NAHODHA wa timu ya Chelsea, John Terry, ametangaza kuondoka katika klabu hiyo baada ya kumalizika kwa msimu huu wa Ligi Kuu nchini England.
Mkataba wa mchezaji huyo unatarajiwa kumalizika mwisho mwa msimu huu na hadi sasa hajapewa mkataba mpya, hivyo amedai kwamba yupo tayari kuondoka baada ya kumaliza mkataba huo.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 35, aliyejiunga na klabu hiyo akiwa na umri wa miaka 14, ameipa ubingwa wa Ligi klabu hiyo mara nne, Kombe la FA mara tano na Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mara moja.
“Ningependa sana kuendelea kukaa katika klabu hii, lakini kwa sasa naona kama uongozi unaelekea sehemu tofauti, baada ya kuondoka Mourinho walisema kwamba akija kocha mpya mambo huenda yakabadilika, lakini bado mambo ni yela yale na ndiyo maana nasema kuwa nataka kuondoka.
“Kwa sasa bado sijapata mkataba mpya, imekuwa tofauti na miaka iliyopita, ambapo kila ikifika Januari mambo yanakuwa sawa, lakini mwaka huu imekuwa tofauti, hata hivyo siwezi kustaafu soka nikiwa na klabu ya Chelsea,” alisema Terry.
Hata hivyo, klabu hiyo imedai kwamba kuna uwezekano mkubwa wa mchezaji huyo kuongezewa mkataba muda mfupi ujao.
Terry ameitumikia klabu hiyo kwa kucheza jumla ya michezo 696 na amedai kwamba bado ana muda wa kucheza soka, japokuwa si lazima iwe kwenye klabu hiyo au klabu nyingine ya nchini England.