25.9 C
Dar es Salaam
Saturday, November 2, 2024

Contact us: [email protected]

Kamati ya saa 72 ni jipu lililoiva TFF

malinziNA ZAINAB IDDY

KWA lugha nyepesi si vibaya kusema soka la Tanzania limefika mwisho na hakuna muujiza unaoweza kufanyika ili lisonge mbele.

Kila kukicha kumekuwa na malalamiko mengi viwanjani, sababu kubwa ikiwa ni waamuzi kushindwa kutumia sheria 17 za mchezo, viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kufanya mambo kulingana na maslahi ya timu wanazozishabikia, vitendo vya rushwa, upangaji matokeo na mengineyo yanayochafua taswira ya soka nchini.

Jambo hili linaonekana kuzidi kulididimiza soka la nchini,  si vibaya tukisema lipo kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Mbali ya kuwepo kwa Ligi Daraja la Kwanza, soka la Tanzania limebebwa na Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo inatoa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ huku ikiwa ndiyo Ligi inayoendeshwa kwa magumashi makubwa.

Ni vipi soka la Tanzania litasonga mbele iwapo kila kukicha kunasikika na kuonekana matukio yanayokatisha tamaa? Kwa sasa figisu figisu zimeonekana kushika hatamu kuliko maendeleo ya soka, malalamiko ya waamuzi kutotumia sheria 17, kupigwa kwa waamuzi viwanjani, uharibifu wa mali za uwanjani limekuwa ni jambo la kawaida.

TFF ndicho chombo chenye dhamana ya kusimamia mchezo huo nchini, na katika hilo imeunda kamati ndogondogo kwa ajili ya kusaidia kusimamai soka, ikiwemo Kamati ya saa 72.

Kiuhalisia Kamati ya saa 72 ndilo jipu kubwa ndani ya TFF, kwani inaongoza kwa kufanya madudu yanayozidi kushusha hadhi ya soka.

Ukiiangalia kwa jicho la tatu kamati hiyo utabaini kuwa ipo kwa ajili ya kuzilinda timu fulani kulingana na matakwa ya mabosi waliopo TFF.

Ni jambo la kushangaza pale timu fulani inapofanya vitendo kinyume cha sheria za soka ikafumbiwa macho, huku nyingine ikifanya jambo kama hilo ikapewa kipaumbele na kutatuliwa kwa haraka masuala yake.

Hali kama hiyo inasababisha kujengeka kwa dhana potofu  miongoni mwa wanachama wa TFF,  kuwa wanaonewa  kwa makusudi ili kuwalinda wengine,  huku wale wanaodaiwa kulindwa wakiongeza kiburi cha kufanya wanachotaka.

Yapo mengi yanayojitokeza, lakini kamati hii imekuwa kimya na hivyo kupoteza heshima yake na hadhi ya wanaounda kamati hiyo.

Ufike wakati kamati hiyo ifanye kazi zake pasipo kuingiliwa majukumu na watu waliopo nje, lakini pia  waweze kufanya kazi ipasavyo kwa kutenda haki na kufuata sheria za soka bila kuangalia timu hii inamhusu kiongozi gani wa TFF.

Lakini pia kama haiwezi kufanya kazi zake kikamilifu, Kirohoo safi inasema haina haja ya kuwepo, kwani tayari inaonekana ni jipu lililoiva na linalohitaji kutumbuliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles