30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Asimulia mumewe alivyotekwa mbele yake

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

VERONICA Kundya, mke wa mfanyabiashara, Raphael Ongangi aliyedaiwa kutekwa hivi karibuni, amesimulia namna mumewe alivyotekwa na watu wasiojulikana.

Juzi, ilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Ongangi ambaye ni raia wa Kenya alitekwa na watu wasiojulikana katika eneo la Msasani jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana jijini Dar es Saalam, Veronika alisema Juni 24 majira ya saa tatu usiku akiwa na mumewe kwenye gari wakielekea nyumbani, walipofika maeneo ya Shule ya Msingi Oysterbay ghafla kuna gari liliwazuia kwa mbele.

Alisema baada ya gari hilo kuwazuia watu wanne walitoka huku mmoja akielekea upande wa abiria alilokaa yeye huku akimgongea na kuonyesha bastola.

“Wakati huyo mmoja akinigongea na kunionyesha bastola, wale wengine nao walikuwa upande wa dereva ambako mume wangu alikuwepo akiendeshagari.

Wakatuambia tuweke mikono juu na mimi wakanipeleka viti vya nyuma na mume wangu akawekwa viti vya mbele yangu na mwingine akawa anaendesha gari.

“Mwingine ambaye nilikuwa nimekaa naye viti vya nyuma, akaniinamisha chini huku akizungusha bastola kichwani kwangu huku wale wengine wawili wakiwa na mume wangu.

“Ghafla wakatoka nje ya gari na mimi nikaweza kuchungulia na nikaona bango la CCBRT na ATM ya CRDB na mbele nikaona IST nyeusi na wakaingia tena ndani ya gari letu na akaongezeka mmoja,”alisema.

Akiendelea kusimulia, Veronika alisema mume wake akashushwa na kuhamishiwa kwenye gari lingine huku yeye akibaki kwenye gari lake na watu watatu.

“Tulipofika Msasani wakaniacha karibu na soko la samaki na wakachukua simu yangu akaitoa kwenye pochi na kuiweka mbele na wakaniacha na yule aliyekuwa na bastola baadaye akaondoka nikabaki na yule dereva huku akiniambia niendelee kuinama.

“Baadaye kushtuka nikajikuta niko peke yangu kwenye gari nikachukua simu yangu haraka haraka nikamtumia mama yangu message kuwa atuombee hatuko mahali salama.

“Baada ya muda kidogo mume wangu naye alinipigia simu akaniambia baby uondoke uende nyumbani huku nikiwa nalia sana nikaendesha gari hadi nyumbani nikakuta watoto wangu wako salama,”alisema.

Veronica alisema baada ya kuwakuta watoto wake wako salama ilikuwa majira ya saa 4:45 usiku ndipo akaenda kuripoti Kituo cha Polisi Oysterbay.

“Na polisi walichonieleza ni kwamba wanashughulikia pia niliripoti ubalozi wa Kenya nao wamesema wanashughulikia,”alisema Veronika.

Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Kinondoni, Mussa Saibu alisema wanazo taarifa za kutekwa mfanyabiashara huyo na kwamba tayari wameshaanza kufanya uchunguzi.

“Ni kweli mke wake ndio alikuja kuripoti na kwa kuwa jukumu la jeshi ni kufanya uchunguzi tayari tumeshaanza uchunguzi lakini sasa hatuna uthibitisho kama kweli alitekwa ama lah.

“Baada ya sisi kufanya uchunguzi ndio tutajua kama alitekwa kweli ama lah. Tunatoa wito kwa wananchi na mkewe kwamba watoe ushirikiano kwa jeshi kama alikuwa labda na figisu figisu na watu wengine ili sisi tuchukue hatua zaidi,”alisema Kamanda Saibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles