30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kairuki afanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini

MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Angellah Kairuki, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Sarah Cooke, jijini Dodoma.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Wizara hiyo, ilisema lengo la mazungumzo hayo ni kujadili maeneo yanayohusu uwekezaji. Taarifa hiyo ilisema Waziri Kairuki alieleza vipaumbele muhimu vya uwekezaji vitakavyochangia azma ya Serikali ya kuwa na uchumi wa viwanda, ikiwemo kuwekeza katika maeneo ya kilimo, elimu, afya, viwanda vya nguo pamoja na ujenzi wa miundombinu ya barabara.

“Ninafarijika kwa ujio wako na ni ishara nzuri ya mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi hizi mbili, naamini yatasaidia katika fursa za uwekezaji hasa kwa namna Uingereza ilivyochangia katika maeneo muhimu ikiwemo elimu,” alisema Kairuki.

Alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwa kuzingatia mchango unaotokana  na wawekezaji hasa katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini.

Kairuki alisema kuwepo kwa Idara ya Uwekezaji katika Ofisi ya Waziri Mkuu, ni hatua muhimu ambayo itasaidia kuongeza nguvu ya ufuatiliaji na utekelezaji wa masuala hayo na kuendelea kuleta mabadiliko katika kutatua changamoto zilizoikabili sekta hiyo.

Naye Balozi Cooke, aliipongeza Tanzania kwa kuwa na sera zinazovutia wawekezaji pamoja na maboresho yanayofanywa kuwavutia wawekezaji nchini, ikiwemo maeneo ya ulipaji wa kodi.

“Tunaelewa kuwa Serikali inafanya jitihada kubwa katika kuboresha mazingira ya biashara, ikiwa ni pamoja na mazingira ya ulipaji wa kodi. Tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuwa na mchango katika maendeleo ya nchi pamoja na kuimarisha mahusiano yaliyopo,” alisema Cooke.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles