KAMATI mpya iliyoundwa kwa ajili ya kuandaa, kuendesha na kusimamia Shindano la Miss Tanzania imejitoa rasmi
jana kufanya shughuli hizo za kikamati kutokana na sababu mbalimbali.
Kamati hiyo iliundwa Agosti, mwaka jana ikiwa na wajumbe 12 ambao ni Juma Pinto, Lucas Ritta, Doris Mollel, Jokate Mwegelo, Hoyce Temu, Mohamed Bawazir, Gladyz Shao, Magdalena Munisi, Shah Ramadhani, Hamm Hashim, Khalfan Saleh na Ojambi Masaburi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa kamati hiyo, Juma Pinto alisema wamefikia uamuzi huo mara baada ya kutokuridhishwa na hali ya utendaji ya Kampuni ya Lino International Agency.
“Tumekuja kutoa taarifa kwamba, kama tulivyoteuliwa na Lino, kuandaa, kuendesha na kusimamia mashindano ya
Miss Tanzania, kamati yangu imeamua kujitoa kutokana na majukumu ya kamati kuingiliwa na kampuni ya Lino,”
alisema Pinto.
Aliongeza kuwa makubaliano yao na Lino yaliwataka kampuni hiyo kuwa washauri tu na kuiachia kamati mpya ifanye kazi kitu ambacho kwa muda mrefu kimeshindikana.