30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MANJI ANA KESI YA KUJIBU

PATRICIA KIMELEMETA NA MANENO SELANYIKA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, amekutwa na shtaka la kujibu katika kesi inayomkabili ya matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi wa awali.

Hakimu Mkeha alisema ameridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wanne wa upande wa mashtaka na kwamba mshtakiwa ana haki ya kujitetea kutokana na mkojo wake kukutwa na dawa aina ya Morphine ambayo zao lake ni heroin.

“Hivyo mshtakiwa anapaswa kujitetea kwa sababu mahakama imemkuta na hatia,” alisema Mkeha.

Baada ya kuelezwa hayo, wakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo, alidai kuwa mshtakiwa atajitetea kwa hati ya kiapo ambapo watakuwa na mashahidi 15 katika kesi hiyo.

Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 30 ambapo itasikilizwa mfululizo hadi tarehe 31, 2017.

MAJIBU YA MKEMIA WIKI HII

Katika ushahidi wake alioutoa wiki hii,

Mkemia kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Domician Dominic, aliieleza mahakama hiyo kuwa ni vigumu kupata heroine ndani ya mkojo kwani inapokuwa ndani ya mwili kwa dakika 20 hadi 60 hubadilishwa na kuwa morphine.

Akijibu hoja zilizoibuliwa na wakili wa  Manji, Ndusyepo iwapo mkojo alioupima ulikuwa ni Manji au wa askari,  Mkemia huyo  alisema hajui ni wa nani kwa sababu wakati Manji anachukuliwa sampuli hiyo aliingia chooni na askari, huku yeye akiwasubiri nje.

Wakili huyo alihoji jambo hilo ili mashahidi waithibitishie mahakama kwani wakati Manji anakwenda msalani kutoa sampuli hiyo ya mkojo aliongozana na askari.

Mkemia huyo pia alisema katika kipimo cha mkojo wa Manji amebaini uwepo wa dawa aina ya Benzodiazipines ikiwa ni zao la heroin, ingawa alisema hiyo ina matumizi mengi ikiwemo kuondoa maumivu makali, ikitegemeana na ushauri wa daktari.

Dominic ni shahidi namba tatu katika kesi ya matumizi ya heroine inayomkabili diwani huyo wa Mbagala, Manji.

Manji anadaiwa kutumia dawa za kulevya aina ya heroine kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu katika eneo la Sea View, Upanga wilayani Ilala.

Manji na Askofu wa Ufufuo  na Uzima, Josephat Gwajima, walifikishwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali mapema mwaka huu na kuchukuliwa sampuli ya mkojo kwa nia ya kuwapima ili kubaini iwapo wanatumia dawa za kulevya.

Wakati Manji kesi yake ikiendelea, Gwajima yeye aliachiwa huru akidai kuwa mkojo wake ulikutwa safi licha ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kumhusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Wakati huo huo, jana mahakama hiyo imeutaka upande wa Jamhuri kuharakisha upelelezi kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara Manji na wenzake watatu.

Akizungumza wakati kesi hiyo ilipokuja kutajwa, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, alisema upande wa Jamhuri wanapaswa kujitahidi kukamilisha upelelezi huo ili matokeo ya kesi yajulikane haraka.

Hoja hiyo iliungwa mkono na upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Hudson Ndusyepo na Semi Malimi ambao waliiomba Jamhuri kueleza hatua ya upelelezi ilipofikia wakati kesi hiyo itakapokuja kutajwa tena.

Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliongozwa na mawakili, Simon Wankyo na Tulumanywa Majigo ambao walidai mahakamani hapo kuwa upelelezi bado haujakamilika na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kesi hiyo pia imeahirishwa hadi Agosti 31, mwaka huu.

Manji na wenzake watatu wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa Taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na mihuri ya jeshi.

Manji na wenzake Deogratias Kisinda, Abdallah Sangey na Thobias Fwere, walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka likiwamo la uhujumi uchumi.

Wanadaiwa kuwa katika eneo la Chang’ombe ‘A’ Wilaya ya Temeke,  Dar es Salaam, washtakiwa hao kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na bunda 35 za vitambaa vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) zenye thamani ya Sh milioni 192.5 na kwamba mali hiyo ilipatikana kinyume cha sheria.

Katika shtaka la pili, Manji na wenzake wanadaiwa Julai mosi mwaka huu huko Chang’ombe ‘A’ walikutwa na polisi wakiwa na mabunda nane ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania zenye thamani ya Sh milioni 44  mali ambayo ilipatikana isivyo halali.

Katika shtaka la tatu, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Juni 30 mwaka huu katika eneo la Chang’ombe ‘A’ walikutwa na muhuri wa Jeshi la Wananchi Tanzania wenye maandishi ‘Mkuu 121 kikosi cha JWTZ’ bila ya kuwa na uhalali kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles