25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

JPM: USIONE SIMBA KALALA UKAMCHEZEA

  • Ahoji kwanini hakukuwa na nyaraka wakati wa mauaji Kibiti

NORA DAMIAN Na ASHA BANI – DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli, ameonya hatawavumilia watu wanaotaka kuvuruga amani ya nchi, huku akisisitiza Serikali ipo, haijalala na haitalala.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa mfumo wa rada za kuongozea ndege, alisema alikabidhiwa Serikali na wananchi na atailinda kwa nguvu zote.

“Serikali ipo, nimekabidhiwa na wananchi kuilinda kwa nguvu zote na ninasema kwelikweli, wengine nawaangalia tu, usimuone simba amelala ukawa unamgusagusa mkia wake,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kwa sasa jukumu lake kubwa ni kujenga uchumi wa Tanzania, lakini anatambua katika harakati hizo wako watakaojitokeza na kutaka kumpinga.

“Nchi yetu kwa miaka mingi imekuwa ni wafadhili (akimaanisha kusaidia nchi nyingine kupata uhuru), mimi jukumu langu sasa ni kujenga uchumi wa Tanzania, tumechelewa kwa kusaidia nchi nyingine, sasa tunataka tujisaidie wenyewe,” alisema.

Rais Magufuli alisema pia hatawasikiliza wanaopiga kelele na badala yake ataendelea kuchapa kazi.

“Kufa kwa Kibiti (akimaanisha mauaji ya Kibiti) hakuna hata waraka uliotoka, ingawaje sipendi sana kulizungumzia hili.

“Kazi ya uongozi ni ngumu sana na usiposimama na kumtanguliza Mungu, unaweza ukakata tamaa. Unageuka huku unaona watu wananung’unika na hata Mussa (mmoja wa manabii katika kitabu cha Biblia) alipata shida, ndiyo maana ya maendeleo, maendeleo yana changamoto.

“Watajitokeza wa kupiga kelele, kunung’unika na wala sitawasikiliza, mimi ninachapa kazi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema anatambua katika harakati za ujenzi wa nchi, wako watakaompinga, lakini akawataka Watanzania kuendelea kusimama imara wakimtanguliza Mungu.

“Mtapigwa vita na kila mtu, hata wa nje. Lakini sisi tusimame imara na tumtangulize Mungu.

“Hata Mungu aliumba malaika pakatokea mashetani yana wivu, yakatupwa duniani. Wapo watu duniani hata ungemfanyaje, ungembeba umpitishe kwenye mto, ukimvusha atasema mgongo wako ulikuwa unanuka jasho. Endeleeni kuwaombea, lakini sisi tusiyumbe, tuko pazuri mno,” alisema.

Rais Magufuli alisema pia ana uhakika kwa takwimu alizonazo, uchumi wa Tanzania umekua kwa zaidi ya asilimia saba.

“Uchumi wa Tanzania ni miongoni mwa nchi tano Afrika ambazo uchumi wake unapaa.

“Kubanabana fedha zilizokuwa zinavuja kwa watu wabaya, ndiyo zinasaidia kuhudumia wananchi masikini na kuitangaza nchi.

“Fedha zangu ziko kwa mafisadi, nitawabana tu watazitema kwa sababu ndio wamekuwa wakichezea fedha zetu, wasipozitema kwa upole, watazitema kwa nguvu hata kama ni kwa kutapika.

“Hata makanisani zaka zimepungua kwa sababu zingine zilikuwa zinatolewa na mafisadi, lakini sisi Watanzania tusimame twende mbele kwa ajili ya taifa hili,” alisema.

RADA

Rais Magufuli alisema kukosekana kwa rada za kutosha za kuongozea ndege, kumesababisha baadhi ya mashirika ya ndege yasite kufanya biashara nchini.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, hivi sasa Tanzania ina rada moja tu yenye uwezo wa kuhudumia asilimia 25 ya anga lake.

Alisema hatua hiyo imesababisha Serikali kupoteza Sh bilioni 1.2 kila mwaka, tozo ambazo zimekuwa zikilipwa kwa Serikali ya Kenya kutokana na Shirika la Usafiri wa Anga la Kimataifa (ICAO) kukasimu sehemu ya anga la Tanzania kwa nchi hiyo.

“Huwezi ukawa na ndege zinaongozwa na nchi jirani, zinaongozwa hadi zinafika Tabora au Tanga, ‘is a shame’, kiporo kilichokaa tangu tupate uhuru, hatuwezi tukawa na taifa la namna hiyo,” alisema.

Rais Magufuli alisema mradi huo utakapokamilika, kutakuwa na uwezo wa kuliona anga lote na anga za Burundi na Rwanda ambazo Tanzania imekasimiwa na ICAO.

“Utaimarisha usalama wa nchi yetu, utarahisisha shughuli za uongozaji ndege na kuiongezea mapato nchi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema usafiri wa anga ni muhimu katika masuala ya biashara, hasa kusafirisha bidhaa kama matunda, mbogamboga, samaki na vingine na hasa katika ukuaji wa sekta ya utalii.

Rais Magufuli alisema zaidi ya asilimia 70 ya watalii duniani wanatumia usafiri wa anga na hivyo, uimarishwaji na uboreshwaji wake ni jambo lisilokwepeka.

Aliwapongeza viongozi na wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), kwa kuvuka lengo la usalama la ICAO kwa kipindi kifupi.

“Mwaka 2013 mlikuwa vilaza kwelikweli, lakini kwa muda mfupi hivi sasa mna asilimia 64, hongereni sana. Niko tayari kwa tuzo ya kutambua matokeo makubwa yaliyofanywa na nchi yetu kutoka kwa Rais wa ICAO,” alisema.

Pia aliitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na TCAA kumsimamia vizuri mkandarasi ili mradi huo ukamilike, ikiwezekana kabla ya muda uliopangwa.

“TCAA mhakikishe mnaandaa wataalamu wa kutosha kwa ajili ya kuendesha na kutunza mradi wa rada, naziagiza mamlaka husika kuimarisha ulinzi na usalama katika viwanja vyetu. Tukio la aibu lililotokea Mwanza lisirudiwe tena,” alisema.

MBARAWA ATAKIWA AACHE UPOLE

Rais Magufuli alimtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kukunjua makucha yake kuhakikisha miradi anayoisimamia inakamilika kwa wakati.

Hatua hiyo ilifuatia baada ya Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari, kumweleza Rais Magufuli ujenzi wa jengo la kuongozea ndege katika uwanja wa Mwanza unasuasua.

“Suala la jengo lisiwe na sababu, tunataka tulimalize. Nakuagiza waziri (Mbarawa) yule mkandarasi wa Mwanza asimamiwe, ahakikishe jengo linakamilika mapema, rada zote ziwekwe kwa pamoja.

“Usiwe mpole, nataka hili ukaonyeshe ukali wako, kama fedha ni tatizo sema hata leo apelekewe. Katibu mkuu yuko hapa, peleka fedha asitafute kisingizio cha fedha,” alisema Rais Magufuli.

NDEGE MPYA

Rais Magufuli alisema ndege nyingine tatu zitawasili baadaye mwaka huu, ikiwamo yenye uwezo wa kubeba abiria 262 na nyingine zitabeba kati ya watu 150 hadi 220.

“Tumenunua ndege sita kwa mpigo bila kukopa, tulitakiwa kwa umoja wetu bila kujali dini, vyama tushangilie mafanikio haya.

“Nchi zilizostaarabika duniani katika masuala ya kitaifa, huwa wanaungana, ndege zikija si za Magufuli, ni kwa ajili ya Watanzania wote,” alisema Rais Magufuli.

WAZIRI MBARAWA

Waziri Mbarawa alisema Agosti 22 mwaka jana, Serikali kupitia TCAA iliingia mkataba na kampuni ya nchini Ufaransa kwa ujenzi wa mradi wa rada.

Alisema mradi huo utagharimu Sh bilioni 67.3 na kwamba TCAA itatoa asilimia 45 ya fedha huku Serikali Kuu ikiongezea asilimia 55 iliyobaki.

Alizitaka taasisi nyingine zinazokusanya kodi mbalimbali kuiga mfano wa TCAA katika kutekeleza miradi mikubwa badala ya kutegemea ufadhili au fedha kutoka Serikali Kuu.

Alisema mkandarasi wa mradi huo atahakikisha vipuri vinapatikana kwa muda wa miaka 15.

Waziri huyo aliipongeza TCAA kwa kusimamia na kudhibiti usalama katika sekta ya usafiri wa anga na kuvuka malengo ya usalama ya ICAO baada ya kupata asilimia 64.35 mwaka jana.

TCAA

Mkurugenzi Mkuu TCAA, Johari, alisema mradi huo una changamoto ya ukamilishwaji wa jengo la kuongozea ndege katika uwanja wa Mwanza kwani bado halijakamilika hadi sasa.

“Kwa sababu jengo la kuongozea ndege uwanja wa Mwanza halijakamilika, tutakwenda Kilimanjaro, Songwe halafu Mwanza itakuwa ya mwisho,” alisema Johari.

Alisema baada ya kukamilika kwa mradi huo, usalama wa anga la Tanzania utaimarika kwa asilimia 100, ndege zinazotua bila kufuata utaratibu hazitakuwapo tena na mapato yataongezeka kutokana na tozo za uongozaji ndege.

Mamlaka hiyo inatoa huduma za uongozaji ndege kwenye vituo 14 ambavyo ni Dar es Salaam, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Mwanza, Tabora, Kigoma, Dodoma, Iringa, Songwe, Songea, Mtwara, Zanzibar na Pemba.

WAKUU WA MIKOA

Katika hatua nyingine, wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza wamekosoa waraka uliotolewa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), huku wakimuhakikishia rais kuwapo kwa usalama katika maeneo yao.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliwataka wanaotangaza kuhusu waraka watangazie katika mikoa yao na si Dar es Salaam.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, alimweleza rais matamko yote yalianzia Kilimanjaro na kwamba yataishia hapo hapo.

“Matamko yameanzia Kilimanjaro na naamini yataishia hapo, tunapima kila hoja na tutakuletea taarifa sahihi jinsi tunavyoyashughulikia,” alisema Mghwira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, alisema wao wapo salama na hakuna tamko lolote lililotoka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles