25.2 C
Dar es Salaam
Monday, December 2, 2024

Contact us: [email protected]

Kigogo OBC, wafanyakazi waachiwa huru, wakamatwa

JANETH MUSHI – ARUSHA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, jana imewaachia huru raia 10 wa kigeni na Mkurugenzi wa Kampuni ya wawekezaji ya Otterlo Business Cooperation (OBC) kutoka Falme za Kiarabu, Isack Mollel (59), baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuwasomea maelezo ya awali kwa zaidi ya mara nne.

Hata hivyo, baada ya kuachiwa huru na shauri hilo kufutwa, watuhumiwa hao walikamatwa tena na polisi na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Niku Mwakatobe, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Janeth Sekule na Mwendesha Mashtaka wa Serikali kutoka Idara ya Kazi, Emmanuel Mweta huku Mollel akitetewa na mawakili Method Kimogogoro, Daudi Haraka, Elvaison Maro na Goodluck Peter.

Shauri hilo la jinai namba 74 la mwaka huu, lilipangwa kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali na kuanza kusikilizwa kwa mashahidi wa Jamhuri.

Wakili Janeth alidai hawako tayari kuwasomea hoja hizo kwa madai kuwa hajajiandaa.

“Kama nilivyoainisha, takribani wiki mbili nilikuwa na matatizo, sikuwepo na leo ndiyo nimeingia ofisini na kukutana ma tarehe hii ya shauri husika, sikuwa nimejiandaa,” alidai.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Niku alisema awali washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 7, mwaka huu na kuwa ni zaidi ya miezi sita ‘facts’ hazijaendelea.

“Licha ya kila mara mahakama kusema inaahirisha shauri hili kwa sababu ya Jamhuri kushindwa kuendelea na kesi (kuwasomea hoja za awali), mahakama inawaachia huru chini ya kifungu cha 225(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, washitakiwa mko huru, mnaweza kwenda,” alisema.

Awali kabla ya uamuzi huo wa Hakimu Niku, Wakili Maro aliieleza mahakama hiyo kuwa hili lilikuwa ahirisho la mwisho kwa upande wa Jamhuri na kuwa wanaiomba mahakama ipange kesi hiyo tarehe za karibuni, ikiwezekana ipangwe Septemba 9, ili wateja wao waweze kusomewa hoja za awali na kesi kuendelea kusikilizwa.

Baada ya watuhumiwa hao kuachiwa huru, walikamatwa tena na polisi waliokuwa mahakamani hapo na kuondolewa kwa gari lililokuwa na namba za usajili T 125 DFQ saa 4:41 asubuhi.

Mollel anashikiliwa Gereza la Kisongo jijini hapa kwa kuwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Katika shauri hilo, Mollel anakabiliwa na mashtaka 37 ya kujihusisha na kuajiri raia 37 wa kigeni wasiokuwa na vibali halali vya kufanya kazi nchini wala cheti cha msamaha, kinyume na sheria ya kuratibu ajira na mahusiano ya wageni.

Mollel anaungana na raia 10 wa kigeni waliokuwa wakifanya shughuli mbalimbali, ikiwemo ufundi magari, ufundi matairi, wapishi, madereva na wapaka rangi nyumba, ambao waliajiriwa OBC iliyopo eneo la Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro mkoani hapa ikijishughulisha na shughuli za uwindaji wa kitalii.

Washtakiwa wengine ni Darweshi Jumma, Riaz Aziz Khan, Mohammad Tayyab, Ali Bakhsh, Abdul Rehman Muhammad, Martin Crasta, Imtiazd Fiaz, Arshad Muhammad, Hamza Sharif na Zukfiqar Ali.

Awali Agosti 21 mwaka huu mawakili wa utetezi katika shauri hilo waliulalamikia upande wa Jamhuri kukwamisha shauri hilo kuendelea kusikilizwa.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mawakili wanaohusika wameenda kwenye mafunzo Dar es Salaam, hivyo kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine.

Kufuatia maelezo hayo, Wakili Haraka alidai mahakamani hapo kuwa hii ni mara ya nne kwa shauri hilo kuahirishwa kwa madai kuwa mawakili wanaopaswa kuwasomea hoja hizo wana dharura.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles