24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

JPM awapa meno watendaji kata

*Awataka watoe taarifa za mawaziri, ma-RC, DC wanaokiuka misingi ya utawala bora katika maeneo yao

ANDREW MSECHU-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amewataka maofisa watendaji wa kata kutembea kifua mbele kwa kuwa mwajiri wao ni Rais wa Jamhuri ya Tanzania, na wao ndio wawakilishi wake katika kata zao.

Kauli hiyo aliitoa jana Ikulu, Dar es Salaam, alipokuwa akizungumza na watendaji hao wa kata nchi nzima.

Alisema kuwa anajua wana majukumu mengi na wanakumbana na changamoto kutoka kwa wakubwa wao, wakiwemo makatibu tarafa na wakurugenzi wa halmashauri, lakini pia kwa nafasi yao wanaweza kuwawajibisha viongozi hao.

“Nimewaita hapa leo (jana) ili kuwapa meno, mtambue kuwa ninyi ni mabosi, asitokee yeyote wa kuwatisha, tembeeni kifua mbele. Nyie ndio mnaosimamia kata zenu, mna wajibu wa kuhakikisha maelekezo ya Serikali yanatekelezwa kikamilifu kwa ajili ya kuwezesha uelewa kwa wananchi.

“Akitokea kiongozi yeyote niliyemteua anamnyanyasa kiongozi wa kata, nitamuona hatoshi, na nitasikitika zaidi akitokea kiongozi yeyote wa kata akimnyanyasa mwananchi wangu aliyekaa juani akanipigia kura, naye nitamuona hatoshi,” alisema.

Alisistiza kuwa cheo cha ofisa mtendaji wa kata si nafasi ndogo kwa kuwa ndio wawakilishi wake katika ngazi ya kata na wanapozungumza mafanikio ya Serikali ndiyo wasimamizi wa mwanzo katika mafanikio hayo, hivyo wanatakiwa kutembea kifua mbele, wasitishwe na yeyote.

Alisema ameamua azungumze nao kwa kuwa huenda wamekosa sehemu ya kuzungumzia kwa kuwa hana uhakika kama wamewahi kuitwa na wakuu wa wilaya au maofisa watendaji wa wilaya kuzungumza kuhusu yale yanayoendelea katika maeneo yao

Aliwataka kutembea kifua mbele kwa kuwa mtendaji wa kata ni mtu mkubwa katika kata hiyo kwa kuwa yeye ndiye bosi, ndiyo sababu ya kuwaita ili kuwapa meno ya kujitambua kuwa wao ni mabosi.

“Sasa akatokee mwingine huko awaambie nyie sio mabosi, mwambieni aje aniambie mimi nione kama ana ujasiri wa kusema hivyo. Ninawaelekeza tembeeni kifua mbele, nawaambieni katika hii nchi hakuna mdogo hakuna mkubwa, sisi wote tuko ‘at par’ (tuko sawa),” alisema.

Alimtaja mtendaji wa Kata ya Mtumba na kusema yeye ndiye mwenye kata na kwamba ndiye msemaji, na viongozi wote wanaoishi katika kata hiyo, akiwemo yeye na mawaziri wote ambao ofisi zao zimehamishiwa Dodoma wanawajibika kwake.

WAJIBU, MAJUKUMU

Rais Magufuli alisema watendaji wa kata ndio viongozi walio karibu zaidi na wananchi, wanaomwakilisha yeye katika maeneo yao na wanaoelewa zaidi changamoto zilizoko huko, hivyo ni muhimu kwao kuelewa vyema mwelekeo wa Serikali ili watekeleze wajibu wao kuelekea huko.

“Wajibu wao mkubwa ni kutatua kero za wananchi, wao ndio wako karibu na wananchi, wajiwekee utaratibu wa kukutana na wananchi na kutatua kero zao na wasisubiri wananchi kuinua mabango wakati wa ziara za viongozi wa juu,” alisema.

Rais Magufuli alisema kero hizo zinahusu migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji, dhuluma, kubambikiwa kesi, kero katika huduma za jamii ikiwemo afya, maji, elimu na kuwataka kuwafuata wananchi.

Aliwataka pia kuacha kuuza ardhi kiholela kwa kuwa baadhi yao wamegeuka madalali wa kuuza ardhi na kusababisha migogoro.

Alisema viongozi hao wa kata jukumu lao ni kubwa ikiwamo kuhakikisha maeneo yao yanakuwa salama, kudhibiti uhalifu ili wananchi wafanye kazi zao bila hofu wala bughudha.

“Hivyo watendaji wa kata milioko mipakani hakikisheni hakuna mgeni anayeingia na kupewa Kitambulisho cha Taifa wakati upo.

“Ulinzi wa kata nzima upo mikononi mwenu, shirikianeni vizuri na watendaji wa vijiji kuwabaini wageni wanaoingia kwenye maeneo yenu,” alisema.

Alisema jukumu jingine ni kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

“Bebeni kikamilifu dhamana zenu za uongozi, endapo kuna kero zilizo juu ya uwezo wenu zibebeni kwa viongozi wa juu, wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya,” alisisitiza.   

Pia, alisisitiza kuwa uwepo wao hautakuwa na maana endapo wananchi watakuwa na kero, akiwataka kuhakikisha  zinatatuliwa kikamilifu.

 “Kila kero mnayoshughulikia hakikisheni inapata suluhu. Msiishie njiani. Wananchi wanyonge wanapata shida sana, wasaidieni,” alisema.

Mbali na jukumu hilo, Rais Magufuli pia aliwakumbusha maofisa hao kusimamia fedha za Serikali katika miradi ya maendeleo.

“Serikali imekuwa ikipeleka hela nyingi kwenye miradi ya elimu, kila mwezi Serikali imekuwa ikipeleka Sh bilioni 23.863 nchi nzima, kwenye afya, kwenye maji na barabara. Ni jukumu lenu kuhakikisha fedha zilizoletwa zinatumika kikamilifu,” alisema.  

Alikumbusha pia jukumu la maofisa hao kuhakikisha maelekezo ya Serikali yanawafikia wananchi ili kutatua kero zao.

“Mathalani Serikali imefuta ushuru wa kusafirisha mazao yasiyozidi tani moja na tozo mbalimbali kwenye kilimo zaidi ya 80, uvuvi karibu tano, mifugo zaidi ya tozo saba,” alisema.

Alitaja pia suala la vitambulisho vya wafanyabiashara ndogo zenye mitaji isiyozidi Sh milioni nne kwa mwaka, akisema watatakiwa kulipa ushuru wa Sh 20,000 pekee.

Alisisitiza kuwa anajua wapo ambao hawajafurahia hatua hiyo kwa kuwa walikuwa wakiwanyanyasa wafanyabiashara hao na kuwatoza viwango vikubwa vya ushuru kwa mwaka.

MSHANGAO

Rais Magufuli alisema atashangaa iwapo watendaji hao hawatawahamasisha vijana na wananchi kujitokeza kuchangamkia fursa za kazi na za biashara zinazojitokeza katika maeneo yao ambayo miradi mikubwa ya Serikali inatekelezwa.

Alisema watendaji hao ndio wenye jukumu la kuwasimamia vijana wa maeneo yao na kuwadhamini ili kufanya kazi katika miradi hiyo.  

Aliwataka kutambua kuwa wao ndio kioo cha Serikali katika maeneo yao, hivyo wakijihusisha na matendo yasiyo na maadili wanaichafua.

“Zingatieni sheria, katiba na kanuni za nchi katika kutekeleza majukumu yenu, mkasimamie haki, haki itawalinda, haki inaenda pamoja na amani, haki inaenda pamoja na utukufu wa Mungu, kazingatieni haki, kasimamieni sheria, kazingatieni katiba na sheria za nchi, msizivunje,” alisema.

MAFANIKIO YA SERIKALI

Mbali na majukumu hayo, Rais Magufuli aliwataka maofisa hao kusemea mafanikio ya Serikali na kuyatetea.

 “Umeme katika miaka mitatu iliyopita, vijiji vilivyokuwa na umeme wa REA (Wakala wa Nishati Vijijini) vilikuwa 2,230, sasa vijiji ni 7,000 vilivyopatiwa umeme. Vituo vya afya katika kata zetu, ninyi ni mashahidi, vituo zaidi ya 352 vimekamilika,” alisema.

KUWAJIBISHA VIONGOZI

Rais Magufuli alisema watendaji hao wana jukumu la kutoa taarifa kuhusu wakurugenzi, mawaziri na wakuu wa mikoa wanaofanya matendo yanayokiuka misingi ya utawala bora.

“Mtendaji wa kata ndio bosi wa eneo lake, hata kama kuna kiongozi wa nafasi gani yuko chini yako na anapoonekana kuenenda visivyo, unapaswa kumwajibisha au kutoa taarifa kwa mamlaka yake.

“Katika kata kuna mkurugenzi wa halmashauri, RC (Mkuu wa Mkoa), waziri au nani, wewe (mtendaji kata) ndio msimamizi, kama wewe upo katika kata na ambayo kuna waziri, RC, mkurugenzi sijui nani wewe ndio msimamizi.

“Usiogope kumlima (barua) na kumwandikia maoni, hata kama anakuzidi cheo, kwamba katika kata hii namwona mtumishi huyu anakwenda kinyume na maadili. Na ukimwona ni mkubwa sana, piga nakala hapa kwangu, lazima watu tujifunze kuogopana.

“Unakuta kuna kiongozi kila siku anapigana baa katika kata yako, hadi mwenye baa anafunga baa yake. Kwa sababu ni mkubwa unaacha kumripoti, charaza kalamu na ndio maana watendaji kata wana kalamu na saini zao,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles