26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kamati ya Lugumi yaanza uchunguzi, mazito yaibuka

jobNA Waandishi Wetu, Dodoma/Dar

KAMATI ndogo ya uchunguzi ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeanza kazi ya kukagua utekelezaji wa mkataba kati ya Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises Limited, huku wajumbe wake wakishuhudia mambo mazito.

Chanzo cha kuaminika kiliambia MTANZANIA mjini Dodoma jana, kuwa kamati hiyo imeanza kazi kutokana na agizo la Spika wa Bunge, Job Ndugai la kutaka uchunguzi zaidi ufanyike ili kubaini ukweli wa sakata hilo.

Katika sakata hilo, Kampuni ya Lugumi inadaiwa kupewa tenda na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Hadi sasa mashine hizo zimefungwa katika vituo 14 tu vya polisi wakati kampuni hiyo tayari imelipwa Sh bilioni 34 ambazo ni asilimia 99 ya fedha za mkataba.

Kamati hiyo imeanza kazi juzi kwa wajumbe wake kugawanywa katika makundi matatu, huku kundi lililoanzia kazi Mkoa wa Morogoro likibaini kuwa hakuna mashine hizo.

“Kamati imeanza kazi, tupo makundi matatu. Jana (juzi) kuna wenzetu wengine wameanza kazi kuanzia mikoa ya Morogoro, Iringa, Mbeya, Rukwa, Katavi, Kigoma na mwisho tutarejea hapo Dodoma.

“Kundi la pili, linaanzia kazi Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Tanga, Kilimanjaro na Arusha, wakati kundi la mwisho mikoa ya Kanda ya Ziwa,” kilisema chanzo chetu.

Chanzo chetu kilisema baada ya kamati kufika mkoani Morogoro ilibainika baadhi ya vituo vya polisi hakuna mashine hizo, licha ya taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mkataba huo, kuonyesha kuna mashine.

Inaelezwa pamoja na hali hiyo, baadhi ya maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi wamekuwa wakihaha kuweka mambo sawa kwa lengo la kuficha ukweli kuhusu sakata hilo.

“Unajua mkataba wa Lugumi ni jambo zito, kuna hatari likaondoka na mtu pindi taarifa itakapowasilishwa bungeni, tunajua wapo baadhi ya viongozi wa upinzani wamekuwa wakionywa (wakiwekwa sawa) na viongozi wa Serikali ili kuficha ukweli katika hili, kamati yetu tutaeleza ukweli na kila kitu kilichojiri,” alisema mtoa habari wetu.

 

KUKWAMA KAMATI

Tangu kamati hiyo ilipoundwa, ilishindwa kuanza kazi zake kwa mujibu wa taratibu kutokana na kukosa fedha.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM) na wajumbe wake wanane, itakwenda kila kona kilipo kituo cha polisi kubaini ukweli na thamani ya fedha kama inalingana na uhalisia wa mashine hizo.

Mbali na kufanya uchunguzi huo, kamati hiyo itawahoji vigogo wote waliotajwa katika mkataba huo na na kampuni zilizoshiriki, na baada ya kazi kukamilika itawasilisha matokeo bungeni kwa ajili ya uamuzi.

Wajumbe wa Kamati hiyo ndogo ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ni Dk. Haji Mponda (Malinyi-CCM), Mbunge wa Dimani, Hafidhi Ali Tahir (CCM) na Mbunge wa Nyamagana, Stanlaus Mabula (CCM).

Wengine ni Mussa Mbaruku (Tanga Mjini-CUF), Tunza Malapo (Viti Maalumu-Chadema), Naghenjwa Kaboyoka (Same Mashariki-Chadema) na Mbunge wa Viti Maalumu, Khadija Nassor Ali (Chadema).

Kamati hiyo ambayo imeanza kazi juzi, itafanya kazi zake kwa siri  kwa mwezi mmoja, na pamoja na mambo mengine, imekabidhiwa hadidu rejea ya namna itakavyofanya kazi hiyo,

Wakati PAC ilipokutana na maofisa wa Jeshi la Polisi kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ilibainika kuwa zabuni ya tenda hiyo ilitangazwa Septemba 22, 2011 na mkataba ukasainiwa siku iliyofuata Septemba 23.

“Halafu jambo jingine linaloshtua, tangu wakati huo mashine zote wanasema zipo, lakini hazifanyi kazi,” alisema Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly.

Kamati hiyo pia imebaini tofauti ya fedha katika mkataba huo ambako wakati taarifa ya Jeshi la Polisi inaonyesha walitoa Sh 37,163,940,127.7, taarifa ya CAG inaonyesha fedha zilizotolewa ni Sh 37,742,913.007 ikiwa na tofauti ya Sh milioni 500.

 

MIKOANI

Taarifa kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Geita na Dodoma, zinasema vifaa vinavyodaiwa kuwa mashine za kuchukua alama za vidole zimepelekwa katika vituo mbalimbali vya polisi.

Vyanzo vyetu kutoka katika mikoa hiyo, vinasema licha ya mashine hizo kupelekwa hakuna wataalamu wa kuzifunga na kuzitumia.

“Tunaona tumeletewa mitambo, tunaambiwa ni kwa ajili ya kuchukulia alama za vidole, sasa tunajiuliza wataalamu wa kuitumia wako wapi?

“Sijawahi kuona askari wetu hapa Dodoma wamepelekwa kupata mafunzo ya namna ya kutumia mashine hizi… jambo hili ni zito labda mumcheki afande IGP ndiye anaweza kuwa na maelezo mazuri,” kilisema chanzo chetu kutoka mkoani Dodoma.

Kutoka mkoani Geita chanzo chetu kilisema: “Unajua hili ni agizo kutoka mamlaka za juu, mashine zimefika hapa Jumatano iliyopita, siku iliyofuata zikafungwa.”

 

IGP MANGU

Hata hivyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu aliiambia MTANZANIA Dar es Salaam jana kuwa hakuna hata kifaa kimoja cha Kampuni ya Lugumi kilichopelekwa kwenye ofisi au vituo vya polisi kwa ajili ya kufungwa.

Alisema laiti kungekuwa na vifaa hivyo, kamati iliyoundwa na Bunge ikishirikiana na wajumbe kutoka ofisi ya mhakiki mali za Serikali ili kufanya ukaguzi wa vituo ambavyo vimefungwa na vilivyokuwa bado ingevibaini.

“Hakuna kitu kama hicho, wanaosema wana sababu zao binafsi ambazo zinapotosha umma.

“Kama kungekuwa na vifaa katika vituo hivyo, wajumbe wa kamati ile wangeviona na kutuambia, lakini mpaka sasa hakuna kitu kama hicho na wajumbe hao bado wanaendelea na kazi yao.

“Kuna watu kazi yao kutoa taarifa za uongo ili kuchafua taasisi, ninachokwambia hakuna kifaa kilichopelekwa katika vituo hivyo mpaka sasa,” alisema IGP Mangu

Alisema kama waandishi hawataamini maneno hayo, wanapaswa kuwatafuta wajumbe wa kamati hiyo ili waweze kuwaeleza ukweli kuhusu taarifa hizo kwa sababu walipita kwenye vituo hivyo na kujionea kwa macho kilichopo.

Awali, Lugumi alidai hahusiki na tuhuma zinazoelekezwa kwake kwa sababu mkataba huo aliutekeleza kwa kushirikiana na wabia wake.

Alisema kama kuna mgogoro katika utekelezaji wa mkataba huo, jeshi hilo lilipaswa kuwasilisha taarifa ya malalamiko kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili aweze kuingilia kati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles