32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

KAMA SIYO HARMONIZE, HARMORAPA ANGEKUWA WAPI?

Na JOSEPH SHALUWA

UKIMSIKILIZA kwa makini msanii Rajab Ibrahim ‘Harmonize’ kutoka Lebo ya Wasafi Classic Baby ‘WCB’, kisha Nasibu Abdul ‘Diamond’ ni kama unamsikiliza mtu mmoja tu – Diamond.

Harmonize ameshindwa kabisa kutafuta identity yake. Ni kweli anajua kuimba, anajitahidi kuvaa na kuishi kisanii, lakini ndani yake anaonekana Diamond. Niseme ukweli kuwa lebo aliyopo ni sahihi na ndiyo maana hata kazi zake ni nzuri.

Tatizo ni namna ya kujitofautisha yeye na Diamond. Kama hujawahi kufutilia kwa makini, jaribu leo. Sikiliza kibao Niambie cha Harmonize, kisha msikilize Diamond kwenye Marry You na nyimbo nyingine nyingi utaelewa ninachosema.

Hata staili yake ya kutoka, ametumia ya Diamond. Enzi za Diamond wakati akianza kuchomoza, alijikuta kila uhusiano anaokuwa nao unampa kiki.

Wakati huo alivuma akitoka na Jacqueline Wolper, msanii wa filamu za Kibongo ambaye kwa sasa eti anatoka na Harmonize – demu wa zamani wa bosi wake. Kwamba, kwa sasa Diamond atalazimika kumuita Wolper shemeji!

Ipo listi ya mastaa waliotoka na Diamond na kumpa kiki kubwa kwenye vyombo vya habari. Tuyaache hayo – kwa sasa Diamond ametulia na Zarina Hassan ‘Zari’, msanii kutoka Uganda.

Ukifuatilia kwa makini zaidi, utagundua staili ya Harmonize kama haimpotezi, basi inamuacha hapo alipo bila kusonga mbele kwa sababu hakuna kipya kinachofika kwa mashabiki, badala yake anakuwa kama  Diamond B!

 

TUCHEKI NA HARMORAPA

Chipukizi kutoka Mtwara, Harmorapa amegueuka habari ya mjini kwenye mitandao ya kijamii na majarida ya burudani nchini. Harmorapa anajipapambanua kuwa anafanana na Harmonize. Kwanza ijulikane siyo dhambi watu kufanana, kujifananisha au kufananishwa.

Hata hivyo Harmonize atabaki kuwa Harmonize na Harmorapa atabaki kuwa yeye, hawawezi kuwa sawa, ingawa wanafanana kidogo.

Harmorapa alipofahamu kuwa kidogo anafanana na Harmonize, akaona tayari ni fursa kwake. Haraka akaamua kutoka Mtwara na kuja jijini Dar es Salaam kujaribu bahati yake ya muziki.

Ameingia jijini kwa kiki ya kufanana na Harmonize na hata jina lake, ni kama ameligeuza kidogo tu ili kuwe na mfanano na Harmonize.

 

KIKI, KUJIONGEZA

Ukimsikiliza Harmorapa anavyoimba, hata kidogo huwezi kumfananisha na Harmonize. Kwanza Harmorapa anarap, wakati Harmonize anaimba. Ni watu wawili tofauti kabisa.

Alichochukua Harmorapa kwa Harmonize ni ule mfanano wao na kuchezesha jina tu. Ameingia na staili mpya kabisa. Harmorapa anatufundisha kuwa kiki siyo lazima ihusishwe na skendo za kutengeneza kama wanavyofanya baadhi ya wasanii.

Tukio lolote linalotokea mjini, Harmorapa analichukulia kama mtaji wa kuzidi kujitanua kisanii. Wakati wadau mbalimbali wa habari na sanaa  wakifika katika ofisi za Clouds Media kutoa pole baada ya tukio lililotokea hivi karibuni, likimhusisha kiongozi mmoja kuingilia utaratibu wa kazi katika studio hizo nyakati za usiku, Harmorapa alikuwa miongoni mwa wasanii wa awali kufika.

Alifika akiwa amevalia nadhifu na alifanya mahojiano na vyombo vya habari. Hata pale aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alipokuwa na mkutano na waandishi wa habari, kuzungumzia kuondolewa kwake kwenye nafasi hiyo, naye alifika.

Harmorapa alijua kwenye mkutano ule, lazima kungekuwa na kamera za waandishi wa habari, hivyo aliwahi na kujisogeza karibu na Nape ili kamera zimuumulike, lakini pia ikitokea nafasi ya kuhojiwa iwe hivyo.

Bahati mbaya iliyogeuka nzuri, Harmorapa alitimua mbio baada ya kuona bastola ikitolewa na aliyedhaniwa kuwa ni askari kanzu. Ikawa kiki kwa Harmorapa.

Bila kuelewa kumbe mbio zile ndiyo zikageuka habari ya mjini. Kila kona ikawa ni Harmorapa, kuanzia kwenye majarida ya burudani, wachora katuni na TV za mitandaoni na hata za kawaida, habari ikageuka yeye.

 

SOMO LA HARMORAPA

Wapo wasanii wengi wamefananishwa na wasanii wenzao mfano marehemu Steven Kanumba amekuwa akifananishwa na msanii wa filamu, Rammy Gallis, huku mwigizaji Irene Uwoya akifananishwa na Wolper. Orodha ni ndefu.

Lakini hapa Harmorapa anatoa somo kwamba kiki siyo lazima ziwe za skendo huku ukihakikisha unatumia kila fursa inayopita mbele yako. Harmorapa pamoja na kutoka kupitia mgongo wa Harmonize, bado ameonyesha jeuri ya kujijenga kivyake kupitia staili yake mwenyewe.

Kubwa zaidi akiwa bado kinda kwenye gemu ameonyesha namna anavyoweza kutumia fursa ya kukutana na kaka zake waliomtangulia kwenye game na kufanya vizuri. Ameweza kufanya ngoma Kiboko ya Mabishoo na mkongwe Juma Nature.

Amekutana na kupiga stori na mkongwe kwenye Bongo Fleva, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ (Mbunge wa Mikumi),  hatujui kwenye stori zao walizungumza nini. Bila shaka walibadilishana namba za simu.

Sasa Harmorapa ni balozi wa kinywaji cha Swala. Ndiyo anatusua hivyo. Tutabaki kutafuta kiki za skendo, wakati Harmorapa akizidi kuchanja mbuga kwa staili ya peke yake.

Naanza kumuelewa huyu dogo. Tumpe muda zaidi. Tutakuja kusikia habari zake nzuri zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles