24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

KALONZO MUSYOKA: UHUSIANO WANGU NA RAILA ULINICHAFUA, ULINIPAISHA KISIASA (2)

kalonzo-na-railaMAKAMU wa Rais wa zamani wa Kenya, ambaye kwa sasa ni Kiongozi wa Chama cha Upinzani cha Wiper, Stephen Kalonzo Musyoka amezindua kitabu chake kipya Jumatano wiki mbili zilizopita.

Kitabu hicho kiitwacho ‘Against All Odds’, yaani Dhidi ya Vikwazo Vyote, kinaelezea safari yake inayoanzia eneo kame la Tseikuru huko Kitui, Ukambani alikozaliwa na kukulia wakati wa Vita za Mau Mau na Shifta hadi kufikia wadhifa wa pili kwa ukubwa nchini humo na namna alivyoshindwa kufikia ndoto zake za urais miaka ya 2002, 2007 na 2013.

Kwa leo kama ilivyotafsiriwa na mwandishi wetu, tunaendelea na sehemu ya pili ya maelezo ya Kalonzo namna anavyouona uhusiano wake na Raila ambao anadai ulichafua jina lake, lakini pia ukimsaidia kumpaisha kisiasa. Wiki iliyopita tuliishia kwa kuona kalonzo akipigiwa simu na Moi Januari 1998. Sasa endelea…

Hiyo ilikuwa baada ya kukamilisha baraza lake la mawaziri, Moi akaniambia: “Stephen ningekupatia kitu fulani kizuri zaidi, lakini ninyi Wakamba mliniangusha kwa kutonipigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1992.

Hata hivyo, nimekupatia wizara ya elimu lakini ikiwa na ‘kitu kingine juu yake.’

Dakika tatu baadaye, taarifa za uteuzi zilitangazwa. Moyoni nilidhani Moi alitaka kuniteua umakamu wa rais akakwamishwa na maadui wangu wa kisiasa, waliotumia kisingizio cha kabila langu la Kamba kutompigia kura.

Hivyo aliniteua kuwa waziri wa elimu na maendeleo ya nguvu kazi. Ukiachana na elimu, ‘nguvu kazi’ ni kile, ambacho Moi alisema ‘ikiwa na kitu kingine juu yake.’.

Ukiachana na hayo, binafsi nilikuwa mtu wa kwanza kuwa mtia saini wa chama cha LDP wakati Kibaki akiwa hivyo kwa chama cha NAK.

Tulifanya majadiliano mazito na Kibaki lakini alikataa kabisa kunifanya kuwa mgombea wake mwenza.

Alikuwa ameahidi umakamu wa rais kwa jamii ya Luhya na hivyo angeweza kubadili msimamo wake huo aliokwishaufanya.

Hata hivyo, mwishowe, tulikubaliana na Kibaki kwamba yeye angewania urais wakati Michael Wamalwa na mimi tungechukua nyadhifa mbili za umakamu wa rais. Kwamba kungekuwa na makamu wawili wa rais.

Raila kwa upande wake alipangiwa uwaziri mkuu, wadhifa, ambao ungeundwa kikatiba.

Hivyo, tukasaini kile kijulikanacho kama Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya vyama vya LDP na NAK.

Lakini kama kawaida siasa chafu, wivu, husda hujitokeza na namna washirika wa Kibaki walivyovuruga MoU hiyo si jambo la kusahau.

Hayo yalisababisha umakamu wa pili wa urais kutoundwa wala Raila kuupata ule uwaziri mkuu aliowahidiwa.

Matatizo kutokana na siasa za Kenya ni ukosefu wa thamani na misingi. Ninaamini kwamba kwa mtu kuwa mzalendo wa kweli, anatakiwa kuwa na imani fulani pamoja na dhamira. Wakenya wanaamini kwamba siasa ni mchezo mchafu na hakuna uwazi, ukweli wala uaminifu.

Kwamba wale ambao ni matapeli, wajanja wajanja na waongo wanaweza kustawi. Sidhani kama hali hii inapaswa kuwa hivi.  Wanasiasa maslahi ndio wana wanaofanya iwe hivi.

Ni hadi pale viongozi watakapojifunza kujitoa kafara, kuachana na ubinafsi, ulafi na tamaa ya pesa vinginevyo itakuwa ngumu kuipatia Kenya uongozi ule inaostahili katika kuipeleka katika ‘nchi ya maziwa na asali.’

Kabla ya MoU kutupiliwa mbali, tulikubaliana wizara ambazo kila mmoja wetu angechagua. Raila alichagua Barabara, Ujenzi wa Umma na Makazi, Saitoti alichagua Mipango nami nilichagua Mambo ya Nje.

Katika wadhifa huo, ndoto yangu muhimu ilikuwa kukamilisha majadiliano ya amani ya Somalia na Sudan.

Lakini miezi kadhaa tu baada ya NARC kuingia madarakani, Wamalwa, ambaye aliteliwa umakamu wa rais alifariki dunia.

Raila wakati huo alishindwa kunisaidia kumshinikiza Kibaki aheshimu MoU na kuteua makamu mwingine wa rais wakati ilikuwa ni haki yangu.

Alionekana kuridhika kwa wadhifa alioupata. Nililiona hilo likija kwa mbali. Kabla ya kifo cha Wamalwa, nakumbuka siku moja nilikuwa katika ndege ya kirais nikitokea Maputo, Msumbiji.

Katika msafara huo nilikuwa pamoja na Dk. Chris Murungaru, waziri wa usalama wa ndani na mmoja wa watu waliokuwa na nguvu ndani ya serikali ya Kibaki kipindi kile na  Dk. Dan Gikonyo, daktari binafsi wa rais.

Wakati wa mazungumzo tukiwa ndani ya ndege, Dk. Murungaru alitoa kile nilichokihesabu kama moja ya kauli mbaya sana kuwahi kuambiwa na wanasiasa.

Aliniambia: “Steve, rafiki yetu kule London (Wamalwa) hana siku nyingi za kuishi hapa duniani. Kwa sababu hiyo bora tumwachie Moody Awori amshikie wadhifa alionao hadi mwaka 2007 wakati utakapokuwa mgombea mwenza wa Kibaki. Sahau hili kwa sasa.”

Nilikasirika sana. nilimwambia: “Chris, tafadhari acha kucheza na Mungu.”

Nikapata safari kwenda kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York, Marekani baada ya kifo cha Wamalwa. Mawaziri katika baraza la mawaziri wakaanza minyukano kuuwania wadhifa wake huo.

Kwa mujibu wa MoU ni mimi niliyapaswa kuchaguliwa umakamu wa rais.

Nilitarajia kwamba wakati nikiwa sipo, Raila atakuwa mtetezi wangu kuhakikisha MoU inatekelezwa iwapo Kibaki angeonesha dalili za kukwepa makubaliano. Lakini Raila hakuweza kufanya hivyo.

Awori akapewa wadhifa huo kama Dk. Murungaru alivyoeleza, kitu kinachoonesha wazi kuwa genge lililomzunguka Kibaki lilikuwa limejipanga zamani kuhakikisha MoU hautekelezwi.

Mwaka 2005, tulikuwa bado tunasukuma ajenda ya katiba mpya. Genge dogo la wanasiasa kutoka Jimbo la kati liliungana kumzunguka Kibaki.

Murungaru, Waziri wa Sheria Kiraitu Murungi na wengine walianza kumbana Kibaki kwanini alisaini MoU ule bila kufikiria. Mimi na Raila taratibu tulianza kutengwa kutoka masuala ya Kibaki.

Wakati Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK), Samuel Kivuitu, akizindua alama za ‘Ndizi’ na ‘Chungwa’ zikimaanisha alama ya ‘Ndiyo na ‘Hapana’ kwa ajili ya kura ya maoni, nilisisimkwa kwamba tulipata tunda bora; chungwa.

Hivyo tulianzisha Vuguvugu la Demokrasia ya Chungwa (ODM) muda mfupi baada ya kuishinda kampeni ya Ndizi. Hata hivyo, tulipata shida kuisajiri ODM.

Ikabidi tuhamasishe maandamano ya mitaani na kuweka shinikizo kwa serikali kupitia vyombo vya habari ili kuwezesha usajiri wa ODM Kenya kuwa chama cha siasa.

Mimi na Raila sote tukiwa wanasiasa wenye ndoto kubwa tuliokuwa na matamanio na urais.

Hivyo, kwa kawaida katika hali kama hivyo hutokea uhasama na shuku katika vuguvugu. Hakuna mtu aliyeonekana akimpitisha mwingine.

Raila alifanya kazi kwa bidii katika wizara yake ya barabara. Siku moja, alikuwa Voi akikagua barabara wakati aliponipigia simu:

“Steve, nimeitwa na rais. Amesema kwamba amefanya marekebisho kadhaa katika Baraza la mawaziri ila hatamwondoa yeyote kutika shughuli zake.”

Raila alibakia katika wizara yake ijapokuwa ile ya Makazi alipokonywa. Nilipelekwa katika Wizara ya Mazingira na Maliasili. Huo ulikuwa msumari wa mwisho katika jenezan lililiozika MoU.

Itaendelea wiki ijayo

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles