Mwandishi Wetu
Kampuni inayosimamia uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kimataifa (KIA), hakuna kifaa chochote cha ukaguzi kilichoharibika wanjani hapo kwa miaka mitatu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo (Kadco), Christopher Mukoma, amesema si tu kwa miaka hiyo mitatu bali hata kwa siku moja hakuna kifaa chochote cha ukaguzi kilichoharibika.
Kauli hiyo ya Mukoma, imekuja muda mchache baada ya gazeti moja la kila siku kuripoti leo Alhamisi Septemba 19, kuwa kifaa hicho kimeharibika na hakifanyi kazi kwa muda wa miaka mitatu.
Amesema KIA inauthibitishia umma wa Watanzania na Jumuiya ya Wasafiri wa Anga kuwa hakuna kifaa chochote cha ukaguzi kilichoharibika si tu kwa miaka mitatu bali hata kwa siku moja na kusababisha abiria kulalamika kama ilivyoandikwa kwenye gazeti hilo.
“Aidha ukisoma muktadha wa habari hiyo inaonyesha kuwa inafanya rejea ya kikao kazi kilichowahusisha wakuu wa mikoa ya kilimanjaro na Arusha, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii na wadau wa utalii na watumiaji wa Uwanja wa Ndege wa KIA.
“Kwa taarifa hii, ninapenda kuuarifu umma kuwa habari hiyo si ya kweli na ama mwandishi wa habari hiyo amepotosha ama kwa kujua au kwa kutokujua na kuripoti jambo ambalo halikuzungumzwa kwenye kikao.
“Vifaa vyote vya ukaguzi vinavyotumiwa na uwanja wetu viko imara na salama na tunauomba umma upuuze habari hii ambayo haiko sahihi,” amesema.