Serikali yatakiwa kutenga bajeti maalumu shule za awali

0
1196

Hadija Omary, Lindi

Serikali imeombwa kutenga bajeti maalumu  kwa ajili ya kununua zana na vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi wa madarasa ya awali vitakavyowawezesha kuboresha utoaji wa elimu nchini.

Ombi hilo limetolewa na Mwalimu wa Darasa la awali wa Shule ya Msingi Stadium, Manispaa ya Lindi, mkoani hapa, Fatuma Kassim leo Ijumaa Agosti 30, wakati akizungumza na Mtanzania Digital shuleni hapo.

Amesema zana hizo zinasaidia kupanua uelewa wa watoto katika masuala ya elimu, malezi na makuzi.

“Changamoto tunayokabiliana nayo hivi sasa katika shule nyingi kwa madarasa ya awali ni serikali kutoweka bajeti kwa madarasa hayo katika fedha za ruzuku jambo ambalo kwa kiasi kikubwa huathiri baadhi ya shughuli za ufundishaji katika madarasa hayo ikiwa pamoja na  kununua vifaa vya elimu changamshi vinavyomuwezesha mtoto kupata elimu ya malezi na makuzi,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Lindi, Jomari Satura amekiri kutokuwapo kwa ruzuku maalumu ya madarasa ya awali kutoka Serikali Kuu katika halmashauri yao huku akisema kuwa changamoto hiyo ni kwa nchi nzima.

“Licha ya changamoto hizo, halmashauri yetu imejipanga kuimarisha menejimenti na utawala bora katika shule zote 35 za msingi na awali ifikapo mwaka 2021 kwa kuimarisha usimamizi na utawala katika Shule hizo,” amesema.

Hata hivyo, amesema katika kulisimamia hilo tayari halmashauri imetenga kiasi cha Sh milioni 19 kwa ajili ya ufuatiliaji wa taaluma na ununuzi wa shajara kutoka katika vyazo vyao vya mapato ya ndani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here