27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JK: WAPINZANI SI MAADUI

Awataka kutorudi nyuma kunadi sera zao, atoa neno kwa wabunge wa vyama tawala

Na Deogratias Mushi

-Johannesburg

RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, amevionya vyama tawala katika Bara la Afrika kuacha kasumba ya kuvichukulia vyama vya upinzani maadui bali viwaone kama washindani.

Kikwete ambaye tangu astaafu baadhi ya wapinzani wamekuwa wakimkumbuka na hata kufuta kumbukumbu za mashtaka ya kufinya demokrasia, kutokana na kile wanachodai kubanwa zaidi na uongozi wa sasa, aliyasema hayo wakati akichangia mada ya Utawala Bora na Utawala wa Sheria iliyowasilishwa na Profesa Barney Pityana, ambaye ni Makamu Mkuu Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini kwenye Kongamano la Uongozi barani Afrika yaani ‘African Leadership Forum 2017’.

Kikwete aliliambia kongamano hilo la siku mbili lililomalizika jana jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini na kukutanisha viongozi mbalimbali akiwamo mtangulizi wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kuwa vyama tawala kuvichukulia vyama vya upinzani kama maadui ni kusababisha uadui usiokuwa na faida kwa nchi.

 

Katika hilo, Kikwete alivitaka vyama vya upinzani barani Afrika kutokurudi nyuma katika kunadi sera zao kwa wananchi.

Alisema vyama vya upinzani barani Afrika vinapaswa kuelezea vyema sera zao kwa wafuasi wao ili wazielewe na ufikapo wakati wa uchaguzi wapiga kura wawe na uelewa wa kutosha kuhusu mipango yao ya kuongoza nchi.

 

“Vyama vingi vya upinzani barani Afrika bado ni vichanga na kwa Tanzania viliruhusiwa tena mwaka 1992 na kwa sasa vinapaswa kujijenga kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi husika,” alisema Kikwete wakati anachangia mada hiyo.

Akielezea umuhimu wa vyama vya upinzani katika Taifa lolote lile, Kikwete alisema ni kuvifanya vyama tawala kuwa macho si kulala.

“Pia kazi ya upinzani ni kuiambia Serikali kile inachofanya ni kibaya, ambacho katika chama chako hawawezi kuona au wanaweza kuona lakini wasiwe na ujasiri wa kusema kipi sahihi.

“Wakati nikiwa rais nilikuwa nikiwaambia wanachama wangu, jukumu lenu ni kuisimamia Serikali, si kwa sababu unatokea chama tawala usiseme kuwa jambo hili baya, isipokuwa  linapokuja suala la kura, basi piga kura na chama chako,” alisema.

Kikwete alisema utawala bora unatokana na kuwepo kwa demokrasia, mahali ambapo kuna udikteta kunakuwa hakuna demokrasia.

Kauli hiyo ya Kikwete imekuja wakati ambako malalamiko ya vyama vya upinzani nchini dhidi ya chama tawala kuhusu kubana demokrasia yakizidi kuongezeka.

Kutorusha Bunge ‘live’, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara, kukamatwa na kufunguliwa kesi watu wanaoikosoa Serikali hususani wanasiasa wa wapinzani, ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wapinzani nchini kuwa yanabana demokrasia.

Mbali na hilo la demokrasia, Kikwete pia alitoa rai kwa wabunge wa vyama vilivyopo madarakani kuhoji Serikali pale mambo yanapokuwa hayaendi vizuri, kwani kufanya hivyo kunaimarisha utawala wa sheria.

 

Alisema wabunge wa chama tawala barani Afrika inabidi waangalie ilani za vyama vyao na kuhoji pale Serikali haitekelezi kama ilivyoahidi, huku akisisitiza hali hiyo isichukuliwe kama kuipinga Serikali, bali kuiweka katika mstari.

“Tunapaswa tusifike hatua ambayo washirika wa chama chako hawawezi kusema kitu kibaya ambacho Serikali inafanya. Kwa sababu kitakachotokea ni watu wataenda kupigia kura upinzani ambao wana ujasiri wa kuwaambia Serikali ukweli,” alisema.

Akilizungumzia Bunge alisema ni chombo muhimu kwani linasimamia shughuli za Serikali bila kuogopa na linasema kipi kilicho bora na kibaya.

“Kama Bunge halifanyi hivyo, Serikali haiwezi kuonywa, makosa yataendelea na kutakuwa hakuna utandawazi na uwajibikaji,” alifafanua Kikwete.

Kwa upande wa chaguzi mbalimbali zinazofanyika Afrika, Kikwete alisema:

“Lazima tuwe na tamaduni ya kukubali kushindwa, migogoro mingi katika Afrika inatokea baada ya uchaguzi. Uchaguzi wa haki usiwe kama ni kushinda tu,” alisema Kikwete.

 

Alisema utawala bora ni jambo muhimu ambalo nchi za Kiafrika zinapaswa kutilia maanani.

Pamoja na hayo, Kikwete alipongeza baadhi ya nchi ambazo zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa zinatilia maanani misingi ya utawala bora.

“Si kweli kuwa barani Afrika hakuna utawala wa sheria au kila kitu Afrika ni kibaya hapana.  Kumekuwa na juhudi nyingi za kuhakikisha kuwa migogoro inayozikumba baadhi ya nchi inatatuliwa ili kuwe na amani na utulivu katika nchi hizo,” alisema Kikwete.

Kauli hizo za Kikwete zilionekana kumkuna mwanasiasa na kiongozi wa upinzani wa chama cha Democratic Alliance (DA) cha Afrika Kusini, Mmusi Maimane.

Maimane aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: “Rais Kikwete ameibua hoja ya umuhimu wa upinzani Afrika  kama kazi ya utawala bora. Si maadui lakini washindani.”

Hoja hiyo ya Maimane ilimwibua mmoja wa wanasiasa wa upinzani hapa nchini, ambaye pia na mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF)  ambacho kipo kwenye mgogoro mkubwa wa kiuongozi,  Ismail Jussa.

 

Jussa kupitia ukarasa wake wa Twitter aliandika kuwa: “Ni uongo wa hali ya juu, maneno matupu. Ni Kikwete ambaye alituma jeshi kwenda Zanzibar, Oktoba 2015 na kufuta uchaguzi kwa sababu CUF ilikuwa inashinda.”

 

 

Akizungumza na wanahabari jana jijini Johannesburg, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, alivitaka vyombo vya habari barani Afrika kuwa wazalendo kwa kuandika habari zitakazosaidia kutatua migogoro na kuleta maendeleo.

Mkutano huo wa siku mbili ulihudhuriwa pia na marais wastaafu Olusegun Obasanjo (Nigeria), Thabo Mbeki (Afrika Kusini), Mohamed Marzouki (Tunisia), Hassan Mohammed (Somalia), Bakili Mulizi (Malawi), Mwanasheria Mkuu wa Uganda, Bart Katureebe.

Ulimalizika jana kwa kuwataka viongozi barani Afrika kuunganisha nguvu zao katika kujenga amani na utulivu barani humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles