26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kabendera asomewa mashtaka uhujumu uchumi, utakatishaji

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MWANDISHI wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera (39), aliyekuwa akishikiliwa na polisi tangu Julai 29, mwaka huu, amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashtaka matatu, likiwemo la kutakatisha zaidi ya Sh milioni 173.

Kabendera alipanda kizimbani jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile na kusomewa mashtaka ya uhujumu uchumi na mawakili wa Serikali watatu; Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, Faraja Nchimbi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon.

Akisoma shtaka la kwanza, Kadushi, alidai kati ya Januari mwaka 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Kabendera na wengine ambao hawapo mahakamani, alitoa msaada kwenye genge la uhalifu kwa nia ya kujipatia fedha.

Nchimbi alisoma shtaka la pili ambalo mshtakiwa anadaiwa kukwepa kodi.

Alisema inadaiwa kati ya Januari, 2015 na Julai 2019 maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, bila sababu za msingi, Kabendera alikwepa kulipa kodi Sh 173,247,047.02 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Wankyo akisoma shtaka la tatu la kutakatisha fedha, alidai kuwa katika tarehe hizo, mshtakiwa alitakatisha kiasi hicho cha fedha huku akijua zimetokana na zao la kusaidia genge la uhalifu na kukwepa kodi.

Hakimu Rwizile alimfahamisha mshtakiwa kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, hivyo hakutakiwa kujibu lolote.

Kesi iliahirishwa hadi Agosti 19, mwaka huu kwa kutajwa.

Baada ya kumaliza kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 75/2019, mahakama iliendelea kusikiliza maombi yaliyowasilishwa na mawakili wa utetezi.

Wakili Jebra Kambole alidai maombi yaliyopo mahakamani, waliomba mshtakiwa apewa dhamana ama afikishwe mahakamani.

Alidai mshtakiwa amefikishwa mahakamani, lakini kwa mashtaka ambayo hayana dhamana, hivyo kwa upande wao hawana cha kuzungumza, waliomba kuondoa maombi yao.

Wakili Kadushi alidai kwa upande wao hawana pingamizi kwa maombi hayo kuondolewa.

Mahakama ilikubali kuyaondoa.

Kesi ya jinai itatajwa Agosti 19, mwaka huu na mshtakiwa yuko gerezani Segerea.

Kabendera anatetewa na Wakili Kambole, Reginald Martine, John Mallya, Benedict Ishabakaki na Swedy Shilinde.

Taarifa za kukamatwa kwa Kabendera zilianza kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii jioni ya Julai 29, mwaka huu na kuthibitishwa na ndugu zake waliodai kuwa mwanahabari huyo alichukuliwa nyumbani kwake Mbweni, Dar es Salaam na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi.

Siku moja baadaye, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, katika mkutano na waandishi wa habari, alisema polisi wanamshikilia Kabendera kwa mahojiano kuhusu uraia wake na kwamba alikamatwa baada ya kushindwa kutii wito wa kumtaka kufika polisi kwa mahojiano.

Hata hivyo siku, moja baadaye Idara ya Uhamiaji ilisema imekuwa ikimfuatilia mwandishi huyo tangu mwaka 2013, baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi ambao wamekuwa wakilalamika kuwa si raia wa Tanzania.

Akitoa ufafanuzi huo, Kamishna wa Uraia na Pasipoti wa idara hiyo, Gerald Kihinga, alisema uchunguzi huo ulianza muda mrefu, lakini yeye alikaidi alipoitwa kutoa maelezo ya upande wake.

“Ni kwamba uchunguzi ulianza kufanyika muda mrefu na tulikuwa tukimwita kuhojiwa akawa hataki kuja, yaani kama angetupa ushirikiano akaja tukamuhoji tukamaliza, tukapata tunavyohitaji, tungemalizana naye tukaendelea na taratibu nyingine,” alisema.

Kihinga alisema watu wanaohojiwa na idara hiyo kuhusu masuala ya uraia ni wengi na wanapotoa ushirikiano ndipo wanawarahisishia kazi yao, kwa sababu uchunguzi unaweza kuanza na kupata taarifa za awali.

Alisema kwa Kabendera, tayari hatua ya taarifa za awali ilishamalizika na ilifikia hatua sasa walikuwa wanataka kumuhoji ili kulinganisha taarifa walizonazo.

“Tatizo yeye alikuwa hataki kuja, kwa hiyo tukaona tumkamate tumuhoji kwa nguvu na kupata vile tulivyokuwa tunavitaka kwa nguvu, angekubali mapema sisi tungekuwa hatuna shida,” alisema.

Kutokana na kuibuka kwa utata wa kukamatwa kwa mwanahabari huyo kuhusu uraia wake, Mei 2013, yalifanyika mahojiano ya mwisho kuhusu suala hilo.

Hatua hiyo ilijumuisha matukio ya kuhojiwa kwa wazazi wake kijijini kwao, jambo ambalo lilizua taharuki na manung’uniko.

Kutokana na hali hiyo kwa wakati huo, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliunda kamati iliyofanya kazi ya kuchunguza uraia wa Kabendera.

Kwa mujibu wa kumbukumbu hizo, Dk. Nchimbi, aliwaagiza maofisa wa uhamiaji kutowasumbua wazazi wa Kabendera kuhusu uraia wao, agizo ambalo alilitoa baada ya mwanahabari huyo kuandika barua ya malalamiko kwa waziri mwenye dhamana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles