23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Kaliua kujenga shule za Msingi kila kijiji

Na Allan Vicent, Kaliua

Halmashauri ya wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora imedhamiria kujenga shule za msingi katika vijiji vyote visivyo na shule ili kuwezesha watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule kupata fursa hiyo katika vijiji wanavyoishi.

Hayo yamebainishwa juzi na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Japhael Lufungija alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili aliyetaka kujua mikakati ya halmashauri hiyo katika kuboresha suala la elimu.

Alisema kuwa katika kipindi cha miaka 5 ya uongozi wake kama Mwenyekiti wa halmashauri hiyo atahakikisha kila kijiji kinakuwa na shule ya msingi na kila kata inakuwa na sekondari ili kuepusha watoto kutembea umbali mrefu kufuata shule katika kijiji au kata nyingine.

Alibainisha kuwa baadhi ya watoto hasa wa kike wamekuwa wakiacha shule au kupata mimba kutokana na changamoto hiyo hivyo akaahidi kuwa watahakikisha shule zinazojengwa katika vijiji vyote.

Lufungija aliongeza kuwa mkakati huo unaenda sambamba na uboreshaji miundombinu ya elimu katika shule zote ikiwa ni sehemu ya utekelezaji ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aidha, alibainisha kuwa katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha elimu nchini watahakikisha maboma yote ya madarasa yaliyoazishwa na wananchi katika kata zao yanakamilishwa ili kila kata iwe na shule ya sekondari.

“Kaliua tuko vizuri kielimu, tunataka kuendeleza rekodi hiyo kwa kuboresha miundombinu ya shule zote ikiwemo kujengwa shule mpya ili watoto wetu wasome hadi ngazi za juu na waweze kutimiza ndoto za maisha yao, alisema.

Lufungija aliitoa wito kwa wananchi na wadau wote wanaotaka kuanzisha miradi ya elimu katika wilaya hiyo kufuata taratibu ili halmashauri iweze kuwapa msaada unaohitajika katika kufanikisha mipango yao.   

Ofisa Elimu Msingi wa halmashauri hiyo, Martin Mahinda alisema kuwa dhamira ya halmashauri hiyo ni kuendelea kuwa miongoni mwa halmashauri 5 au 10 zinazofanya vizuri sana kielimu kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari.

Alibainisha kuwa asilimia 90 ya vijiji vyote 99 vya wilaya hiyo vina shule za msingi na kata 20 kati ya 28 zina shule za sekondari na juhudi kubwa zinaendelea kufanywa kwa kushirikiana na wananchi na wadau ili kuhakikisha vijiji vyote vinakuwa na shule za msingi na kata zote zinakuwa na sekondari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles