Leonard Mang’oha -Dar es salaam
MCHAKATO wa kupokea maoni na kujadili rasimu za kanuni za Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini (Latra), umeibua mvutano miongoni mwa wadau na kusababisha baadhi yao kususia kikao.
Mvutano huo uliibuka jana Dar es Salaam, katika kikao cha kujadili rasimu ya kanuni hizo kilichohusisha Latra, Jeshi la Polisi, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (Tadu), Chama cha Kutetea Abiria (Chakua) na wadau wengine vikiwamo vyuo na taasisi.
Uliibuka baada ya mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Aron Kisaka, kutoa nafasi kwa washiriki kupendekeza utaratibu ambao ungetumika kuwasilisha kanuni na kupokea maoni ya wadau.
Wakati hatua hiyo ikiendelea, Katibu Mkuu wa Taboa, Enea Mrutu, aliomba kutoa taarifa na akaomba kanuni hizo zisijadiliwe kwa sababu hawakupewa muda wa kutosha kuzipitia ili kupata maoni ya kutoa kama walivyoelezwa katika barua za mwaliko, kauli ambayo iliungwa mkono na wanachama wa Taboa, Tadu na baadhi ya wawakislishi wa vyama vingine.
“Tulipokea taarifa Ijumaa, Jumamosi muda wa kazi ni nusu siku, Jumapili ni mapumziko leo (jana), tunatakiwa tutoe maoni, muda huu haututoshi. Pia kanuni tulizopewa hapa ni za Kiswahili zile mlizotupatia ni za Kiingereza ambacho wengi hapa hawakijui.
“Kwa sehemu ndogo tuliyopitia, hizi kanuni zina mambo mengi magumu, kwanza ongezeni muda angalau siku 14 tuzipitie, pili badilisheni iwe kwa Kiswahili, ukiangalia humu kwa mfano wanasema mmiliki atatozwa asilimia 0.3 ya mapato yake bila kuangalia hasara wala nini,” alisema Mturu.
Licha ya kuahidiwa kupewa muda zaidi wa kutoa maoni katika vikao vingine vya kujadili kanuni hizo, baadhi ya wadau hao walionyesha kutokubali kwa madai kuwa tangu wakati wa Sumatra walikuwa wakiahidiwa kuwa watapewa muda zaidi, lakini hilo halikufanyika.
Mwenyekiti wa Tadu, Shaban Mdemu, alisema hali hiyo inaonyesha kuwa Latra haitaki kushirikiana nao kwani licha ya kupewa muda mfupi wa kupitia kanuni hizo, pia zina mambo mengi ya kumkandamiza dereva.
Baadhi ya wadau hao, hasa Taboa na Tadu walikataa hata kusaini fomu za mahudhurio kwa kile walichoeleza kuwa zitatumika kuonyesha kuwa wameshiriki kikao hicho, badala yake wakaamua kuondoka na kuwaacha wengine wakiendelea na madajiliano.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya wadau hao kususia kikao hicho, Mkurugenzi wa Huduma za Uchukuzi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Kisaka, alisema baada ya kupokea malalamiko yao walikubali kuwaongeza muda wa siku saba hadi 14 pamoja na kuwapa kanuni zilizoandikwa kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha kuzipitia na kuzielewa kisha wakutane tena.
Kisaka alisema kikao hicho kililenga kuwapa uelewa wadau na kwamba hata kama hawakuwa tayari kutoa maoni yao, wangewaruhusu kuyatunza na kuyawasilisha hapo baadaye.