Serikali, Barick zaingia ubia kuunda Kampuni ya Twiga Minerals kusimamia migodi mitatu

0
1195

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Barrick Corporation, zimeingia ubia na kuunda kampuni moja ya pamoja inayojulikana Twiga Minerals Company Ltd.

Kampuni hiyo ambayo imeandikishwa na kusajiliwa hapa nchini Makao Makuu yake yatakuwa jijini Mwanza itasimamia migodi ya Bulyankulu, Buzwagi na North Mara, lakini pia katika kila mgodi serikali ina asimilia 16 na Barick asilimia 84.

Akitangaza hatua hiyo kwa umma mbele ya waandishi wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumapili Oktoba 20, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amesema katika kampuni hiyo, Barick ina asilimia 84 na serikali asilimia 16.

“Kampuni hii imeundwa baada ya Kampuni ya Acacia ambayo Barrick Gold alikuwa na asilimia 63.9 na nyingine zilikuwa kwa wanahisa wadogo na kampuni ya Barrick kununua hisa zote ikawa na hisa 100 na baadaye kuifuta Kampuni ya Acacia ambayo ilikuwa na Makao Makuu London. Kwa hiyo sasa Acacia imekufa haipo na badala yake imekuja Kampuni ya Twiga,” amesema Profesa Kabudi.

Akizungumzia mchakato wa kuanzisha kampuni hiyo, Profesa Kabudi amesema Machi 2017, Rais Dk. John Magufuli aliwatangazia wananchi na dunia kwamba serikali ina mgogoro na Acacia iliyokuwa inaendesha migodi ya Buzwagi na North Mara kwa vitendo vilivyokuwa vinaifanya ipoteze mapato akaunda tume mbili.

“Baada ya hapo tukawa katika mgogoro mkubwa na ndipo Mwenyekiti wa Barrick alipoamua kuja nchini wakakubaliana na rais na kuanza mazungumzo.

“Tulianza mazungumzo na Timu ya Barrick ambapo yalikamilika Oktoba mwaka 2017 kwa kutia saini kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick kwamba sasa tumekubaliana moja; kuchangia faida za kiuchumi 50/50, kuunda kampuni mpya, kuhakikisha tunabadilisha mtindo wote wa uendeshaji wa migodi hiyo, kufunga ofisi ya London, kufunga ofisi ya fedha iliyokuwa Johannesburg na mambo yote kufanyika hapa nchini kuendana na mfumo wa mabadiliko tuliyoyafanya,” amesema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here