24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

shule zifunguliwe Juni 29

 RAMADHAN HASSAN-DODOMA

RAIS Dk. John Magufuli, ametangaza kufunguliwa shule za msingi na sekondari na shughuli zote kuanzia Juni 29, mwaka huu, baada ya kupungua maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Amesema ugonjwa wa corona, ni kati ya changamoto kubwa zilizoikumba nchi katika kipindi cha uongozi wake lakini Serikali imefanikiwa kuudhibiti. 

Akizungumza jana wakati wa kuvunja Bunge la 11, alisema uamuzi uliochukuliwa na Serikali kukabili ugonjwa huo ulikuwa sahihi, ndiyo maana Serikali imefanikiwa kuudhibiti.

“Napenda nitumie nafasi hii kutangaza kuanzia Juni 29, mwaka huu, ninafikiri itakuwa Jumatatu shule zote zifunguliwe na shughuli nyingine ambazo tulizuia kama kufunga ndoa…tumewachelewesha watu kuoana.

“Maisha lazima yarudi kama ilivyokuwa zamani, hata hivyo naendelea kuwasihi Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wetu wa afya,” alisema Rais Magufuli.

Alisema utabiri uliotolewa asilimia 60 ya nchi za Kusini mwa Afrika zilizopo Jangwa la Sahara zitashuhudia ukuaji hasi wa uchumi, lakini Tanzania kutokana na hatua zilizochukulia uchumi hautakua kwa ukuaji hasi.

Rais Magufuli pia alimpongeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, kwa kazi nzuri aliyoifanya kukabiliana na janga hilo.

“Nampongeza kwa namna ya pekee, mwanamama jasiri Waziri wa Afya, Ummy kwa uvumilivu wake, nataka niseme kwa dhati nilimtesa sana waziri huyu kwa sababu simu nilikuwa nampigia hadi saa nane usiku…naomba niombee msamaha kwa mume wake,” alisema.

Alilishukuru Bunge kwa kupitisha azimio la kumpongeza na kusema pongezi hizo zinastahili Watanzania wote na Bunge hilo, kwani liliendelea na vikao vyake kama kawaida.

“Ingawa nafahamu wapo wachache waliokimbia na sijui kama wamesharejea, kukimbia halikuwa jambo sahihi kwa sababu matatizo au changamoto hazikimbiwi, kukimbia changamoto ni ishara ya udhaifu, lakini pia ni ishara ya woga, kutojiamini.

“Siku zote njia sahihi ni kukabiliana na matatizo ndiyo sababu sisi tuliamua kukabikiana na ugonjwa wa corona tukiwa tumemtanguliza mwenyezi Mungu na kwa kufanya hivyo, tumeweza kutatua kwa kiasi kikubwa na kupunguza athari za kiuchumi,” alisema Rais Magufuli.

WAZIRI WA ELIMU

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema leo wizara yake itatoa ratiba ya mitihani kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, huku akisisitiza wanafunzi watasoma mfululizo mpaka Desemba bila kupumzika.

Alisema wanafunzi wanatakiwa kujiandaa vizuri pindi watakapokuwepo shuleni, kwani watasoma mfululizo mpaka Desemba.

“Wanafunzi sasa huu ni wakati wa kusoma si kulala lala, tukirudi ni kusoma tu mfululizo mpaka mwezi Desemba, tunataka kukamilisha kila kitu baada ya kutokusoma kwa muda mrefu,”alisema Profesa Ndalichako. 

Akitoa tathmini yake ya miaka mitano katika wizara hiyo, alimshukuru Rais Dk. Magufuli kwa kutoa fedha nyingi katika elimu bila malipo pamoja na kukarabati shule na ujenzi wa shule mpya.

“Nyota yangu inang’aa namshukuru sana mheshimiwa rais kwa kuniamini, hii si kazi nyepesi, ninamshukuru kwa kutoa fedha nyingi katika wizara yangu,” alisema Profesa Ndalichako.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles