PENGINE nitasikika , lakini kimekuwa ni kilio changu kwa muda mrefu sana kuwa viongozi wetu hawaelewi utalii maana yake nini. Nimekuwa nikisema kuwa ainisho la utalii linaloongoza viongozi wetu ni lile lililoachwa na wazungu waliokuja Afrika wakati wa ukoloni, kuwa ni wanyama wa mwituni. Wakatuanzishia Hifadhi za Taifa za wanyama, basi na sisi tukabaki na ainisho finyu la utalii ambalo hata wao hawanalo.
Tulipoanza kugundua miaka ya karibuni kuwa utalii unaweza kutuletea pato kubwa sana kitaifa. Na kugundua pia kuwa utalii wa Watanzania wenyewe unaweza pia kuongeza maradufu pato hilo, tukaanza kuhimiza utalii wa ndani. Lakini ainisho likawa lile lile, la utalii wa kwenda mbugani. Tumeanzisha idara ya malikale (antiquities), lakini imeshindwa kujipambanua, aidha kwa sababu ya kukosa sheria au kwa sababu ya kukosa uwezeshaji au wao wenyewe hawajui wajibu wao (jambo ambalo sidhani kama ni kweli).
Lakini inakuwaje majengo ya kale ambayo yalipaswa kuhifadhiwa yanabomolewa. Mfano wa hivi karibuni ni wa Soko Kuu la Manispaa ya Morogoro. Kulikuwa na masoko mawili, moja lilijengwa na Wajerumani na jingine lilijengwa na Muingereza. Haya ni masoko yenye historia yake. Historia ya ukoloni, historia ya nani walikuwa wanauza wakati wote huo, historia ya aina ya ujenzi (architectural style), historia ya umiliki toka yalipojengwa hadi leo. Lakini ni hazina na kivutio cha utalii kwa wageni wa mji, wanahistoria, watalii wenyewe hasa kutoka Uingereza na Ujerumani, wanafunzi wa akiolojia, ujenzi na picha na wanafunzi wanaosoma utalii pia kwa sababu wanajifunza kutembeza wageni.
Nilidhani miji ingeweza kutumia majengo ya kale kama sehemu ya kujipatia fedha kwa sababu wageni wanapokuja kufanya ziara au semina wanaweza kuwekewa utaratibu wa kutembezwa kwa ada maalumu. Kuwa mkurugenzi anaweza kuwa na basi na kuuza utalii wa chakula, historia na utamaduni ndani ya mji wake kwa kuwapatia ziara hiyo wageni wa kutoka nje ya mji au nchi na hata wanafunzi wa sekondari na msingi wanaotaka kujua maeneo ya kihistoria ndani ya mji.
Wananchi wanapozoea utaratibu huu wanaweza kuutumia mara kwa mara kwa ajili ya kujielimisha na kujiburudisha.
Lakini silo ninaloliona. Nasikia ile sheria ilifutwa. Majengo yetu hatuyalindi tena na kuwapatia watu kama National Housing Corporation, na wamiliki wengine wa majumba hayo ya kale kujifanyia watakavyo. Maeneo ya kale ni kumbukumbu ya historia yetu ya utamaduni wetu wa sisi ni nani katika uhusiano wetu na mazingira na wageni kutoka nje.
Lakini ni fedha. Inakuwaje hazina hii inaachiwa watu wachache waipoteze. Waondoe kumbukumbu, ni kwa sababu ya kukosa mwelekeo au kukosa mwitikio wana utashi wa kisiasa au ni kwa sababu hatujui tutakacho tunapozungumzia utalii. Ulitolewa waraka kwa mikoa na wilaya juu ya kuimarisha utalii wa ndani. Lakini waraka huu umeingiwa na walakini kwa sababu viongozi wale wanaopaswa kusimamia wamekuwa wa kwanza kuruhusu maeneo ya kale kubomolewa.
Ndio maana naandika makala hii nikiomba Serikali ya JPM kuliangalia hili kwa jicho pevu. Kama utalii unaingiza asilimia 17 ya pato la Taifa nini kinazuia sekta hii kufikia hata asilimia 30 kwa nchi yenye vivutio anuai vya utalii… nadhani ni udhaifu katika kusimamia sekta na Serikali kutojua inataka nini, au wataalamu wetu wameshindwa kujieleza kwa Serikali.
Haiwezekani tukawa na sekta kubwa inayoweza kujiendesha yenyewe na kuendesha uchumi wa nchi halau ikaachwa iharibiwe kwa sababu ya uzembe au rushwa. Kama kweli Mheshimiwa JPM unakubaliana na sisi wengine kuwa utalii ni sekta muhimu kiuchumi, basi haya ya kuharibu vivutio vya utalii visimamishwe hata kama wanaofanya hivi ni idara za Serikali yenyewe.