23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Saratani ya kizazi tishio kwa wanawake nchini

NA HERIETH FAUSTINE, DAR ES SALAAM

ZAIDI ya asilimia 69 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa wana virusi vya Human Papilloma Virus (HPV) vinavyosababisha ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.

Pia zaidi ya asilimia 80 ya wanawake wenye ugonjwa huo hufariki dunia ndani ya miaka mitano kutokana na kutopatiwa matibabu mapema.

Hayo yalisemwa juzi na mtaalamu wa magonjwa ya saratani kutoka katika Asasi isiyo ya Kiserikali ya Tanzania Social Outreach Initiative (TASOI), Dk. Walter Kweka, wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya magonjwa ya saratani.

Alisema ugonjwa huo huwashambulia wanawake ambao walianza mahusiano katika umri mdogo pamoja na wanawake wenye mpenzi zaidi ya mmoja ambao wanafanya ngono bila kutumia kinga pamoja na kansa ya kurithi kutoka katika ukoo.

“Kwa Tanzania inakadiriwa kuwa na wanawake zaidi ya milioni 14 walioko katika umri wa kuzaa ambao ni kati ya miaka 18 hadi 45, wako katika hatari kubwa ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.

“Tafiti mbalimbali zinaonyesha kila mwaka kuna wagonjwa wapya 7,304 na 4,216 kati yao hufariki dunia kwa ugonjwa huo kutokana na virusi vya HPV, hivyo kila mwanamke aliyefanya ngono bila kutumia kinga ana hatari ya kupata saratani hii kama hana utaratibu wa kuchunguza afya yake,” alisema Dk. Kweka.

Kuhusu saratani ya matiti, alisema ugonjwa huo huwashambulia zaidi wanawake, na kwamba inakadiriwa kuwa katika Afrika Mashariki wagonjwa wapya kwa mwaka hufikia 18,000 na kati yao 10,000 hufariki dunia.

“Utafiti uliofanywa mwaka 2008 hapa nchini kulikuwa na wagonjwa wapya 2,500 ambao waligundulika na saratani ya matiti, lakini 300 ndio waliopatiwa tiba katika Hospitali ya Ocean Road Dar es Salaam,” alisema.

Alisema zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wanaofika hospitali wanakuwa wamechelewa ambapo hufika katika hatua ya 3B na hivyo kushindwa kupona.

Dk. Kweka alisema katika idadi hiyo asilimia mbili hadi saba ya saratani ya matiti huwakumba wanaume.

Kuhusu saratani ya tezi dume ambayo imekuwa ikiwashambulia wanaume wenye umri wa miaka 55 hadi 70, alisema husababishwa na ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi pamoja na nyama nyekundu.

“Kwa hapa nchini tafiti zinaonyesha kuwa kati ya wanaume 1,200 na 1,300 hugundulika na ugonjwa wa saratani ya tezi dume kwa mwaka na wanaume waliokuwa na shida za mkojo waligundulika kuwa na ugonjwa huu,” alisema Dk. Kweka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles