32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

KAMATI KUU CCM YAMPITISHA CHIZA BUYUNGU

PATRICIA KIMELEMETA – Dar es Salaam


KAMATI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imepitisha jina la Mhandisi Christopher Chiza kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma.

Kamati hiyo ambayo iliongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli, ilipongeza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kwa maendeleo.

Uamuzi huo umekuja baada ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Mwalimu Kasuku Bilago (Chadema), kufariki dunia Mei 26, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole, ilisema katika kikao hicho, wajumbe walimpongeza Rais Magufuli kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama hicho ambayo imeleta maendeleo kwa wananchi wa Tanzania bila ya kujali itikadi zao.

“Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kwa pamoja kimepitisha jina la Christopher Chiza kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Buyungu, tuna imani mgombea wetu anauzika, tutapita kwa wananchi ili tuweze kumnadi,” alisema Polepole.

Alisema licha ya kupitisha jina hilo, lakini pia wajumbe wa kamati hiyo wamempongeza Rais Magufuli kwa kuleta maendeleo kwa wananchi, hususani katika huduma za kijamii na kiuchumi.

Polepole alisema hali hiyo imeonyesha wazi kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM inatekelezwa kwa vitendo hali ambayo imechangia kuleta maendeleo kwa wananchi.

Alisema lakini pia kamati hiyo imepokea na kupongeza taarifa ya kuwasili kwa ndege aina ya 787-8 Drimliner itakayokodishwa kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Polepole alisema kamati hiyo pia imempongeza Rais Magufuli kutokana na uamuzi wake wa kukutana na viongozi wastaafu wa kitaifa na kufanya nao mazungumzo pamoja na kupokea ushauri wao.

Alisema kutokana na hali hiyo, kamati hiyo imetafakari kwa kina na kuweka mjadala mpana juu ya mageuzi yanayofanyika katika chama na jumuiya zake, lakini pia Serikali na taasisi zake.

Polepole alisema wajumbe kwa pamoja wameridhishwa na kuona jitihada zinazofanywa zimeweza kuongeza tija, ufanisi na faida kwa wananchi na kuongeza uadilifu, utumishi wa watu.

Alisema Serikali imeweza kupambana na vita dhidi ya rushwa na kupunguza vitendo vya ubadhirifu wa mali za chama na umma kwa ujumla wake.

Polepole alisema shughuli za uchapakazi katika chama na Serikali zinaendelezwa maradufu ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles