23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Uchache wa Mahakimu kikwazo kesi za ujangili

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

KUTOKUWAPO kwa idadi kubwa ya Mahakimu wa kushughulikia kesi za ujangili kunatajwa kuwa moja ya vikwazo katika  mapambano dhidi ya ujangili nchini.

Hayo yamewekwa wazi na Hakimu Mkazi, Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, Mary Mrio katika mahojiano maalum na Waandishi wa Habari za Mazingira nchini.

Mrio alisema kuwa kuna changamoto nyingi zinazowapa ugumu katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kesi kuchukua muda mrefu kutokana na kukosekana kwa ushahidi na upelelezi kutokamilika kwa wakati.

 “Upungufu wa rasilimali watu ni changamoto, mathalani kwenye kituo cha Bariadi, Hakimu niko peke yangu na ninatakiwa kuhudumia Wilaya tatu za Bariadi, Itilima na Busega.”

Alisema kesi nyingi zilizopo kwenye wilaya hizo zinatoka Pori la akiba la Maswa na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Wakati huo huo una mambo mengine ya kiutawala, kuhudumia Mahakama za watoto, kwahiyo rasilimali watu ni changamoto”, alisema.

Aliongeza kuwa changamoto nyingine ni Mahakama kutoa fedha kidogo za kuwawezesha mashahidi wanotoka maeneo ya mbali kufika Mahakamani.

“Mfano mashahidi wanaotakiwa kutoa ushahidi mkoani Simiyu wakati wao wanaishi  Songea au Dar es Salaam.”

Aidha alitaja suala la washtakiwa kutoroka kabla ya hukumu pamoja na kukosa vifaa vya kuhifadhia vidhibiti na uelewa mdogo wa makosa ya ujangili.

Mrio alisema wapo watu wengine wanashuhudia uhalifu wakiwa katika eneo la tukio, lakini kutokana na kutokufahamu namna yakuyaelezea makosa hayo katika lugha ya sheria huwa kunawasababishia matatizo wakati wa kutoa ushahidi haswa Mahakamani.

“Kubwa kabisa ni kukosa mafunzo kwa waendesha mashtaka wengi, ambapo wakati wa hukumu inakuwa ni tatizo kuendesha kesi. “Tunapata bahati wale ambao tunadili na sehemu za uhifadhi kwa maana tunafanya jitihada binafsi kupata mafunzo hayo,”.  

Licha ya changamoto hizo, Hakimu Mrio alisema kuwa katika kesi zilizoripotiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, asilimia 90 ya kesi zote zilipata hukumu na kubwa kuliko zote ilitolewa hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela.

Akiongelea mabadiliko yaliyopo alisema kesi za ujangili zimepungua kwani zilizofunguliwa mwaka 2015 hadi Mei 2019 ni 479, mwaka 2015 zilipatikana kesi 175, mwaka  2016 kesi zilikuwa  111, mwaka 2017 kesi zilizoripotiwa ni 106, mwaka 2018 kesi zilikuwa 66 na hadi Mei 2019 kesi zilizopatikana ni 21.

Katika kuweka mambo sawa ili kuendeleza nia njema ya kuzitunza hifadhi pamoja na wanyamapori, alisisitiza kuwepo na mafunzo maalumu ya Uhifadhi wa Wanyamapori kwa mawakili na wadau wengine ili kuwepo na uelewa mpana ambao utasaidia kutokomeza ujangili nchini.

“Ipo haja ya kuongezwe pesa kwa ajili ya kuwasaidia mashahidi wanaotoka mbali pamoja na kuongezwa nguvu kazi haswa katika vituo vya kazi kuhakikisha kesi zinashughulikiwa kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa,” alisisitiza Hakimu Mrio

Kwa upande wake Mwanasheria (Principal State Attorney, National Prosecution), Rosemery Leonard alisema kuwa  kesi za wahalifu ni ngumu kama hakuna vielelezo na ushahidi wa kutosha utakao wasaidia kuendesha kesi mahakamani na kutolewa hukumu stahiki ili kuepuka changamoto ya kukamata wahalifu, kuwafungulia mashtaka kisha wakaachiwa huru.

“Kesi za ujangili zinahitaji umakini mkubwa pamoja na vielelezo vya kutosha ili kukamilisha ushahidi wakati wa kuendesha kesi Mahakamani,” alisema Leonard

Akizungumzia changamoto za kisheria na namna yakuendesha kesi za ujangili, Ofisa kutoka Shirika la Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Wanyamapori (TRAFFIC), Linah Clifford amesema kuwa changamoto kubwa ni uelewa wa masuala mazima ya uhifadhi wa wanyama pori hivyo wao wanachokifanya ni kutoa elimu kwa wadau mbalimbali haswa waendesha mashtaka. 

“Tuna miradi mingi, karibu mia inayosaidia kupambana na uhalifu wa wanyamapori. Tunafanya mafunzo kwa mahakimu, waendesha mashtaka juu ya jinsi yakuendesha kesi za uwindaji haramu wa wanyama pori, pia tunafanya tafiti mbalimbali za matumizi mbalimbali ya wanyamapori kujua ni kwanini wanafanya uwindaji kama ni kwaajili ya dawa, chakula n.k,” alisema Clofford

Aliongeza kuwa, “ Tunafanya kazi na Sekta binafsi kwenye masuala ya usafirishaji, tunawafundisha namna yakukagua mizigo inayosafirishwa kwa kutumia mbwa maalumu na namna nyingine nyingi. Tunafanya tafiti za uvuvi kuangalia nini kinafanyika, katika mikoa inayozungukwa na ziwa, bahari. Tunafanya mafunzo kwa watu wa Bandari na kuona namna watakavyodhibiti biashara haramu pamoja na kuwafundisha sheria zinasema nini,”.

Clifford alisisitiza kuwa, “Sheria zinabadilika kila siku na majangili wanabadili mbinu kila uchao kwahiyo na sisi tunaendelea kutoa mafunzo kuwasaidia waendesha mashtaka na wadau wengine kuwa na uelewa wa nini kinaendelea katika sekta ya uhifadhi wanyamapori na haswa katika kukabiliana na ujangili nchini.” 

Naye Mkuu wa Chuo cha Taalauma ya Wanyamapori, Pasinasi, Mwanza, Damalu Lowaeli amesma katika kuhakikisha ujangili unakabiliwa vilivyo, chuo chao kimekuwa kikitoa askari wanyamapori wengi waliohitimu mafunzo kuhusu mbinu za kukabiliana na usafirishaji haramu wa wanyamapori. 

Lowaeli alisema kuwa mafunzo hayo hutolewa na wakufunzi waliobobea kwenye masuala ya uhifadhi wanyaapori na ujuzi wanaoupata askari hao ni muhimu sana katika kusaidia jitihada za kukabiliana na usafirishaji haramu wa wanyamapori.

Akiongelea hali iliyopo sasa hivi, Mwindaji wa zamani na Mkazi wa Pugu, Samweli Mpipi (62) alisema kuwa wanaona Serikali na vikosi maalumu vikifanya kazi zake kwa ufasaha za kuzuia uhalifu na ujangili katika hifadhi lakini anasema kuwa haziwezi kuzaa matunda kama hazitaungwa mkono na Jeshi la polisi, wanakijiji, wadau wengine wa mazingira. 

“Hata hivyo ni vyema kuendeleza mapambano na kuendelea kutafuta mbinu madhubuti kukabiliana na majangili kwani hawachoki na wanabadili mbinu kila kukicha, hivyo jitihada ziendelee ili kuhakikisha ujangili unabaki historia katika nchi yetu,” anasisitiza Mpipi. 

Mkurugenzi Msaidizi na Mwenyekiti wa Kikosi kazi Taifa cha Kuzuia na Kupambana na Ujangili, Robert Mande anasema kuwa Serikali na Bunge ilivyotunga sheria ambayo inaitwaa ‘Permanent Sovereignty’, sheria namba 3 ya mwaka 2017 ambayo ipo kwenye katiba ibara ya 9 na ibara ya 27  katika kulinda rasimimali za taifa na kuhakikisha kwamba wananchi wanafaidika na rasiliamali, imesaidia sana katika usimamizi na utekelezaji

“Hiyo imetupa nguvu zaidi kwasababu imetoa uwanja mpana katika kulinda rasiliamali za nchi na kuhakikisha kwamba wananchi wanafaidika. Na kwakutumia sheria ya wanyamapori namba 5 ambayo inakataza watu kumiliki nyara na kuwinda kiharamu, inatupa nguvu ya kutekeleza na kusimamia sheria za wanyamapori,”. 

Akitilia mkazo suala la ulinzi na usimamizi kwenye hifadhi kupitia Jeshi USU, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Uhifadhi ya eneo la Ngorongoro, Freddy Manongi  ameeleza kuwa kuanzishwa kwa Jeshi USU ni maalumu kwa ajili ya kuongeza nidhamu na ukakamavu kwasababau kumekuwa na tuhuma nyingi kuwa askari wa wanyama pori wamekuwa wakionea watu na kuwa wanachukua rushwa hivyo jeshi hilo limekuja kuweka nidhamu na kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa na haswa kuutokomeza ujangili kabisa.

Pamoja na hilo Kamishna aligusia suala la shoroba (mapito ya wanyamapori) ambapo anasema, “Sheria ya mwaka 2009, namba 5 ya wanyamapori ilitambua hilo na ikaweka kipengele cha uhifadhi cha shoroba, na kukiri kuwa hawakuitekeleza ipasavyo kwahiyo unakuta maeneo mengi yalifungwa. 

“Mi ningeshauri yale maeneo yawe hifadhi za taifa kama kweli tunataka kuyalinda, ama yawe chini ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ama yawe chini ya TAWA kama Mapori ya Akiba kwa usimamizi zaidi, yani zipandishwe hadhi. ” alisema Manongi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles