26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

KANISA LAGOMA KUMZIKA BILIONEA WA NGURDOTO

Na WAANDISHI WETU-ARUSHA

KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Arusha limekataa kuendesha misa ya heshima ya mazishi ya mfanyabiashara bilionea katika sekta ya hoteli na utalii jijini hapa, Faustine Mrema kwa madai hakuwa na Sakramenti ya ndoa na mke wake wala Kipaimara.

Akizungumza na MTANZANIA   mjini hapa jana baada ya kuwapo  taarifa za Kanisa kugoma kumzika marehemu, Paroko Msaidizi Parokia ya Mtakatifu Theresia Mtoto Yesu, Padri Festus Mangwangi alisema ni kweli Mrema wakati wa uhai wake hakuweka heshima kwa kanisa

“Marehemu ni mkatoliki wa kuzaliwa, lakini hakuwahi kuwa na Sakramenti ya ndoa na mke aliyezaa naye watoto wala kupata kipaimara. Kanisa haliwezi kumzika kabisa, kawaida mazishi ya Kanisa Katoliki ni heshima inayotolewa kwa muhusika kama anastahili.

“Huyu hakuwahi kufunga ndoa kanisani, alijitenga na Kanisa kwa hiyo kusema tumemtenga si kweli, yeye ndiyo alijikataa hakutaka kutafuta heshima yake na kanisa akiwa hai,” alisema Padri Mangwangi.

Kuhusu kutokwenda kwenye Misa za Jumuiya ambayo nayo ni moja ya taratibu muhimu inayowataka waumini wa Katoliki kushiriki ibada za nyumba kwa nyumba, Padri Mangwangi alisema  hata ibada hizo nazo pia  alikuwa hashiriki.

“Jumuiya ni utaratibu wa Kanisa unaowataka waumini wawe na ushirika wa karibu ikiwamo kufahamiana, Mrema   pia alikuwa hashiriki,   sasa unaanzaje kumzika mtu kwa heshima za Kanisa Katoliki?.

“Ni sawa na wewe pale nyumbani kwako una mtoto umemsomesha akawa na maendeleo na uwezo mkubwa,   leo hii huwezi kuamka asubuhi ukamsalimia hiyo haiwezekani, bado yule ni mtoto wako anapaswa kukusalimia,” alisema.

Wakati Kanisa hilo likijivua kushiriki misa ya heshima ya maziko ya marehemu Mrema hiyo jana, Askofu Dk. Eliud Issangya wa Kanisa la Kanisa la International Evangelism Church ndiye aliyeongoza Ibada iliyofanyia ukumbi mkubwa wa mikutano wa Hoteli ya Ngurdoto wilayani Arumeru.

Akizungumzia waumini wasiokuwa na sakramenti za kanisa hilo ikiwamo kushiriki ibada za jumuiya, Padri Mangwangi aliwaonya viongozi wa madhehebu mengine ya Kikristo wanaojitokeza kuwazika waumini wa aina hiyo.

“Ni makosa kumzika muumini ambaye si wa kanisa lako, nimesikia kuna askofu sijui anadai eti marehemu alikwenda kwake kukiri makosa yake, hao ni maaskofu wenye njaa.

“Hivi unawezaje kumkosea kwa mfano Rais Dk. John Magufuli halafu ukaenda kuomba msamaha kwa Rais Yoweri Museven wa Uganda, haiwezekani. Mrema aliapaswa kuja kukiri na kusafisha imani yake kwa kanisa lake,” alisema Padri Mangwangi.

Katika mazishi hayo, viongozi mbalimbali   walihudhuria akiwamo Rais Mstaafu wa Awau ya Nne, Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.

Wengine ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Benard Membe, Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, James Mbatia, Balozi Mstaafu wa Tanzania nchini Nigeria, Daniel ole Njoolay, Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Mramba, huku Balozi David Kapya akimuwakilisha Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.

Mrema alianza kusumbuliwa na shinikizo la  miaka mitatu iliyopita tangu Mwaka 2014 hadi 2017  u na kutibiwa KCMC Moshi, AICC Arusha na Nairobi Kenya.

Juni mwaka huu alipelekwa Hospital ya Millpark  Afrika Kusini alikobainika kuwa na saratani ya mifupa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles