28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

KALONZO MUSYOKA: UHUSIANO WANGU NA RAILA ULINICHAFUA, ULINIPAISHA KISIASA 

raila-odinga-kushoto-na-kalonzo-musyoka-2MAKAMU wa Rais wa zamani wa Kenya ambaye kwa sasa ni Kiongozi wa Chama cha Upinzani cha Wiper, Stephen Kalonzo Musyoka, amezindua kitabu chake kipya Jumatano ya wiki iliyopita.

Kalonzo, ambaye pia ni mmoja wa vinara wa muungano wa CORD unaoongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, unaohaha kuiondoa madarakani Serikali ya Jubilee katika uchaguzi wa mwaka ujao, alizindua kitabu hicho kwenye Hoteli ya Dusit 2 mjini Nairobi.

Kitabu hicho kiitwacho ‘Against All Odds’, yaani Dhidi ya Vikwazo Vyote, kimeandikwa na mwandishi wa zamani wa gazeti la Nation Caleb Atemi na kuchapishwa na kampuni ya Peace Book Co Ltd ya Hong Kong.

Kinaelezea safari yake inayoanzia eneo kame la Tseikuru huko Kitui, ambako alizaliwa na kukulia wakati wa Vita za Mau Mau na Shifta hadi kufikia kushika wadhifa wa pili kwa ukubwa nchini humo na namna alivyoshindwa kufikia ndoto zake za urais miaka ya 2002, 2007 na 2013.

Katika ukurasa huu kuanzia leo tutakuwa tukiwaletea baadhi ya mambo na matukio ya kuvutia hasa ya kisiasa kama mwenyewe anavyosimulia katika kitabu hicho.

Kwa leo kama ilivyotafsiriwa na mwandishi wetu, Kalonzo pamoja na mambo mengine ameeleza namna anavyouona uhusiano wake na Raila kuwa ulichafua jina lake, lakini pia ukimsaidia kumpaisha kisiasa.

Anasema: Uhusiano wangu na Raila Odinga umekuwa wa kufurahisha na pia njama, mwingi wa simulizi na utata.

Ni uhusiano ambao umeniacha na makovu na kupakaziwa matope ya kisiasa na wakati mwingine, lakini wakati mwingine wenye kuleta tabasamu na kung’ara katika mafuta ya kijasiri.

Vyombo vya habari na wachambuzi wa kisiasa kwa wakati fulani walitueleza kwamba sisi tu maadui hadi kaburini.

Wafuasi wake kwa mifano walinituhumu kumsaliti. Baadhi walienda mbali hata kunibatiza majina ya utani kama vile; tikitimaji, wakati wa kampeni kuhusu muswada wa katiba mpya mwaka ule wa 2010.

Wakati nilipojiunga na Serikali ya Mwai Kibaki mwaka 2008 baada ya Uchaguzi Mkuu wenye utata mwaka 2007, wafuasi wa Raila hasira na ghadhabu zao kali walizielekeza kwangu.

Wengi wao walikuwa na dhana potofu kuwa nilimnyima Raila urais mwaka ule 2007.

Hata hivyo, pamoja na tofauti zetu hizo, mimi na Raila tulikuwa kitu kimoja linapokuja suala la matamanio tuliyo nayo kwa Kenya; haki na demokrasia.

Historia na nyakati kuhusu maisha yetu huenda zikawa tofauti kimaandishi, lakini yetu dhamira ni ile ile. Urafiki wetu umezingirwa na tuhuma, propaganda na njama; zilizotokana zaidi na taarifa zisizo sahihi kutoka kwa nguvu fulani ambazo daima zilipenda kutuona tukiwa tumefarakana.

Kihistoria, hatuna mengi ya kufanana. Wakati mimi nikitokea eneo la vijijini la Ukambani, Raila anatokea katika familia maarufu ya kisiasa.

Baba yangu Mzee Peter Musyoka Mairu, alinilea katika malezi ya kawaida na ya kinyenyekevu akianzia kama muuza duka kule Tseikuru.

Ilhali Baba wa Raila, Jaramogi Oginga Odinga, alikuwa kivuli cha kisiasa kilichojongea mno juu ya Kenya mithili ya pandikizi kubwa la mtu atishaye.

Ushawishi wake hasa katika siasa za upinzani uko wazi na unaonekana katika kurasa nyingi za historia ya Kenya.

Tofauti zetu hizi hata hivyo, hazikutuzuia kufanya kazi pamoja kila mara safari zetu za kisiasa zilipokutana njiani.

Mwaka 2002, wakati mwandishi Denis Kodhe aliponikaribisha katika chama cha Liberal Democratic (LDP), niliwasilisha mwaliko kama huo kwa Raila ili aungane nami chamani humo.

Wengi katika siasa na dunia walidhani kuwa Raila alikuwa mwasisi wa LDP.

Ni muhimu nitumie fursa hii kusahihisha dhana hiyo isiyo ya kweli na hata kuongeza kwamba hakika kuingia kwetu LDP ulikifanya chama hicho kuwa imara na chenye nguvu mno.

Ijapokuwa mimi na Raila tulitumikia katika Serikali za Moi na Kibaki, hatukuwa na ukaribu sana hata pale tulipokuwa ndani ya baraza lile lile la mawaziri.

Mkutano wetu wa kwanza makini ulikuwa wakati ule tulipokuwa timu moja ndani ya Chama cha LDP na baadaye katika Vuguvugu la Chungwa (Orange Movement) baada ya Serikali kushindwa katika kura ya maoni kuhusu katiba mpya mwaka 2005.

Tuliungana dhidi ya muswada wa Katiba ya Wako na dhidi ya utawala mkuu wa kikabila na ukosefu wa haki katika nchi yetu.

Kufikia mwaka 2002, nilikuwa tayari kuwania urais. Kufikia wakati huo nilimkaribisha Raila kuungana nami LDP kipindi ambacho Moi alidhamiria kumfanya Uhuru kuwa mrithi wake bila kujali kwamba huyo alikuwa mwanasiasa mchanga mno kuwa rais au kuweza kushinda.

Nilitumia miaka 13 kukitumikia Chama cha KANU kama Katibu na nilijua lini itakuwa siku ya kukipa mkono wa kwaheri.

Nilibaini na kushuhudia ujanja ambao Kanu ilionekana imejipanga kuwachezea shere viongozi wake.

Nilikiangalia chama kikimeza watoto wake wenyewe. Sikuwa tayari kuharibiwa kiakili na kimwili. Hivyo niliamua kuondoka katika chama hicho, nilijua hakuna kurudi nyuma na nilijiandaa kuwania urais.

‘Mnyukano’ wangu wa kwanza na Raila ulitokea wakati wa kuunganisha Kanu-NDP kuelekea chaguzi za 2002.

Muungano huo ulishuhudia kuundwa kwa nafasi nne za makamu wa rais, ambazo ziliwaniwa na wanasiasa kutoka maeneo manne; Pwani, Kati, Magharibi na Mashariki.

Nilijua kwamba wakati vyama vikiungana, Raila alikuwa akijiweka katika nafasi nzuri ya uongozi wa nchi. Wakati akifanya hivyo, aliweka vikwazo kadhaa njiani katika safari yangu ya kisiasa.

Kwa mfano, wote Raila na Moi waliendesha kampeni kali kwa ajili ya John Harun Mwau na Joe Nyaga, wanasiasa wawili kutoka eneo langu la Mashariki, kunipinga katika chaguzi za chama cha Kanu ile Machi 2002 zilizofanyika kwenye Uwanja wa Michezo wa Moi, Kasarani.

Nyaga alijitoa katika mchuano huo, Uhuru hakuwa na mpinzani kwa sababu hakukuwa na Kanu katika Jimbo la Kati.

Musalia Mudavadi wa Magharibi alikuwa na mpinzani Cyrus Jirongo, lakini pia Katana Ngala pia hakuwa na mpinzani katika eneo la Pwani.

Kabla ya mkutano ule wa Kasarani, nilikutana na Raila katika Hoteli ya Norfolk, nikiwa na malengo ya kumwomba atumie ushawishi wake kwa rafikiye Mwau ajitoe katika mpambano ule kwa ajili yangu.

Lakini Raila hakuwa na jibu la moja kwa moja. Wakati siku ya uamuzi ilipokuja, jina langu lilipendekezwa na kupata uungwaji mkono. Jina la Mwau lilipendekezwa lakini halikupata uungwaji mkono.

Licha ya hayo ilikuwa wazi kuwa Moi na Raila walifanya juu chini kujaribu kukwamisha ndoto zangu za kuelekea uongozi wa juu.

Na kwa Moi hali kama hii inarudi nyuma zaidi ya mwaka 2002, kwani nakumbuka Moi alinipigia simu jioni moja ya Januari 1998.

Imetafsiriwa na mwandishi wetu Joseph Hiza kutoka gazeti la Daily Nation la Kenya

Itaendelea wiki ijayo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles