Na Mwandishi wetu -Dar es Salaam
RAIS John Magufuli, ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwangu na Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo, Bakari Mohamed.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku chache tangu afanye ziara wilaya humo na wananchi kulalamikia ujenzi wa soko na stendi.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msingwa, Rais Magufuli amemteua Hashim Komba kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo. Kabla ya uteuzi huo, Komba alikuwa Katibu Tawala Wilaya ya Iringa.
Pia amemteua Hassan Rungwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ya Nachingwea.
Taarifa ya Ikulu pia ilisema pia Rais amemteua Mathias Kabunduguru kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania.
Ilisema kabla ya uteuzi huo, Kabunduguru alikuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia elimu.
Ilisema Kabunduguru anachukua nafasi ya Hussein Katanga ambaye ameteuliwa kuwa balozi. Ilisema pia Rais amemteua Godfrey Mweli, kuwa Naibu Katibu Mkuu Tamisemi (anayeshughulikia elimu).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, kabla ya uteuzi huo Mweli alikuwa Mkurugenzi wa Mipango, Wizara ya Sheria na Katiba.
JPM akiwa Nachingwea
Rais Magufuli akiwa wilani Nachingwea Oktoba 16, wananchi waliwalalamikia viongozi wa wilaya hiyo juu ya ujenzi wa soko na stendi ambapo Rais aliamua kutembelea soko lililokuwa likilalamikiwa.
Rais Magufuli aliamua kwenda kuliona soko hilo baada ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Mohamed, ambaye uteuzi wake umetenguliwa kusema Sh milioni 71 zimeshatumika, lakini ujenzi haujakamilika kwa mwaka sasa haujakamilika.
Rais alieleza kukasirishwa kwake na kutotumika kwa fedha zinazotengwa kwa miradi ya maendeleo, hivyo kuwataka watendaji wa Serikali, kuanzia Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, na DED Mohamed wahakikishe wanatekeleza wajibu wao.
“Huyu DED (Mohamed) anadai tukusanye kwanza mapato, sasa kwanini usitumie kwanza hizi ili ukusanye zaidi?” alihoji.
Alisema Mkurugenzi Mohamed amemuudhi na kumtaka DC Muwango awe mkali kwa kuwa yeye ndiye Mkuu wa Kamati ya Usalama ya Wilaya.
“Na wewe Mkuu wa Mkoa unapotoa maagizo ni lazima uyafuatilie yanatekelezwaje, ninataka watendaji wanaofanya kazi, kero niliyoikuta pale Nachingwea lazima nyie viongozi muwajibike.
“Soko halijamaliza kujengwa, milioni 71 zimetumika, Mkurugenzi anajifanya amekaa Marekani sijui Marekani alikuwa anokota makopo huko, kwa sababu mambo mengine yanaudhi sana kwa sababu fedha zinazotolewa na Serikali zinatakiwa zikatumike kwa ajili ya maendeleo.
“Stendi mmewahamisha watu, mmewapeleka stendi nyingine wakati bado haijakamilika. Sasa ninaagiza watendaji wa wilaya hii ya Nachingwea mkajipange upya, kama kuna anayetaka kufanya kazi afanye na asiyetaka aondoke,” alisema.