24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

JUKATA WAMTEGA PROFESA KABUDI

Na ARODIA PETER-DAR ES SALAAM



JUKWAA la Katiba Tanzania (JUKATA) limesema lina matumaini makubwa kwamba Waziri mpya wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi atawezesha kukamilishwa kwa mchakato wa Katiba mpya ambao umekwama. 


Jukwaa hilo limesema kupitia kwa Profesa Kabudi, Watanzania watapata Katiba mpya ambayo waliitolea maoni kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba na waziri huyo alikuwa mjumbe wake.


Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Jukwaa hilo  Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa JUKATA, Hebron Mwakagenda alisema uzoefu wa Profesa Kabudi unahitajika   wakati huu ambao mwelekeo wa kupatikana kwa Katiba mpya haupo bayana.
“Kutokana na ushiriki wake katika mchakato mzima wa kukusanya maoni ya Watanzania akiwa Kamishna wa Tume, ni matumaini ya JUKATA na Watanzania kwa ujumla kwamba msomi huyo atawezesha kukamilisha mchakato wa Katiba mpya itakayokuwa imekidhi vigezo, mahitaji na matumaini ya walio wengi.


Mkurugenzi huyo wa JUKATA alisema kwa kutambua mchakato wa Katiba mpya ulisimama wenyewe zipo changamoto kuu mbili ambazo zinatakiwa kutafutiwa ufumbuzi kwanza.


Alizitaja changamoto hizo kuwa ni kurekebisha Sheria ya mMbadiliko ya Katiba Na. 8 ya 2011 na marekebisho yake pamoja na Sheria ya Kura ya Maoni ya 2013.


Alisisitiza kuwa ni vema marekebisho hayo yalenge kuhuisha vifungu vilivyopitwa na wakati.
 Jukwaa la Katiba limeishauri Serikali kutoa taarifa rasmi kwenye Gazeti la Serikali kuufanya mchakato huo kuwa hai.


Mwakagenda alisema kabla ya kufanya marekebisho yoyote ya sheria kwa sasa ni vema wananchi wapate fursa ya kujadili kwa kina masuala ya msingi ambayo lazima yaingizwe kwenye marekebisho hayo.


“Tunashauri katika Bunge hili la bajeti 2017/2018 waziri apeleke miswada ya marekebisho ya sheria zinazosimamia mchakato wa Katiba mpya.


“Kwa kuwa Tume ya Mabadilio ya Katiba haipo, tunashauri kiundwe chombo maalum kusimamia hatua zilizobaki,” alisema.  
Wiki iliyopita, akitoa ufafanuzi kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Profesa Kabudi alisema Serikali itaanza kazi ya kurekebisha sheria  kukamilisha upatikanaji wa Katiba mpya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles