26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Ni kazi ngumu kurejesha mali za Waislamu-Mufti

NA VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM



MUFTI wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, ameeleza jinsi baadhi ya viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) wanavyopigwa vita na namna wanavyokabiliana na  ugumu katika kurejesha mali za waislamu nchini.

Alikuwa akizungumza katika Baraza Kuu la Maulid  lililofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga jana.

Mufti Zubeir alisema pamoja na mambo yote yanayojitokeza kamwe baraza halitarudi  nyuma katika kuhakikisha mali zote zinarejeshwa.

“Wapo baadhi ya viongozi waliokuwa BAKWATA tangu 1968 hawakufanya jambo miaka 47, wameingia wa sasa ndani ya miaka mitatu tu, utashangaa.

“Pale mezani kwangu ofisini kuna makaratasi yamejaa, muondoe sheikh fulani wa mkoa ule hafai, muondoe katibu fulani wa wilaya hafai, muondoe sheikh wa wilaya hafai.

“Sasa utashangaa hawa wamekaa kwa muda kidogo tu na wanafanya kazi… ingekuwa mimi mwendawazimu usingekuta sheikh yeyote hapa hata mmoja.

“Lakini ndiyo haya anayozungumza Rais Magufuli, kwetu kumenoga, rudini, Bakwata kumenoga, imekuwa nzuri sasa kila mmoja uongozi anautaka, uongozi si ndiyo wewe uliyehujumu!

“Umeuza mali, umeuza kila kitu tunapata tabu kuzirudisha sasa hivi tunazunguka huko mikoani hatulali, hawa masheikh wanazunguka mikoani huko kwa sababu ya ile ile mijitu, tunaifahamu si kwamba hatuwajui.

“Tunamjua mmoja baada ya mwingine, ipo siku nitawaita, sisi tunaendelea na tunazidi kuiombea serikali yetu na umma uwe na maadili mema,” alisema.

Mufti Zubeir pia aliwaalika Watanzania katika sherehe za miaka 50 ya Bakwata zitakazofanyika Dar es Salaam Desemba 17, mwaka huu.

“Yanasemwa mengi mno huko, siku hiyo tutaeleza kila kitu kuhusu Baraza kila mmoja akitoka pale atakuwa na moyo mweupe na atakuwa amejua kwa nini baraza hili lilianzishwa.

“Mshikamano ni suala muhimu la kusisitizwa kwa taifa lolote linalohitaji kupata maendeleo.

“Masheikh na maimamu kila mmoja kwa nafasi yake anayo nafasi ya kuhimiza mambo haya lakini pia ni lazima tujenge uwezo wa kujitegemea kwa uchumi kwa kila mmoja kwenye madrasa na misikiti yetu.

“Dini na uchumi vitatupeleka mbele, ni uwongo mtu kuhubiri dini tu na kuacha uchumi, utaelewa mantiki ya maneno haya ukisoma quran tukufu utaona kuna aya nyingi zinahimiza uchumi, lazima tufanye kazi, lazima tuwe wamoja” alisisitiza kiongozi huyo.

Aliongeza: “Ikiwa tunataka kumfuata Mtume Muhamad, amehubiri sana umoja, mnaijua vema historia yake kutoka Makka hadi Madina, fanyeni kazi hii kwa uadilifu na weledi mkubwa.

“Stilafu (tofauti) zisitugawe, tumekubali kuwa mapande mapande, kila mmoja anatetea timu yake huyu anatetea jambo lake, msikiti wake, Uislamu haupo hivyo.

“Uislamu Tanzania inatazamwa na nchi zote zilizotuzunguka, napata salamu kutoka nchi nyingi, wanatupongeza, sisi lazima tuonyeshe mfano kumuiga Mtume Muhamad,” aisema.

Mufti  ambaye pia ni Sheikh Mkuu wa Tanzania alisema pamoja na hayo, Baraza hilo linatarajia kujenga Chuo Kikuu cha Kiislamu wilayani  Korogwe Mkoa wa Tanga na mipango imeshaanza na inaendelea vizuri.

 

SALAM ZA JPM

Akizungumza kwa niaba ya Rais John Magufuli, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo, alimpongeza Mufti Zabeir kwa kuwaunganisha waislamu na uongozi ulio imara.

“Tunashuhudia kazi unayoifanya tangu umepewa kuongoza nafasi hiyo, Mungu anakupa nguvu kusimamia, umekuwa kiongozi wa mfano, una dira, msimamo na mtazamo wako ni wa pekee.

“Binafsi nimeshuhudia umma wote wa kiislamu wakizungumza  karibu asilimia kubwa wana lugha moja na hii ni kwa sababu ya uongozi wako.

“Hivi karibuni, ukiangalia weledi wako wa kutenda kazi na uhusiano, dalili njema inajionyesha… ukifika Kinondoni, majengo yanayojengwa chini ya uongozi wako na msaada mkubwa wa Rais Magufuli kama kuna ambao hawajafika Makao Makuu ya Bakwata (Kinondoni) ikifika Februari (mwakani) watapotea wasijue ndipo yalipokuwa.

“Hili lote linatokana na uadilifu, bila uadilifu haiwezekani, hatuwezi kupata mafanikio mahali popote, leo hii nikikuangalia unavyosimamia kuhakikisha mali zote zilizopotea ama kwa ufisadi wa wachache ambao kwa njia moja au nyingine walipewa dhamana wakamuweka Mungu pembeni wakajali masilahi yao ya muda mfupi.

“Leo hii tunaona jinsi unavyosimamia kuhakikisha zinarudi,” alisema.

Waziri Jafo alisema katika awamu hii ya tano Tanzania imepata neema ya kuwa na viongozi waadilifu akiwamo Mufti Zubeir na Rais Magufuli.

“Hii ni neema lakini kuna ambao bado hawajui jambo hili, viongozi hawa ni neema tumepewa na Mwenyezi Mungu, nchi ilikuwa mifugo inakufa yenyewe, nilienda Longido hali ya ukame ilikuwa mbaya.

“Ndani ya miaka mitatu tutathmini yapi tunaona, hadi mazao mengine yanakosa ununuzi, hii ni neema kubwa tuliyojaliwa, naamini in kutokana  na uadilifu wa viongozi tuliowaweka madarakani.

“Hata makusanyo ya mapato huko nyuma ilikuwa wastani wa Sh bilioni 800 kwa mwezi sasa imefikia Sh trioni 1.3, hii ni neema kubwa lakini kuna binadamu ambao hawafurahi wale ambao mianya ile ilikuwa kwao fursa.

“Tulikuwa na watoto ambao hawakuwa na uwezo wa kwenda shule sababu ya michango, Serikali imeweka Sh bilioni 20.85 kuwezesha watoto wa maskini wapate elimu.

“2016 tuliwaosajili wengine walivuka miaka saba, usajili uliongezeka hadi kufikia milioni mbili, ndiyo maana tulikuwa na shida ya madarasa na madawati.

“Hii ni kazi kubwa serikali inatoa elimu bure kwa sababu uadilifu umetawala,” alisema.

Jafo alisema serikali imepanga kufanya maboresho makubwa katika shule kongwe 89 na  45 tayari zimekarabatiwa kwa zaidi ya Sh bilioni 53.

“Kwa upande wa afya, waziri alisema bajeti ya dawa imeongezwa kutoka Sh bilioni 31 mwaka 2015 hadi kufikia Sh bilioni 269 na hospitali 69 mpya zinajengwa kote nchini,” alisema.

BAKWATA NA AMANI

Awali, akisoma hotuba ya Maulid kwa mgeni rasmi, Kaimu Katibu Mkuu wa Bakwata, Nuhu Jabir, alisema  Mtume Muhammad (S.A.W) alihubiri haki na kukemea uovu na dhulma katika jamii.

Alisema  alihimiza amani, umoja na mshikamano baina ya Waislamu wote na kuulinganisha umoja na mshikamano wao kuwa sawa na viungo vya mwili wa mwanadamu au kuta za jengo moja namna zinavyotegemeana na kuimarishana.

“Kupitia hadhara hii na kupitia funzo hili adimu alilotufundisha Mtume Muhammad (S.W.A) BAKWATA inawahimiza Waislamu wa Tanzania kuimarisha umoja na mshikamano baina yao kwa yale yote yenye maslahi kwa Waislamu, Uislamu na jamii kwa ujumla,” alisema.

Alisema Baraza chini ya uongozi wa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir Bin Ally  wanatarajia kwamba umoja na mshikamano kati ya Waislamu na Waislamu, Waislamu na wasiokuwa Waislamu na ule wa baina ya taasisi na taasisi utaimarika zaidi kwa kuweka mbele na kutegemea sira na mwenendo wa Mtume Muhammad (S.A.W) kutekeleza mafundisho ya Qur’aan.

“Umma wa Kiislamu unapaswa kueneza uadilifu, utulivu na amani kote nchini na kwingineko duniani kwa kutegemea aya ya 103 ya Surat Alimran inayotuamuru Waislamu kushikamana na tusifarakane.

“Iko haja kwa jamii ya Kiislamu kukumbushana na kuhimizana juu ya wajibu wa kuenzi na kulinda mila, silka, desturi na utamaduni wa Kiislamu.

“Katika kuuenzi utamaduni wa Kiislamu na silka zake kwa Waislamu wa Tanzania, hakuna budi kwetu kama wazazi kuwasomesha watoto wetu   wajue elimu zote pamoja na historia ya Uislamu wetu,” alisema.

Alisema jukumu la kuwalea watoto katika maadili mema ni la kila mzazi na wale wote wanaohusika katika jamii.

“Ni jukumu letu wazazi kuhakikisha  haki za watoto zinalindwa.  Pia kuhakikisha watoto wa kike na wa kiume hawabaguliwi katika suala la elimu.

“Tujitahidi   kuhakikisha watoto wetu wanapata elimu ya msingi na elimu ya juu bila kuwakatisha ndoto zao.

“Elimu kwa watoto wote bila ubaguzi wa jinsia kutalipatia taifa letu la Tanzania warithi wa maadii mema ambayo ndiyo ndoto ya kila Mtanzania, milele.

“Tunawaasa wazazi wote na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wote wanapata elimu bila kukatishwa kwa sababu yoyote ile,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles