30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, December 9, 2021

Waziri Mkuu azindua msikiti Ruangwa

Na MWANDISHI WETU-RUANGWAWAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezindua msikiti wa Nandagala na amewataka waumini wa dini ya Kiislamu katika Kata ya Nandagala wilayani hapa wautumie vizuri kwa kufanya ibada na kuhamasisha amani na si vinginevyo.

Akizindua msikiti huo juzi, aliwasisitiza waumini wa dini ya Kiislamu kuhakikisha muda wa kufanya swala unapofika waende msikitini hapo kufanya ibada.

“Msikiti huu ninauzindua leo (juzi) naomba tuutunze vizuri na tuutumie kwa kufanya ibada na si ibada za kiuanaharakati. Watakaokuja msikitini na kufanya mambo ya hovyo Mwenyezi Mungu atawalaani,” alisema

Majaliwa aliwataka waumini hao waanzishe madrasa na kuwafundisha watoto Quran lengo likiwa ni kuwafundisha misingi ya dini na kuwaandaa vizuri na kuwawezesha kukua kiimani ili waje kuwa waja wema.

Alimshukuru Mzee Suleiman Mamboleo na familia yake kwa uamuzi wao wa kujitolea kujenga msikiti huo ambao utawawezesha waumini katika Kijiji cha Nandagala kufanya ibada zao.

“Namshukuru na Mzee Mamboleo na mkewe kwa kutoa eneo lao bure ili litumike kujengea msikiti,” alisema.

Kwa upande wake Sheikh Hilal Kipozeo ambaye alihudhuria uzinduzi wa msikiti huo, aliwasisitiza waumini wa dini ya Kiislamu watumie muda mwingi kufanya ibada na wajiepushe na vitendo vyenye kumuasi Mwenyezi Mungu na wadumishe amani.

“Mtume Muhammad (S.A.W) baada ya kutoka katika mji wa Makka na kuhamia Madina kitu cha kwanza alijenga msikiti ili watu waweze kumwabudu Mwenyezi Mungu, alijenga soko ili watu washiriki shughuli za kiuchumi na alifanya upatanishi kwa makabila mawili kwa lengo la kuonesha kuwa kuishi kwa amani ni kitu bora,” alisema.

Wananchi na waumini wa dini ya Kiislamu katika Kijiji cha Nandagala walimshukuru mfadhili aliyejenga msikiti huo kwa sababu utawawezesha kuwa na eneo la kufanyia ibada baada ya lile la awali kubomolewa kwa kuwa walijenga katika hifadhi ya barabara.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,702FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles