27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM amwaga takwimu za mafanikio

 NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM 

RAIS Dk. John Magufuli, amevunja Bunge la 11 na kutaja takwimu za mafanikio yaliyopatikana kipindi cha awamu ya kwanza ya uongozi wake tangu alipoingia Ikulu mwaka 2015. 

Katika hotuba yake ya zaidi ya saa mbili jana, Rais Dk. Magufuli alijikita kueleza takwimu za mafanikio katika ukuaji wa uchumi, miradi ya kimkakati, sekta kuu za uzalishaji, biashara za nje, utatuzi wa kero, uhusiano wa kimataifa, usimamizi wa sheria na utoaji haki.

Alisema Seriali imejitahidi kukuza sekta kuu za uchumi na uzalishaji kama vile viwanda, kilimo, biashara, madini pamoja na utalii sambamba na kuimarisha sekta za ulinzi, sayansi, teknolojia, habari, misitu, ufugaji nyuki na nyingine. 

Alisema uchumi miaka mitano umekua kwa asilimia 6.9 kutoka ukuaji wa asilimia 6.2 (2015), huku pato ghafi la Serikali likiongezeka kutoka trilioni 94.345 hadi trilioni 139.9 (2019) na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 zenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika. 

Alisema pia wamefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei kutoka asilimia 6.1 hadi asilimia 4.4. 

“Akiba ya fedha za kigeni imeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 4.4 kwa miezi minne hadi Dola bilioni 5.3 ambazo zinatosheleza kununua bidhaa na huduma kwa miezi sita pointi mbili, na kiwango hicho ni zaidi ya lengo lililowekwa katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ( SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). 

“Umaskini wa kipato umepungua hadi asilimia 26.4, na Februari 2020 tulizindua awamu ya tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF 111), utakaogharimu shilingi trilioni 2.032,” alisema. 

Alisema katika kipindi hicho, ajira 6,032,269 zimezalishwa na kati ya hizo 4,056,576 zilizalishwa na sekta isiyo rasmi. 

MIRADI YA KIMKAKATI 

Alisema juhudi za kufufua usafiri wa anga zimeongeza wasafiri kutoka milioni 4.8 mwaka 2015 hadi milioni 5.8 (2018/19). 

Alisema ndege mpya 11 zimenunuliwa na nyingine zinaendelea kutengenezwa. 

Alisema ujenzi wa viwanja 11 upo hatua mbalimbali na wapo mbioni kumpata mkandarasi wa kujenga kiwanja kikubwa eneo la Msalato, Dodoma sambamba na barabara ya kilomita 110 ya njia nne. 

“Tumejenga rada Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza, Songwe ujenzi unaendelea kukamilika. “Watanzania waliokuwa wamekwama nchi mbalimbali ikiwemo India wameweza kurejeshwa kwa sababu ya kuwa na ndege zetu,” alisema. 

UMEME 

Alisema mradi wa kinyerezi 11 unatarajiwa kuzalisha megawati 240 na ule wa Kinyerezi 1 utakaozalisha megawati 325 nao unaendelea kukamilishwa. 

“Mradi wa Bwawa la Nyerere ulipigwa vita sana,tumefanikiwa na gharama ya mradi huu ni Sh trilioni 6.5 na fedha zote zinatolewa na Watanzania, utakapokamilika utazalisha megawati 2,500 na utatusaidia kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira linalosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa,” alisema. 

Alisema pia Serikali imekamilisha miradi mikubwa ya kusafirisha umeme maeneo ya Iringa, Shinyanga, Makambako, Songea, Lindi, Mtwara na mengine. 

Kwa upande wa vijiji vilivyounganishiwa umeme, alisema vimeongezeka kutoka 2,018 (2015) hadi 9,112 (Aprili 2020) na kati ya vijiji 12,268 vilivyopo nchini, vimebaki 3,156 tu na kuahidi wakichaguliwa watavimalizia. 

Alisema watumiaji umeme wameongezeka kutoka asilimia 35 hadi 85 na mafanikio hayo, yamechagizwa na ushushaji wa gharama za kuunganisha umeme kutoka Sh 177,000 hadi Sh 27,000. 

“Katika kipindi chote cha miaka mitano nchi yetu haikuwahi kuingia gizani, tumeokoa kiasi kikubwa cha fedha (Sh bilioni 719 kwa mwaka), zimeokolewa kwa kuzima mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL na Agreco na kusaidia Tanesco lianze kujiendesha lenyewe,” alisema Rais Magufuli. 

SEKTA KUU 

Alisema viwanda vimeongezeka kutoka 52,633 (2015) hadi 61,110 (2020) na viwanda vipya ni 8,477 na kati ya hivyo, vikubwa ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406, vidogo sana 4,410 ambavyo kwa pamoja vimezalisha ajira 482,601. 

“Tumeendelea kuweka mkazo sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji, sekta hii bado ni uti wa mgongo. Inazalisha fedha za kigeni kwa asilimia 25, Pato la Taifa asilimia 30, asilimia 65 malighafi za viwandani, asilimia 70 ya ajira zote nchini na asilimia 100 ya mahitaji yetu ya chakula. 

“Tumeendelea kuipa kipaumbele sekta hiyo kwa kuhakikisha kuna upatikanaji wa mbegu bora, mbolea, viuatilifu, matrekta, uzalishaji miche ya mazao ya kimkakati, tumefufua masako ya mazao, skimu za umwagiliaji, tumeimarisha vyama vya ushirika,” alisema. 

Kwa upande wa ufugaji, alisema maeneo ya ufugaji yameongezeka kutoka hekta milioni 1.4 hadi milioni 5 (2020), huku ng’ombe waliohamilishwa wakiongezeka kutoka 105,000 (2015) hadi 514,700 (2020). 

Kwa upande wa wafugaji samaki, alisema wameongezeka kutoka 18,843 hadi 26,474 (2020) na mabwawa yameongezeka kutoka 22,545 hadi 26,445, huku vizimba vya kufugia samaki vikiongezeka kutoka 109 hadi 431. 

“Tumeimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi na kudhibiti matumizi ya uvuvi haramu, nakumbuka kuna wakati Waziri wa Mifugo na Uvuvi, alikuwa akitembea na rula hadi kwenye migahawa, hii ilikuwa ni katika kazi ya kuhakikisha tunapata mafanikio,” alisema. 

Alisema pia mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), umeongozwe kwa Sh bilioni 208 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Serikali pia imeipitia Sh bilioni 57.8 kuiwezesha kutoa mikopo zaidi hasa kwa wakulima wadogo waogo na makampuni ya kati.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, hadi sasa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 166.9 kutoka katika benki hiyo imetolewa kwa wakulima. 

Alisema pia sangara wameongezeka kutoka tani 417,936 (2016) hadi tani 816,864 (2020), huku mauzo ya samaki nje ya nchi yakiongezeka kutoka Sh bilioni 379 (2015) hadi Sh bilioni 692 (2020). 

“Kutokana na marekebisho ya sheria mbalimbali tumefanikiwa kupunguza urasimu kufuta tozo 114 za kilimo, uvuvi na ufugaji, na tozo 54 za sekta nyingine na tano zilizokuwa zinatozwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA),” alisema Rais Magufuli. 

BIASHARA NJE 

Kwa upande wa mauzo ya bidhaa mbalimbali nje, alisema yameongezeka kutoka Sh trilioni 11.5 hadi Sh trilioni 16.6. 

Alisema katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), bidhaa za Tanzania zimekuwa na urali chanya kwa wastani wa Dola za Marekani bilioni 288.04 na Kituo cha Uwekezaji (TIC) kimesajili miradi 1307 yenye thamani ya Dola bilioni 14.6 itakayotoa ajira 183,503. 

MADINI 

Rais Maguful, alisema mageuzi makubwa yaliyofanyika sekta ya madini yamesaidia kuongezeka kwa mapato kutoka Sh bilioni 194 hadi Sh bilioni 349. 

 Alisema kupitishwa kwa Sheria ya Kulinda Rasilimali za Taifa ya 2017, kumewezeha kwa mara ya kwanza Watanzania kumiliki rasilimali zao na kuanzishwa kwa Kampuni ya Twiga ambapo Serikali ina hisa asilimia 16 na Barick asilimia 84. 

“Mwaka huu Sh bilioni 470 zinatarajiwa kukusanywa, Aprili, mwaka huu, licha ya corona Sh bilioni 58 zimekusanywa, haijawahi kutokea kiwango cha juu kabisa kilikuwa Sh bilioni 43. 

“Mageuzi makubwa yamefanyika, ikiwa ni pamoja na kudhibiti utoroshaji na usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi, kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara wadogo kwenye mnyororo wa uchumi wa madini, kuwafutia viwango vya kodi,” alisema. 

UTALII 

Rais Magufuli alisema mapato ya utalii yameonngezeka kutoka Sh bilioni 1.9 (2015) hadi Sh bilioni 2.6 (2019) sambamba na idadi ya watalii kutoka milioni 1.1 hadi milioni 1.5. 

Alisema kuanzishwa kwa jeshi usu kumesaidia kudhibiti vitendo vya ujangiri na kuwezesha wanyama waliokuwa hatarini kutoweka kuongezeka kama vile faru kutoka 162 hadi 190, huku tembo wakiongezeka kutoka 43,330 (2014) hadi 51,269. 

Alisema hifadhi tano zimeanzishwa ambazo ni Nyerere, Chato, Rumanyika, Ibanda Kyerwa na Karagwe pamoja na kuanzisha chaneli malaumu ya utalii katika teleshine ya taifa. 

SANAA NA UTAMADUNI 

 Rais Magufuli aliema shughuli za sanaa na burudani ziliongoza kwa ukuaji mwaka 2018 ambapo sekta hiyo ilikua kwa asilimia 13.7 na kwamba mwaka 2019 ilishika nafasi ya tatu kwa ukuaji wa asilimia 11.2.

“Wasanii na wanamichezo kazi zenu si tu zinaburudisha na kuchangia ukuaji uchumi lakini pia zinaitangaza nchi yetu kimataifa, naipongeza timu ya Taifa kwa kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

“Serikali imejipanga katika miaka mitano ijayo kuweka mkazo mkubwa zaidi kwenye sekta hiyo, ni sekta iliayoajiri vijana wetu wengi,” alisema Rais Magufuli.

SHERIA, UTOAJI HAKI

Rais Magufuli, alisema Serikali iliteua majaji 17 wa Mahakama ya Rufani na 52 wa Mahakama Kuu na kuajiri watumishi wa mahakama 859 wakiwemo mahakimu 396.

Alisema mahakamau kuu mpya mbili zimejengwa na kwamba mahakama za hakimu mkazi zimejengwa tano, za wilaya 15 za mwanzo 18 na mahakama za kutembea ambazo zimeanza kufanya kazi mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza na hadi Machi, mwaka huu, mashauri 337 yalisajiliwa.

Pia alisema mahabusu 2,812 wamefutiwa kesi sambamba na kushughulikia ucheleweshaji, ubambikkaji wa kesi na mrundikano wa wafungwa.

UTATUZI WA KERO

Alisema wakulima, wavuvi, wafugaji na wafanyabiashara wamefutiwa tozo 114 zilizokuwa zikikwamisha shughuli zao.

“Kwa wafanyakazi tumeshughulikia upandishwaji vyeo na malipo ya madeni mbalimbali, kodi ya mapato tumepunguza kutoka asilimia 11 hadi 9 na kulipa deni la trilioni 11.2 ambalo Serikali ilikuwa ikidaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii,” alisema.

Alisema pia wajasiriamali wadodo wadogo wakiwemo bodaboda, bajaji na mamalishe milioni 1.5 wamepatiwa vitambulisho na kuwafanya waondokane na usumbufu uliokuwepo.

Kuhusu mikopo isiyo na riba inayotolewa kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu kutoka katika mapato ya ndani ya halmashauri alisema hadi Machi Sh bil 93.2 zimetolewa.

“Tumeshughulikia migogoro ya ardhi kwa kuanzisha ofisi za ardhi kwenye mikoa yote, maeneo ya viwanja yaliyorathimishwa ni 464,158, hati miliki za kilima zilizotolewa ni 515,474 na kuvirasimisha vijiji 920 vilivyokuwa kwenye maeneo ya hifadhi na kuondoa migogoro kwa wananchi,” alisema Rais Magufuli.

UHUSIANO KIMATAIFA

Rais Magufuli alisema balozi mpya nane zimefunguliwa na kwamba Ethiopia na Poland nazo zimefungua balozi zao nchini.

Alisema pia askari 2,305 wako katika nchi mbalimbali wakilinda amani kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jumuiya ya Afrika ya Kati, Lebanon na Sudani Kusini.

“Nchi yetu imeaminiwa kuogoza EAC na SADC na tumefanikiwa kuzishawishi nchi wanachama kuridhia lugha ya Kiswahili kutumika kwenye taasisi hizo, haya yote ni mafanikio tuliyoyapata,” alisema.

KUHAMIA DODOMA

Rais Magufuli alisema; “Aprili 2019 nilizindua mji wa Serikali pale Mtumba, tumetekelza ahadi yetu zaidi ya tulivyoahidi, nina imani kwa kutekeleza ndoto hiyo si tu tumemuenzi Baba wa Taifa bali wajumbe wa mkutano wa Tanu waliofanya uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya nchi yetu mwaka 1973.

UCHAGUZI MKUU

Rais Magufuli aliwahakikishia Watanzania uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, utakuwa huru na wa haki na kuvitaka vyama na wanasiasa kujiandaa kushiriki kikamilifu.

“Tutasimamia uhuru na haki wa vyama vyote na hii ndiyo demokrasia ya kweli, navisihi vyama vya siasa na wanasiasa kujiandaa vizuri kushiriki katika uchaguzi huu. 

“Navihimiza vyama kutoka fursa za kutosha kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu, nawasihi wagombea kuepuka matusi na vurugu nchi hii ni yetu sote tujiepushe sana shetani wa matusi, tumtangulize Mungu katika kampeni zetu, matusi na kejeli hayajengi, sisi sote ni wamoja, tukabisheni kwa hoja na kushindanisha ilani yetu. 

“Atakayetaka kuleta vurugu namtahadharisha kwamba Serikali ipo macho, uchaguzi haumaanishi kwamba Serikali imeenda kulala, Serikali itaendela kuwepo kusimamia sheria na taratibu za nchi. Kipindi cha uchaguzi kikaishe salama tukiwa bado tunaupeleka Utanzania wetu mbele,” alisema Rais Magufuli.

AWAPONGEZA VIONGOZI

Katika hotuba yake, Rais Magufuli aliwamwagia sifa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai, mawaziri, katibu mkuu kiongozi, makatibu wakuu na viongozi wengine wa Serikali.

“Dk. Shein anamaliza muda wake, nampongeza kwa utumishi uliotukuka, akiwa makamu wa rais kwa miaka 8 na akiwa Rais wa Zanibar kwa miaka 10, kazi umeifanya. 

“Ameweka historia ya namna yake katika utumishi wa umma na ametoa mchango mkubwa kwenye taifa letu. Namtakia kila la kheri na tunamuahidi kuendelea kumuenzi kama tunavyowaenzi viongozi wengine wastaafu.

“Namshukuru makamu wa rais, mwanamama jasiri na shupavu kwa kunisaidia majukumu, nampongeza waziri mkuu kwa heshima na unyenyekevu wake, uchapakazi wake mzuri, amenisaidia sana.

“Mawaziri walinivumilia sana hawakuwa na uhakika na uwaziri wao,wamechapa kazi sana,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles