27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Kangomba yakimbiza wenyeviti wa vijiji

Na NORA DAMIAN-RUVUMA



BAADHI ya wenyeviti na watendaji wa vijiji katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wamekimbia makazi yao na kusababisha wake zao wakamatwe kutokana na kujihusisha na biashara ya kangomba.

Kangomba ni ulanguzi unaofanywa katika zao la korosho ambapo wahusika hutumia mbinu mbalimbali kama vile kununua korosho ikiwa kwenye maua, kununua kinyume na bei elekezi au kubadilisha kwa vitoweo na pembejeo.

Akizungumza jana, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera alisema katika operesheni inayoendelea, juzi walikamatwa watu wanane wakiwemo wake wa viongozi wa vijiji.

“Tulifanya operesheni katika vijiji vya Liwanga, Mkotamo na Misechela vilivyoko Tarafa ya Namasakata, Kata ya Misechela. Tuliwakamata watu wanane wakiwa na roba 15 na mifuko midogo ambayo uzito wake jumla ni tani mbili,” alisema Homera.

Kuhusu wake wa viongozi wa vijiji, alisema walikamatwa baada ya waume zao kukimbia na kwamba wengine walikutwa wakipima korosho majumbani mwao saa 9 usiku.

Alisema viongozi wa vijiji waliokimbia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Misechela kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Mtendaji wa kijiji hicho, Mtendaji wa Kijiji cha Liwanga na karani wa Chama cha Msingi cha Liwanga ambaye naye amekimbia.

Homera alisema katika nyumba ya mtendaji mmoja kulikutwa viroba tisa vya korosho na nyumba nyingine kimoja.

DC huyo alisema Mtendaji wa Kijiji cha Liwanga, alikutwa akikusanya korosho kwa wakulima – kilo 30 kwa kila mfuko mmoja wa sulphur.

“Walisambaza sulphur sasa walikuwa wanakusanya mzigo, na kilo 30 kwa kila mfuko mmoja wa sulphur maana yake ni kwamba wanamwibia mwananchi Sh 99,000,” alisema.

Alisema wananchi wengine waliokamatwa walitiliwa shaka baada ya kupeleka mzigo ambao haulingani na uwezo wa mashamba yao.

Kati ya wananchi hao wako waliokutwa na viroba vitano, kilo 503 na mwingine alipeleka kilo 831.

 

WAKULIMA WALIOLIPWA

Wakulima waliolipwa fedha zao katika Kijiji cha Mtonya wilayani Tunduru waliipongeza Serikali kwa usimamizi mzuri wa malipo ambao umewaongezea imani ya kuzalisha zaidi.

Mmoja wa wakulima hao, Issa Msanjo (48) ambaye alipata kilo 1,600 alisema ataongeza juhudi kwenye uzalishaji ili apate mazao mengi zaidi.

“Kwa kweli namshukuru mheshimiwa rais, nimelipwa fedha zangu zote bila kukatwa, tena ngoja nipige magoti (anapiga magoti) kumshukuru Rais Magufuli kwa hiki alichotufanyia,” alisema Msanjo.

Hata hivyo mkulima huyo aliiomba Serikali kuangalia upya gharama za pembejeo, hasa sulphur ambayo ni muhimu katika kilimo cha korosho.

Mkulima mwingine, Ester Mchopa (58) alisema mwaka huu alilima heka moja iliyomwezesha kuvuna kilo 57.

“Nina shamba la heka 10, lakini nililima heka moja tu, lakini kwa hamasa tuliyoipata mwaka huu nitafufua heka nyingine moja,” alisema Mchopa.

Naye Shaibu Said, ambaye alipata kilo 405, alisema kwa sasa hatokuwa na hofu kwani hata akivuna korosho nyingi ana uhakika zitanunuliwa.

Hadi sasa katika Wilaya ya Tunduru tayari wakulima 534 wamelipwa Sh milioni 550.7.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles