Tanzania ilipofikia mapambano dhidi ya surua

0
794

AVELINE KITOMARY, DAR ES SALAAM

CHANJO ni jambo muhimu kwa watoto kwa sababu wanapoikosa wanaweza kushambuliwa na magonjwa haraka hatimaye kupoteza maisha.

Zipo chanjo ambazo zinatolewa pindi tu mtoto anapozaliwa, ambapo ya kwanza huwa ni ile ya kifua kikuu.

 Akifikisha wiki sita anapata chanjo ya nimonia, kifadulo, tetenasi, dondakoo, polio na kuhara, hizo zote mtoto hupatiwa ndani ya siku 14 baada ya kuzaliwa.

Chanjo ya surua ni mojawapo ambayo mtoto anaipata, baada ya kufikisha miezi tisa anaanza dozi ya kwanza na dozi ya pili ni baada ya miezi 18.

Hata hivyo, licha ya umuhimu wa watoto  kupewa chanjo hiyo, kuna maeneo mengine duniani bado watoto wanakumbwa na visa vya surua.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), takribani watoto milioni 169 duniani walikosa chanjo ya kwanza ya dozi ya surua mwaka 2010 na 2017, idadi hiyo ni sawa na wastani wa watoto milioni 21.1 kila mwaka.

Shirika hilo linasema ongezeko la watoto ambao hawapati chanjo huchangia mlipuko wa surua katika nchi mbalimbali.

UNICEF inasema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2019 zaidi ya visa 110,00 vya surua vimeripotiwa katika maeneo mbalimbali duniani.

Hata hivyo, licha ya matukio ya surua kuendelea kuongezeka, hapa nchini wamefanikiwa kupambana na ugonjwa huo.

Kwa sasa, chanjo ya surua imekuwa ikihusishwa na aina mpya ya surua rubela, lengo ni kutokomeza kabisa ugonjwa huo kufikia mwaka 2020.

Meneja wa Mpango wa Chanjo Taifa, Dk. Dafrossa Lyimo, anaiambia MTANZANIA kuwa utoaji wa chanjo nchini umefanya kiwango cha magonjwa kwa watoto kupungua.

Anasema kwa sasa Tanzania ni nchi ya tatu Afrika kwa utoaji wa chanjo zote na kupunguza magonjwa kwa watoto, nchi ya kwanza ni Rwanda ikifuatiwa na Zambia.

Kwa mujibu wa Dk. Lyimo. mwaka 2014 walianza kampeni  kwa ajili ya kutoa chanjo ya surua rubella na polio, ambapo kwa sasa wanafanya mwendelezo wa utoaji chanjo hiyo na wanatarajia kuanza zoezi hilo Septemba 26 hadi 30 mwaka huu.

Kampeni hizo za utoaji chanjo ni mpango wa kidunia wa kutokomeza kabisa magonjwa ya surua rebela na polio.

“Katika kampeni, tutatoa chanjo kwa watoto wote wenye umri chini ya miaka miatano haijalishi kama kapata ile iliyoko kwenye ratiba au la, kwani hii inasaidia wale ambao kinga zao zilishindwa kupokea chanjo ya awali,” anasema Dk. Lyimo.

Ugonjwa wa surua unaathiri mno watoto  na unaenezwa na virusi  kwa njia ya hewa.

JINSI INAVYOATHIRI WATOTO

Kwa mujibu wa Dk. Lyimo, madhara ya surua rubella, mtoto anaweza kuyapata akiwa tumboni kwa mama yake iwapo mama ameathirika.

Hali hiyo husababisha mtoto kuzaliwa na ulemavu wa viungo mbalimbali.

“Tunapoona watoto wanazaliwa na matatizo kama matundu kwenye moyo, matatizo ya figo, tatizo la mgongo wazi na ulemavu mwingine utakuta mama zao ndio wameathirika na ugonjwa wa rubella.

“Tunapotoa chanjo tunamkinga mtoto na virusi vya rubella ambavyo vinafanana na surua kwahiyo mtoto huyo akikua na kuwa mama anakuwa na uwezo wa kumkinga  hata mtoto wake tumboni asipate matatizo,” anabainisha.

Anasema surua rubella pia inaweza kuathiri viungo vya mwili, macho kuwa mekundu, ubongo unaathirika, homa kali na kuharisha.

“Mara nyingi watoto wanapoteza maisha licha ya ugonjwa huu kuwa na chanjo, ila tunahimiza ni lazima apate kinga inayostahili,” anasema Dk. Lyimo.

MAFANIKIO YA CHANJO

Dk. Lyimo anasema kwasasa watoto wamekuwa wakipelekwa kwa wingi kupata chanjo hivyo ugonjwa huo umepungua kwa kiasi kikubwa.

“Zamani wakati mimi nasoma Muhimbili kulikuwa na wodi ya surua, lakini sasa hivi wodi zimefungwa na hakuna wagonjwa tena.

“Idadi ya wagonjwa imepungua hadi kufikia asilimia 95 kutokana na utaratibu wa chanjo kutolewa baada ya mtoto kuzaliwa, pia kampeni hizi zimesaidia kwa kiasi kikubwa,” anaeleza.

Dk. Lyimo anasema asilimia 99 ya watoto tayari wameshachanjwa dozi ya kwanza huku asilimia 84 wamepata dozi ya pili.

“Kisayansi ukichanja watoto 100 kwa dozi ya kwanza, watakaopata kinga ni asilimia 80 hadi 85, wanaobaki mwili haukupigana ili kupata ile kinga ndio maana zamani unakuta mtoto kachanjwa lakini bado anapata surua.

“Hilo ni lile kundi la asilimia 15 hadi 20 ambao miili yao haikuweza kutengeneza kinga kwa mfano, wakipata dozi mbili kati ya 100 ni asilimia 95 ndio watapata kinga wengine asilimia 5 watabaki,” anaeleza.

Anasema kuwa kwa wastani asilimia 25 ya watoto wanakuwa hawana chanjo ya surua kwenye miili yao.

“Ukijumlisha hiyo asilimia 15 hadi 20 ya watoto ambao miili yao haijapokea chanjo na hao ambao hawajapata kabisa – asilimia tano, jumla inakuwa asilimia 25, wengine lishe duni inachangia.

Anasema lengo mojawapo la kampeni hizo ni ili wale ambao wamechanjwa na miili haijapata kinga wapate.

Dk. Lyimo anaeleza kampeni hizo zitagharimu kiasi cha Sh bilioni 11  ambapo jumla ya watoto milioni 12 watapatiwa chanjo ya surua rubella na polio.

 CHANGAMOTO ZILIZOPO

Changamoto kubwa inayotajwa ni wazazi au walezi kutokuzingatia chanjo ya  dozi ya pili baada ya kupata ile ya kwanza.

“Kwa kawaida, mtoto anatakiwa apate chanjo mbili  lakini wakati mwingine watoto wanakuwa hawapati dozi hii ya pili, hii inatokana na mzazi baada ya kupata dozi moja anafikiri inatosha kumbe sio hivyo,” anasema Dk. Lyimo.

Pia anasema changamoto zingine ni uhamasishaji mdogo kwa ngazi za chini na uelewa mdogo kuhusu aina za chanjo kwa wakati.

“Changamoto za umbali pia zipo, lakini tunatoa huduma za mkoba sasa matangazo inabidi yaende haraka ili kule huduma inapokelekwa wajue huduma zitatolewa muda fulani,” anaeleza.

MALENGO NA USHAURI

“Malengo ya kutokomeza surua kidunia walikuwa wanasema ifikapo 2020 kusiwe na mgonjwa, kwa Tanzania tuko vizuri lakini kuna majirani zetu ambao hawako vizuri.

“Sisi pia malengo yetu ni hayo, ndio maana serikali inaendelea kuwekeza kwenye utoaji wa chanjo bure kwa sehemu zote za mjini na vijijini,” anasema Dk. Lyimo.

Anatoa ushauri kwa jamii kuhakikisha inashiriki katika kukamilisha ratiba ya chanjo.

“Chanjo zinazotolewa kwa watoto zinauwezo wa kumkinga na magonjwa 13 hizo ni zile zinazotolewa kwa ratiba. Wazazi au walezi wanatakiwa kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo zote.

“Pia wale wazazi wanaopuuzia chanjo waache hasa hii ya surua rubella kwani kunabaadhi yao mtoto akipata chanjo moja wanaacha kumpeleka ya pili.

Pia anawashauri wazazi pindi watakapoona dalili ambazo sio za kawaida kwa mtoto wamuwahishe kituo cha afya haraka badala ya kuamini katika ushirikina.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here