Na NORA DAMIAN
-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, wametaja sababu zinazochangia uharibifu wa rasilimali za asili katika Bara la Afrika na kusema changamoto za Afrika zitatatuliwa na Waafrika wenyewe.
Wakati Rais Magufuli akitaja sababu sita, Rais Mkapa amesisitiza kutatuliwa kwa migogoro ya wakulima na wafugaji huku akitahadharisha kuwa kama uharibifu wa mazingira utaendelea, kuna uwekezekano ifikapo mwaka 2075 ikawa hakuna misitu tena nchini.
Viongozi hao walieleza hayo Ikulu jijini Dar es Salaam jana, wakati wa mkutano wa sita wa Jukwaa la Uongozi Afrika, ulinaojadili masuala ya usimamizi wa rasilimali za asili kwa ajili ya mabadiliko ya kiuchumi barani Afrika lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi.
Jukwaa hilo pia lilihudhuriwa na marais wastaafu akiwemo Jakaya Kikwete, Olusegun Obasanjo (Nigeria), Thabo Mbeki (Afrika Kusini) na Hery Rajaonarimampianina (Madagascar).
JPM
“Afrika ina utajiri wa maliasili, ardhi yenye madini, gesi, mafuta, maeneo ya uvuvi na kadhalika. Asilimia 30 ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani inapatikana Afrika lakini haijasimamiwa vizuri.
“Changamoto za Waafrika zinatatuliwa na Waafrika wenyewe, hakuna wajomba watakaokuja kutusaidia. Tunafahamu changamoto zetu vizuri kuliko mtu mwingine yeyote,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alitaja sababu sita zinazochangia uharibifu wa rasilimali katika Bara la Afrika kuwa ni migogoro na hali tete ya kisiasa, masalia ya fikra za kikoloni, kushindwa kusimamia rasilimali kuleta mageuzi ya kiuchumi na ukosefu wa ubunifu na teknolojia ya viwanda.
Nyingine ni mikataba ya makubaliano inayonufaisha upande mmoja na uharibifu wa maliasili unaosababishwa na uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya tabia ya nchi.
“Migogoro na hali tete ya kisiasa Afrika inasababishwa na mabeberu wanaotaka kuendelea kutumia rasilimali zetu, wakati sisi tunagombana wao wanachukua rasilimali zetu.
“Hatukutafsiri vizuri dhana ya uhuru na kutokana na kutoelewa, tukadhani watawala wetu wa zamani ndiyo wenye uwezo wa kutusaidia kusimamia na huo ndio mwanzo wa utegemezi.
“Tunadhani fedha ndiyo msingi wa maendeleo, tunazunguka kuomba wahisani fedha na pengine hizo zinazotolewa zinatokana na rasilimali zetu,” alisema Rais Magufuli.
Alisema ukosefu wa uzalendo na hujuma zinazofanywa na mabeberu zimesababisha nchi nyingi kuathiriwa, akitolea mfano hapa nchini ambapo mikataba mibovu iligharimu sekta ya madini.
Rais Magufuli alisema kumekuwa na uchafuzi wa mazingira unaofanywa na mataifa makubwa na kusababisha kuwepo kwa ukame, mafuriko na kutotabirika kwa mifumo ya hali ya hewa.
Alieleza hatua zilizochukuliwa na Serikali kudhibiti uharibifu wa mazingira kuwa ni pamoja na kutungwa kwa Sheria ya mwaka 2017 ya kulinda utajiri na maliasili zilizopo, kupitia upya na kurekebisha mikataba ya uchimbaji wa madini, msukumo wa ujenzi wa viwanda na kuanzisha miradi kupunguza matumizi ya nishati ya kuni kama vile mradi wa uzalishaji umme katika bwawa la Nyerere.
Hatua nyingine ni kuanzishwa kwa hifadhi mpya (Burigi – Chato, Ibanda – Kyerwa na Rumanyika Karagwe), kudhibiti nidhamu ya watumishi wa umma, ufisadi na ubadhirifu na tayari wameanza kuona matokeo ya hatua hizo.
MKAPA
Kwa upande wake Mkapa alisema asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima na wafugaji lakini wengi wamekuwa wakikabiliwa na migogoro kila kukicha kutokana na kila mmoja kudhani ana haki juu ya ardhi kuliko mwingine.
“Ardhi ni tatizo mojawapo linalowakumba wakulima na wafugaji, unakuta wafugaji wanasema eneo lote ni lao na hilo linasababisha mtafaruku baina yao na wakulima, kama nchi ni vyema kuangalia suala hili kwa namna ambayo haiathiri maendeleo,” alisema Mkapa.
Alisema uharibifu wa mazingira unaoendelea nchini umesababisha sehemu kubwa ya misitu kupotea kila mwaka na kutahadharisha kuwa kama hali itaendelea hivyo, kuna uwezekano ifikapo mwaka 2075 kutakuwa hakuna misitu nchini.
“Njia sahihi ya kuondoa unahiribifu wa misitu ni kuwa na mikakati ya upandaji miti kwa sababu ardhi ya nchi haijaharibiwa sana kama nchi nyingine, miti inazuia mabadiliko ya tabia nchi, mmomonyoko wa ardhi, inatunza vyanzo vya maji na inaweza kutunza hewa ya ukaa kwa kiwango cha theluthi mbili ambacho ni kikubwa sana,” alisema.
Alisema pia utafiti uliofanywa Julai unaonyesha hekta bilioni 1.7 zimeathiriwa lakini tayari nchi mbalimbali zimeanza kampeni ya upandaji miti ikiwemo Ethiopia ambayo hadi sasa imeshapanda miti bilioni 2.6 huku ikilenga kupanda miti bilioni 4 na Kenya ambayo imeshapanda miti zaidi ya milioni 15.
Aliwataka viongozi watambue kuwa tatizo ni kubwa hivyo wasimamie sheria na kuhakikisha wanafanya maamuzi ya muda mrefu na si kulaumu watu.
Alisema kadiri watu wanaovyoongezeka kunakuwa na ongezeko la shughuli za kibinadamu ambazo kwa kiasi kikubwa zinaathiri hali ya hewa na kusababisha joto katika uso wa nchi na kuathiri unyeshaji wa mvua.
“Hatuweki kipaumbele kwenye masuala ya msingi, watu wanaongezeka kwa kasi na kutumia ardhi nadhani mambo haya yangepewa kipaumbele kama uchaguzi,” alisema Mkapa.
MARAIS WENGINE
Marais wengine wastaafu walisema ingawa Afrika ni tajiri lakini matatizo yanafanana karibu nchi zote na kulitaka bara hilo liamke na kujenga uwezo wa kujitegemea lenyewe ili kutunza maliasili kwa ajili ya urithi wa dunia.
Pia walishauri kuwe na sera zinazozingatia matumizi bora ya ardhi, miongozo na taratibu sahihi za utunzaji mazingira na wananchi waone umuhimu wa misitu na kuelekezwa kutumia nishati mbadala sambamba na kuwa na juhudi za pamoja baina ya sekta ya umma na binafsi.
Obasanjo alisema “mimi naamini jambo la kwanza kabisa ni elimu, nilijaribu kuongea na kinamama vijijini wapande miti lakini kwa bahati mbaya wengi wanateketeza tu mapori. Anakuambia ‘mme wangu akitoka porini akiwa na kuni na mkaa nitatumia nini?’ Ni kama hatuna jibu.
“Kwa watu wa vijijini tunatakiwa twende mbali zaidi kuwafanya wawe na mtazamo chanya sambamba na kupanda miti ya kutosha.”
Naye Rais Mbeki alisema changamoto ni mataifa makubwa yanayoendelea kukata mbao na magogo katika nchi zenye misitu inayoleta mvua kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Gabon.
“Uongozi bado ni tatizo kubwa na kama hatulizungumzi hili tutaendelea kulalamika rasilimali zetu zinapotea hivyo, tunapaswa kuendelea kuwa na ushirikiano wa pamoja,” Mbeki.
Rais Mstaafu wa Madagascar, Rajaonarimampianina alisema wameanza kuwafundisha watoto kuanzia elimu ya msingi juu ya umuhimu wa utunzaji mazingira waweze kutambua kuwa rasilimali ni mtaji muhimu katika kukuza uchumi.
“Elimu ni tatizo kubwa na bila elimu hatuwezi kwenda mbele, tuangalie miaka 20 hadi 30 ijayo tupate suluhisho la kudumu kwa ajili ya mazingira yetu,” alisema Rajaonarimampianina.
Mwenyekiti Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEOrt), Ali Mufuruki, alisema hekta 72,000 za misitu hukatwa kila mwaka hapa nchini na kutahadharisha miaka mitano ijayo vita itakayotokea ni ya maji na inaweza ikatokea hata hapa nchini.
“Tumekusanyika katika chumba hiki (ukumbi wa mikutano Ikulu) watu ambao tuna elimu, hatuwezi kusema sisi ni wajinga au hatuna elimu ya kutosha. “Suala hili linaongelewa sehemu tofauti na hata juma hili tumesikia suala la moto katika Msitu wa Amazon, wote tunaelewa tatizo, asili na madhara yake lakini hatutafuti ufumbuzi, tunazungumza kidiplomasia tunaishia hapo hapo,” alisema Mufuruki