27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

JWTZ yatoa kauli nzito vijana wanaojiunga jeshi

*Viongozi waliopenyeza ndugu, madaktari kitanzini

*Nida, Takukuru, Necta kufanya uhakiki upya

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema litapitia upya vijana walioandikishwa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika mikoa yote nchini baada ya kubainika kuwapo upungufu katika uandikishaji.

Vijana hao ni wale wenye viwango mbalimbali vya elimu ambao hujiunga JKT kujitolea kwa mkataba wa miaka miwili.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa JWTZ, Luteni Kanali Gervas Ilonda, alisema watafanya zoezi kabambe la uhakiki wa vyeti na nyaraka husika kwa vijana walioandikishwa.

CHANGAMOTO ZILIZOBAINIKA

Alizitaja changamoto zilizobainika kuwa ni vijana wengi kwenda kujiandikisha katika mikoa mingine na kusababisha wenyeji wa mikoa husika kukosa nafasi, kutoa taarifa za uongo, baadhi ya viongozi kuingilia mchakato kwa kuwaombea nafasi ndugu na jamaa zao, utapeli katika uandikishaji na taratibu zilizowekwa kutozingatiwa.

“Kimsingi mantiki ya kugawa nafasi katika mikoa na wilaya ni kuhakikisha vijana wanapatikana kutoka nchi nzima kwa uwiano ulio sawa.

“Tunasema kijana aandikishwe anakoishi kwa sababu anashirikishwa hadi kiongozi wa kijiji au mtaa ndiyo anajua mwenendo wake ukoje, kama ni Mtanzania, ana tabia njema kwa sababu ndiyo viongozi wa taifa la kesho.

“Tunapochukua kwa mapenzi ya wazazi au viongozi tunaharibu taifa na hatutapata viongozi wa kesho,” alisema Luteni Kanali Ilonda.

Alisema pia vijana wengi wamefanya vitendo viovu vya kushawishi na kujaribu kutoa rushwa na hatimaye kughushi vyeti vya kuzaliwa na vile vya elimu.

“Kuna watu wanawasaidia kughushi vyeti na kuwapa mawazo ya jinsi gani ya kufanya ili waweze kujiunga, jeshi hili lina weledi, nidhamu, hatuwezi kubeza vitendo vinavyofanyika, lazima hatua zichukuliwe,” alisema.

VIONGOZI WALIOKUWA NA ORODHA YA MAJINA

Kuhusu viongozi, alisema baadhi yao wamekuwa wakienda na orodha ya majina ya vijana ambao ni ndugu na jamaa zao kuwaombea nafasi makao makuu ya jeshi na JKT kinyume na utaratibu, wakati nafasi hushindaniwa maeneo wanakotoka kulingana na sifa zilizoainishwa.

“Huko waliko (viongozi) wanajijua walioleta majina, kiongozi anakuja na vijana 10 hadi 20, hao vijana nani anawajua uzalendo wao, tabia zao, wametumwa na nani… anaweza kutengeneza zaidi ya vijana 100 akaenda kuwatumia kwa mapenzi yake,” alisema.

UTAPELI

Kwa mujibu wa Luteni Kanali Ilonda, changamoto nyingine ni utapeli, kwamba watu wasio waaminifu huwarubuni vijana na wazazi na kuwataka watoe fedha ili waweze kuwaingiza vijana hao JKT.

Aliwataka wazazi na vijana wafuate utaratibu unaotangazwa na mamlaka husika ili kuingia JKT, vinginevyo watapoteza fedha na kuchukuliwa hatua kwa kutoa rushwa.

“Ninawataka wale wanaofanya vitendo hivyo kuacha mara moja kwa sababu vinalichafua taifa letu na vinaweza kusababisha matatizo makubwa, nafasi za JKT hazitozwi fedha,” alisema Luteni Kanali Ilonda.

KUTOZINGATIWA KWA TARATIBU

Kuhusu kutozingatiwa kwa taratibu, alisema baadhi ya wazazi na vijana hupuuza taratibu zilizoweka na kusisitiza vijana wao wachukuliwe nje ya utaratibu au wachukuliwe hata kama wana mapungufu katika sifa zilizotangazwa kama vile elimu, umri, afya, nyaraka na nyingine.

“Vijana wanasema ni yatima, analipenda jeshi kabla hajazaliwa ili kushawishi watu waweze kukiuka taratibu.

“JKT ni chungu cha kulea vijana, kuweka uzalendo, kijana aweze kuwa na maadili mema. Tukianza kumwingiza kwa kutumia rushwa, kughushi vyeti, tunatengeneza taifa ambalo litaanguka.

“Vigezo vyote vinavyowekwa kwa ajili ya kupata vijana wa JKT ni muhimu na lazima vikamilike, ikiwa una mapungufu usipoteze muda wako na wa watu wengine kuomba, maana hutafanikiwa. Tujifunze kuelewa na kuheshimu taratibu zilizowekwa,” alisema.

WATAKAOBAINIKA KUTOA TAARIFA ZA UONGO

Luteni Kanali Ilonda alifafanua kuwa katika zoezi hilo la uhakiki watashirikiana na JKT, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), Baraza la Mitihani (Necta) na wadau wengine wakiwamo Takukuru ili kuwabaini wote waliofanya udanganyifu.

“Watakaobainika kutoa taarifa za uongo watachukuliwa hatua za kisheria, wengine wanaghushi hadi afya na tutakuwa na jopo la madaktari bingwa kuwapima upya kwa sababu kazi ya jeshi inahitaji utimamu wa mwili, akili na mawazo.

“Kusudio letu ni kutaka kuwachunguza ni Watanzania kweli, anatoka katika eneo husika, ana afya bora na tukijiridhisha hata kama idadi itapungua bora tukapeleka vijana wachache kuliko kupeleka vijana ambao hatujui wametoka wapi.

“Hakuna atakayesalimika na hatutaangalia sura au wadhifa wa mtu, kama ni kiongozi umetumia dhamana yako vibaya sasa itakaa pembeni kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Alisema kujiunga JKT si tiketi ya kupata ajira kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, serikalini au sehemu nyingine, bali lengo ni kuwajengea vijana uzalendo na kuwapatia stadi mbalimbali ili warudipo katika jamii waweze kujitegemea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles