LONDON, ENGLAND
BAADA ya Anthony Joshua juzi kutangazwa kuwa bingwa wa ngumi uzito wa juu baada ya kumchapa mpinzani wake, Wladimir Klitschko, bondia huyo ametuma salamu za vitisho kwa bingwa Tyson Fury.
Joshua juzi aliweza kumgaragaza Klitschko kwa KO katika raundi ya 11 na kufanikiwa kutwaa mkanda wa WBA na IBF, pambano ambalo lilifanyika kwenye Uwanja wa Wembley, jijini London.
Pambano hilo lilianza kwa mabondia hao kushambuliana kwa kushtukiza, huku raundi ya tano Klitschko akishambuliwa ngumi na kuanguka chini kabla Joshua na yeye kuangushwa katika raundi ya sita.
Joshua, mwenye umri wa miaka 27, amesema kwa sasa anataka kuwa bingwa wa dunia na kuweka historia nchini England kwa kuwa bora zaidi ya mabondia wote, ikiwa pamoja na Fury mwenye umri wa miaka 28.
Fury amekuwa na historia kubwa katika mchezo huo kwa uzani wa juu, huku akiwa jumla amecheza mapambano 25 na kushinda mapambano yote, huku mapambano 18 akishinda kwa KO na hajawahi kupoteza hata mchezo mmoja.
Wakati huo, pambano la juzi limemfanya Joshua kufikisha mapambano 19, huku akishinda yote kwa KO na hajawahi kupigwa hata pambano moja, hivyo amesema sasa yupo tayari kupigana na Fury.
“Fury uko wapi? Wewe ni mtoto mdogo tu kwenye ngumi, najua ulikuwa unaongea sana juu ya uwezo wangu kabla ya pambano hili dhidi ya Klitschko, sasa nataka watazamaji 90,000 wapate nafasi ya kutuona tukipambana ulingoni,” alisema Joshua baada ya pambano lake.
Hata hivyo, kupitia akaunti ya Instagram, Fury amemjibu Joshua kwa kusema yupo tayari kwa pambano hilo muda wowote kuanzia sasa.
“Njoo tucheze, nipo tayari kupambana na Joshua muda wowote kuanzia sasa, sina wasiwasi na uwezo wake na ninaamini nitaweza kuvuruga mipango yake.
"Kama tutapigana ninaamini tutawapa mashabiki pambano la aina yake ambalo halijawahi kutokea na litaweka historia kwa miaka 500, nipo tayari kwa hilo kwa kuwa utanifanya nitimize ndoto zangu,” aliandika Fury.
Hata hivyo, Fury alimpongeza Joshua kwa kuweza kushinda katika pambano hilo dhidi ya mpinzani wake mwenye uzoefu mkubwa katika ngumi.
Fury amekuwa nje ya uwanja tangu pambano lake la mwisho dhidi ya Klitschko ambalo lilipigwa Novemba 2015, huku Fury akiibuka bingwa wa mchezo huo kwa pointi.