32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

KABILA ATANGAZA KUTOWANIA URAIS

KINSHASA, DRC


RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila, hatawania tena urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Desemba 23.

Uamuzi huo umetangazwa jana jioni baada ya kumalizika mkutano wa siku mbili wa muungano wa vyama vinavyomuunga mkono Kabila, Common Front for Congo (FCC).

Kwa mujibu wa msemaji wake, Lambert Mende, FCC ilimteua waziri wa zamani wa mambo ya nje, Emmanuel Ramazani Shadary kuwa mgombea wake wa urais.

Shadary, mshirika wa karibu wa Kabila, alikuwa miongoni mwa watu waliowekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya kwa tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu mwaka 2017.

Pamoja na kwamba Shadary anahesabika kama mmoja wa wafuasi watiifu wa Kabila, kama mwanasiasa si maarufu miongoni mwa Wakongo milioni 80.

“Ni ndege wa nadra,” alisema Mende baada ya tangazo hilo, akikataa kujibu maswali ya wanahabari kuhusu mgombea huyo.

Wagombea kadhaa wa vyama vya upinzani wamejisajili kwa uchaguzi huo akiwamo makamu wa rais wa zamani, Jean-Pierre Bemba, huku mfanyabiashara Moise Katumbi akizuiwa kuingia nchini hapa baada ya kutumia miaka miwili uhamishoni Ubelgiji.

Kupatikana kwa mrithi wa Kabila, kunahitimisha minong’ono ya miaka mingi ya iwapo atakiuka ukomo wa urais, ambao ulimalizika mwaka 2016.

Serikali ilisubiri hadi dakika za mwisho kutangaza uamuzi wa Kabila kutogombea, ukizingatia Tume ya Uchaguzi iliweka siku ya mwisho kwa wagombea urais kuwsilisha majina yao kuwa jana adhuhuri

Awali majina kadhaa ya kumrithi Kabila yalikuwa yakisambaa katika mitandao, wakiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Augustin Matata Ponyo, Mkuu wa Shughuli za Ikulu ya Rais, Nehemie Mwilanya Wilondja na Spika wa Bunge, Aubin Minaku.

Uchaguzi huo ambao umeahirishwa mara mbili, unatazamwa kuwa muhimu kwa mustakabali wa DRC ambayo mara nyingi si imara kisiasa.

Waliohudhuria mkutano wa juzi, ambao ni matokeo ya mkutano wa jana uliotangaza mrithi wa Kabila, awali walisema rais huyo aliwahutubia waliokuwapo, bila ya kujadili mustakabali wake kisiasa.

Kabila ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2001, alipaswa kuondoka madarakani mwaka 2016 wakati mihula yake miwili kikatiba ilimalizika na alikataa kueleza iwapo atagombea urais tena, hali iliyozua wasiwasi, machafuko na maandamano yakiwamo yaliyoitishwa na viongozi wa dini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles