NA TIGANYA VINCENT
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kaliua kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu, imenunua bandali 300 kwa gharama ya Sh milioni 80 kutokana na mapato ya ndani.
Kauli hiyo, ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Haruna Kasele wakati wa kikao cha baraza la madiwani.
Alisema bati hizo zitagawanywa kata zote ambazo zimekamilisha mabona, ununuzi wa mbao na vifaa kwa ajili ya upauaji.
Alisema wanaendelea na ujenzi wa vyumba 6 vya maabara katika shule za sekondari za Kanoge, Kamsekwa, Zugimulole, Silambo, Seleli na Ilege.
Katika hatua nyingine, Kasele alisema Kaliua imepokea Sh bilioni 1 kwa ajili ya mpango wa elimu bila malipo kutoka Serikali kuu.
Alisema kwa upande wa shule za msingi, wamepokea Sh milioni 683.9 na shule ya sekondari wamepokea Sh milioni 399.8.
Aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo ambazo zimewawezesha wanafunzi kujiunga na shule za msingi na sekondari.
Wakati huo huo,halmashauri hiyo imetoa mikopo ya Sh milioni 345 kwa vikundi mbalimbali.
Alisema Sh milioni 133.5, zimetolewa kwa vijana, Sh milioni 184 zimetolewa kwa wanawake na milioni 27.5 zimetolewa kwa walemavu.
Alivitaka vikundi ambavyo vimekopeshwa kuhakikisha wanarejesha fedha hizo ili ziweze kukopeshwa kwa vikundi vingine.