Mwandishi Wetu, Mwanza
Rais Dk. John Magufuli, anatarajiwa kuzindua rasmi hifadhi mpya ya Taifa ya Burigi iliyoko Chato mkoani Geita, wiki ijayo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla amesema hayo jijini Mwanza leo, katika mkutano wa mwaka wa Wahariri na Waandishi waandamizi ulioandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa).
Amesema ili sekta ya hifadhi iweze kuleta mabadiliko ni lazima jamii wakiwamo wanahabari washiriki katika kutangaza vivutio vya utalii kama njia ya kuongeza idadi ya wageni wa ndani na nje.
“Bila wanahabari sekta ya utalii haiwezi kujulikana hivyo tushirikiane pamoja katika hili.
“Na pia kama mnakumbuka hivi karibuni tumetangaza hifadhi mpya za taifa na Jumanne Rais Magufuli, atazindua hifadhi ya Burigi Chato, lengo ni kuhakikisha wageni waweze kuona maliasili zetu popote pale Tanzania,” amesema Dk. Kigwangalla.
Awali, Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa, Dk. Allan Kijazi, amesema kufanyika kwa mkutano huo wa kila mwaka umeleta mafanikio makubwa ikiwamo kuongezeka kwa idadi ya watalii katika hifadhi za taifa.
“Wanahabari ni wadau muhimu sana, kwani hata mabadiliko ya mfumo wetu wa uundwaji wa Jeshi Usu ni hatua ya muhimu ambayo itakwenda kuchochea kuongeza chachu ya utalii na kupambana na majangili ambao wamekuwa wakiharibu rasilimali zetu,” amesema.