mimea na wanyama zimepungua kwa asilimia 31 ikilinganishwa na wakati walipowasili walowezi kutoka Ulaya.

Athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwa zinaongezeka zimechangia sababu nyingine, kupotea huko kwa viumbe hai kunatabiriwa kufikia asilimia 40 ifikapo mwaka 2050.

Katika Afrika, kilomita 500,000 za mraba za ardhi tayari zinakadiriwa kuwa zimeharibiwa na matumizi makubwa ya rasilimali za asili, mmomonyoko wa ardhi, myeyusho wa chumvi na uchafuzi wa mazingira.

Aidha, mabadiliko ya tabianchi na shughuli za binadamu yanaelezwa kusababisha upotevu wa aina mbalimbali za miti ikiwamo mibuyu pamoja na zaidi ya nusu ya ndege wa Afrika na aina fulani za mamalia ifikapo mwaka 2100.

Katika Umoja wa Ulaya, ni asilimia saba pekee ya viumbe hai vya baharini na asilimia tisa ya aina za viumbe vinavyoishi humo zinazoonyesha ‘hali nzuri ya hifadhi’.

Asilimia 66 ya aina za viumbe vinavyoishi baharini inaonyesha ‘hali mbaya ya hifadhi’ na aina nyingine zimeorodheshwa kama ‘haijulikani’.

Kanda ya Asia-Pasifiki imeonyesha matokeo ya kutia moyo zaidi. Katika miaka 25 iliyopita, maeneo ya bahari yanayohifadhiwa katika kanda hiyo yameongezeka kwa takriban asilimia 14 na maeneo ya ardhini yanayohifadhiwa yameongezeka kwa asilimia 0.3. Maeneo ya misitu yameongezeka kwa asilimia 2.5.

Ripoti hizo pia zimegundua ukosefu wa mafanikio katika mipango mikakati mbalimbali ya Umoja wa Mataifa kuhusu viumbe hai, ikiwa ni pamoja na Mpango wa Mikakati wa Viumbe Hai 2011-2020.

Mengine ni malengo yanayohusu viumbe hai, yaliyofikiwa na makundi tofauti yaliyohusika katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Viumbe Hai uliofikiwa huko Aichi nchini Japan mwaka 2010.

Lakini pamoja na kuonyesha hali ya kutisha, ripoti hizo pia zimetoa matumaini mapya ya kupambana na tatizo hilo.

Mapendekezo maalumu kuhusu jinsi watunga sera wanavyoweza kusitisha au kurekebisha uharibifu wa viumbe hai katika maeneo tofauti.

“Zikiwekwa pamoja, ripoti hizi tano za utafiti zinawakilisha mchango mmoja muhimu wa kitaalamu kwa ufahamu wetu wa kimataifa wa viumbe hai na mfumo wa ekolojia wa miaka 10 iliyopita.

“Tathmini hizi zitatoa ufahamu ambao haukuwahi kushuhudiwa juu ya hali ya viumbe hai duniani na ubora wa ardhi, vitu viwili, ambavyo ni muhimu kwa ubora wa maisha na afya, na mifumo ya ekolojia. Uhitaji wa hatua za kuchukua haujawahi kuwa muhimu zaidi kuliko wakati huu tulionao,” anasema Robert Watson, mwenyekiti wa mkutano huo.

Kwa mujibu wa ripoti, kila mwaka binadamu hutumia rasilimali nyingi zaidi kuliko uwezo wa dunia na hivyo matokeo yake ni kwamba mifumo muhimu ya ekolojia inaharibiwa.

Madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanasababisha tatizo kuwa baya zaidi, isipokuwa pale wasimamizi watakapochukua hatua. Lakini Anne Larigauderie, katibu mtendaji wa IPBES, ambaye anaamini ushahidi mpya uliotolewa utahamasisha kuchukuliwa hatua za kukabili mwelekeo mbaya wa kimazingira unaoikabili dunia.

“Kuna ufahamu mkubwa wa haja ya mazingira kujumuishwa katika mipango yote ya maendeleo na IPBES inajivunia kuwapatia watoa uamuzi duniani kote ushahidi wanaouhitaji utakaowawezesha kutunga sera bora na kuchukua hatua bora zaidi kuweza kuwa na maisha ya baadae yaliyo endelevu tunayoyataka,” anasema.

Ripoti hizi zimekuja huku mwaka jana ripoti nyingine ikionya kuwa ukataji miti, uwindaji na uvuvi haramu wa viumbe vilivyo hatarini kutoweka unafanyika katika nusu ya maeneo ya hifadhi za maliasili ulimwenguni.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Shirika la Wanyamapori Duniani (WWF), maeneo ya urithi wa dunia kama vile Matumbawe makuu ya Australia, Hifadhi ya Taifa ya Virunga katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Visiwa vya Galapos yana idadi kubwa ya wanyama na mimea iliyo adimu duniani.

Lakini WWF inasema kuwa Mkataba wa Kimataifa wa Kuvilinda Viumbe Vilivyo Hatarini (CITES) unakabiliwa na kitisho kikubwa kutokana na asilimia 45 ya usafirishaji haramu kwenye zaidi ya maeneo 200 ya urithi wa asili wa ulimwenguni.

“Maeneo ya urithi wa dunia ni miongoni mwa yanayotambuliwa kuwa ya asili ulimwenguni kutokana na thamani yake,” anasema Marco Lambertini, Mkuu wa WWF International.

“Mengi ya maeneo hayo yanaharibiwa na shughuli za viwanda na hivyo mimea na wanyama wake wanaathirika vibaya mno. Bila kuyalinda kikamilifu, tutawapoteza moja kwa moja.”

Ripoti hiyo inasema takribani robo moja ya chui 3,890 wa msituni na asilimia 40 ya tembo wa Afrika wanapatikana katika maeneo yaliyoorodheshwa na Shirika la Maendeleo ya Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), ambayo ndilo kimbilio la mwisho la viumbe walio hatarini kabisa kutoweka duniani kama vile kifaru aina ya Javan nchini Indonesia.

Pomboo wadogo kabisa aina ya ‘vaquita’ waliopo Ghuba ya California nchini Mexico wako hatarini kumalizika ndani ya mwaka mmoja ujao.

Kwa hivyo, ukataji miti, uwindaji na uvuvi haramu ndani ya maeneo kama hayo unaelezwa kusababisha viumbe vilivyo hatarini kuwa ukingoni mwa kutoweka kabisa kabisa,” inaonya ripoti hiyo ya WWF.

Wakati pomboo wadogo wakiwa hawavuliwi kinyume cha sheria, bali wanajikuta wakinaswa na nyavu zinazovua samaki wakubwa wa Kimexico waitwao ‘totoaba’, ambao hupelekwa China wanakouzwa kutokana na mapezi yao.

Ripoti inasema kwamba miaka miwili iliyopita pomboo hao aina ya ‘vaquita’ walikuwa wamebakia wamebakia 96, lakini sasa wako chini ya 30. Kutokana na sababu hiyo, pomboo hao wadogo watakuwa wametoweka kabisa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles