NA JULIETH JULIUS, DSJ
RAIS Dk. John Magufuli, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mkesha mkubwa wa dua maalumu utakaofanyika Desemba 31, mwaka huu.
Mkesha huo umeandaliwa na Kanisa la Tanzania Fellowship of Churches na utafanyika katika Uwanja wa Uhuru.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Askofu wa TFC, Godfrey Malassy, alisema mkesha huo utakuwa ni wa kihistoria nchini kutokana na Mungu kuwatendea Watanzania mambo makuu kwa kuwapatia kiongozi mwenye uwezo na mcha Mungu.
“Mkesha huu utakuwa wa kihistoria na utafanyika katika mikoa 10 ikiwemo na Zanzibar na utakuwa na lengo la kuombea taifa letu pamoja na kumwombea rais wetu ili aweze kufanya kazi zake kwa kumtegemea Mungu.
“Katika kipindi kilichopita cha uchaguzi, kulikuwa na tetesi za kupotea kwa amani katika nchi yetu hasa Zanzibar, wengi walifikiria kuwa tutamwaga damu lakini taifa letu limekuwa la tofauti na tumepata kiongozi mwenye sifa za uchapakazi, mwadilifu, mcha Mungu na mkweli,” alisema Askofu Malassy.
Alisema katika mkesha huo kutakuwa na viongozi mbalimbli wa kiroho ambao wataongoza kutoa shukrani ya kipekee ya taifa kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata Tanzania Mpya.
Pia aliupongeza uongozi wa awamu ya tano kwa kufungua ubalozi wa Israel nchini baada ya miaka 19 kwani katika maombi waliyokuwa wakiomba lilikuwa ni mojawapo.