27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

KADA MWINGINE WA CCM AUAWA RUFIJI

Na PATRICIA KIMELEMETA

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rufiji, mkoani Pwani, anayefahamika kwa jina la Amir Chanjale, amepigwa risasi na watu wasiofahamika.

Kifo cha kada huyo ni mwendelezo wa mauaji ya watu mbalimbali, wakiwamo askari wa Jeshi la Polisi na viongozi wa serikali za mitaa na vijiji mkoani Pwani.

Tukio la Chanjale linafanya jumla ya idadi ya watu waliouawa katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja kutimia 20.

Kuuawa kwa kada huyo kumekuja ikiwa zimepita siku 21 tu tangu watu wasiofahamika na ambao vyombo vya dola havijatangaza kuwatia hatiani kuwauwa kwa risasi askari wanane wa Jeshi la Polisi waliokuwa wakitoka doria katika Kijiji cha Jaribu, wilayani Kibiti.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Njwayo, alisema tukio hilo lilitokea saa mbili usiku katika Kata ya Umwe, wilayani humo, ambapo mtu huyo alivamiwa na watu hao na kisha kumpiga risasi na kukimbia.

Alisema, serikali ya wilaya hiyo inashirikiana na Jeshi la Polisi ili kufanya msako na kuhakikisha kuwa wahusika wote wanakamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.

Alisema, kwa sasa wameanzisha timu maalumu ya kushughulika na masuala hayo, na kwamba, mtu au kikundi chochote cha watu watakaobainika wanajishughulisha na mauaji hawataachwa, bali watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine.

“Bado tunafanya msako ili kuhakikisha kuwa wauaji waliofanya vitendo hivyo wanakamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria… hatutawaacha,” alisema Njwayo.

Naye Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Dk. Mohamed Mchengelwa, alisema hali hiyo inawatia hofu wananchi wa maeneo hayo kutokana na kuendelea kwa vitendo vya mauaji.

“Tunaiomba Serikali iangalie kwa jicho la huruma kwenye jimbo letu kwa sababu vitendo vya mauaji bado vinaendelea, hali inayosababisha wananchi kuishi kwa wasiwasi na hofu kubwa,” alisema Mchengelwa.

Aliongeza, tatizo hilo limevuka mipaka kwa sababu kila baada ya mwezi mmoja kupita utasikia mauaji mengine, jambo ambalo linapaswa kuangaliwa kwa umakini na kuimarisha ulinzi zaidi.

Alisema bila kufanya hivyo, mauaji ya wananchi yataendelea siku hadi siku, jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya wananchi wasio na hatia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Rianga, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema tayari Jeshi la Polisi limewasili maeneo hayo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa tukio hilo ili watuhumiwa waweze kukamatwa.

Alisema, jeshi hilo linaendesha operesheni maalumu kwa ajili ya kuwasaka watu watakaobainika kufanya mauaji hayo, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kuwakamata wauaji.

“Tumepeleka askari katika maeneo hayo kwa ajili ya kufanya uchunguzi juu ya mauaji hayo ili wahusika waweze kusakwa na kuchukuliwa hatua,” alisema Rianga.

Aliongeza kuwa, Jeshi la Polisi litaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo na kuhakikisha kuwa hakuna mauaji mengine yatakayoweza kutokea kwenye maeneo hayo.

Matukio ya mauaji katika Mkoa wa Pwani yanaelezwa kuonyesha kila dalili kutekelezwa na watu wenye ujuzi na malengo mapana.

Tukio la sasa na lile ambalo lilichukua uhai wa askari wanane ni mwendelezo wa matukio mengine saba ya aina hiyo yaliyotokea katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja Mkoa wa Pwani.

Ingawa hadi sasa, si Jeshi la Polisi wala mamlaka nyingine ambazo zimekwishaeleza kwa uwazi kiini cha kuwako kwa mfululizo wa matukio ya aina hiyo katika maeneo yale yale, lakini utekelezaji wake na aina ya watu wanaotekeleza unaelezwa kuwa na mwelekeo wa kigaidi.

Zaidi ya wiki mbili zilizopita, gazeti dada la MTAZANIA Jumapili liliripoti juu ya taarifa ilizozikusanya kutoka vyanzo vya ndani ya Jeshi la Polisi, na katika maeneo ambayo matukio ya  mauaji yanayotokea mara kwa mara na kuonyesha kuwa ukatili huo wa kutisha unaendeshwa na mtandao mpana wa kihalifu ambao umejikita zaidi katika Wilaya ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji.

Mtandao huo unadaiwa kusheheni wataalamu wenye ujuzi wa kutumia silaha nzito waliopatiwa mafunzo katika Taifa la Sudan na Mashariki ya Kati.

Inaelezwa, mtandao unaotekeleza mauaji hayo, mbali na kuwa na intelijensia kali, pia una mizizi iliyokomaa ndani ya jamii, hatua inayosababisha kushindwa kuufichua kwa hofu ya kuuawa.

Kuwapo kwa mazingira hayo kunawafanya wakazi wa maeneo hayo kuwa wasiri wakubwa wa wahalifu.

Hilo linaweza kuthibitishwa kwa kiasi fulani na mazingira ambayo mwandishi wa habari wa MTANZANIA Jumapili alishuhudia katika vijiji vya Mwalusembe, Kimanzichana na Bungu.

Tofauti kabisa na dhana iliyozoeleka ya ukarimu wa Watanzania, watu wa maeneo hayo hukwepa wageni na hawataki kuzungumza nao kwa hofu ya kuuawa.

MLOLONGO WA MAUAJI

 

Kumekuwapo na mlolongo wa matukio ya mauaji katika Wilaya ya Kibiti na Mkuranga na kinachozua maswali ni kitendo cha wauaji kutochukua mali yoyote.

APRILI 14, askari nane waliuawa, ikiwa ni siku chache baada ya askari wa Jeshi la Polisi kuwaua kwa risasi wanaume watatu waliokuwa wamevalia baibui za kike.

Wanaume hao, ambao walikuwa na pikipiki mbili, walikuwa wakijaribu kukwepa vihunzi vya polisi vilivyokuwa vimewekwa katika Daraja la Mkapa.

Siku chache baada ya  tukio la kuuawa kwa askari, kada mwingine wa CCM naye aliuawa.

Februari mwaka huu, watu watatu, akiwamo Ofisa Upelelezi wa Wilaya (OC CID) ya Kibiti mkoani Pwani, Mrakibu wa Polisi, Peter Kubezya, waliuawa kwa risasi.

Wengine waliouawa ni Ofisa wa Misitu ambaye alikuwa Mkaguzi wa Kituo cha Ukusanyaji mapato ya ushuru katika Kijiji cha Jaribu, Peter Kitundu na Rashid Mgamba ambaye ni mlinzi/mgambo ambao walipigwa risasi kichwani na begani na walikufa papo hapo eneo la tukio.

Mei, 2016 Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambunda, Said Mbwana aliuawa kwa risasi.

Oktoba, 2016, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho hicho, Aly Milandu aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wanne.

Novemba 2016, wenyeviti wawili wa vitongoji wa kijiji hicho, waliuawa kwa kupigwa risasi.

Januari, 2017, watu ambao Jeshi la Polisi hadi sasa halijawafahamu walimuua mfanyabiashara Oswald Mrope, kwa kumpiga risasi mbele ya familia yake.

Februari 3, 2017, watu wasiojulikana walivamia nyumba ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Jaribu, Bakari Msanga na kuichoma moto, huku yeye mwenyewe akifanikiwa kuwatoroka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles