Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MAZUNGUMZO ya kusaka mwafaka kati ya Rais, Jakaya Kikwete na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) yamemalizika huku kila upande ukitoa masharti ya kumaliza mgogoro uliopo kuhusu kusitishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba.
Mkutano huo uliofanyika Ikulu ndogo mjini Dodoma jana, uliratibiwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), huku ukiwa umehusisha viongozi wa vyama vyote vya siasa nchini.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho kililiambia MTANZANIA kuwa, katika kikao hicho viongozi wa Ukawa walikwenda na pendekezo la kumtaka Rais Jakaya Kikwete asitishe mkutano wa Bunge la Katiba ili kuruhusu mabadiliko ya Katiba.
Wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo walitoa mapendekezo hayo kwa Rais Kikwete ikiwemo kuitaka Serikali kupeleka marekebisho madogo yafanyike katika Katiba ya sasa kuruhusu mgombea binafsi na uundwaji wa Tume huru ya Uchaguzi.
Mbali na hilo pia wamemuomba Rais Kikwete katika marekebisho hayo ya Katiba ya mwaka 1977 kuwepo kwa Mahakama ya Juu (Supreme Court) na matokeo ya urais yaruhusiwe kupingwa mahakamani.
Hata hivyo taarifa hizo zilidai kuwa, mjadala huo mkali ulihitimishwa na Rais Kikwete kuwataka wajumbe hao wa TCD kuhakikisha wanakaa pamoja na kuangalia namna bora ya kuliahirisha Bunge hilo kwani sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 haielezi namna ya Bunge hilo kuahirishwa.
Chanzo hicho kilisema kutokana mapendekezo hayo ya kila upande wajumbe wanaounda TCD walitakiwa kwenda kujadiliana kwa kina namna bora ya kuliendea jambo hilo kama ilivyopendekezwa na Rais Kikwete.
Katika kikao hicho TCD walilazimika kuunda kamati ndogo itakayoongozwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia huku wajumbe wake wakiwa ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, Mwenyekiti wa Chama cha Wanannchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa.
Kamati hiyo itafanya kazi ya kuchambua mapendekezo mbalimbali ambapo itakutana tena Septemba 6-7 mwaka huu kabla ya Septemba 8 kukutana na Rais Jakaya Kikwete.
Taarifa hizo kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza baada ya kikao hicho cha pamoja Rais Kikwete, atawasiliana na mamlaka husika kuangalia namna bora ya kusitisha vikao vya Bunge hilo ili kuruhusu mazingira ya kufanyika kwa Bunge la Jamhuri.
Hatua hiyo italifanya Bunge la Jamhuri kufanya marebisho hayo kwa ajili ya muundo wa Tume ya Uchaguzi na namna bora ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu na baadaye uchaguzi mkuu mwakani.
Awali akitoa taarifa za kikao hicho na Rais Kikwete, Mwenyekiti wa TCD, John Cheyo alisema kwamba baada ya mjadala mzito walikubaliana kukutana tena na Rais Kikwete Septemba 8 mwaka huu.
“Ndugu waandishi wa habari, leo (jana) wenyeviti na makatibu wa vyama vya siasa vinavyounda TCD tulikutana na rais kujadili ajenda mbili. Ajenda ya kwanza ilihusu mchakato wa Bunge Maalumu la Katiba na ajenda ya pili ilihusu mambo ya kuimarisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Rais amekubali kuangalia mambo tuliyomweleza na akatuomba na sisi wajumbe wa TCD tukayatafakari huku na yeye akiendelea kuyatafakari ili tukutane Septemba 8 mwaka huu.
“Kwa kuwa jambo hili ni muhimu, tumeunda kamati ndogo itakayoangalia mambo yaliyozungumzwa na kuyatolea ufafanuzi kisha kamati hiyo itawasilisha ripoti yake Septemba 8 tutakapokutana,” alisema Cheyo.
Kabla ya Rais Kikwete kukutana na wajumbe wa TCD, wajumbe hao walianza kukutana wenyewe katika Hoteli ya Dodoma na kujadiliana mambo ya kuzungumza pindi watakapokutana na Rais Kikwete.
Baada ya kutoka hapo, walielekea Ikulu ndogo iliyoko Kilimani mjini hapa. Hata hivyo, kabla Rais Kikwete hajakutana na TCD, inasemekana alikuwa na mazungumzo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Steven Wasira pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi.
Taarifa za ndani zilinaeleza kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Phillip Mangula, nusura achafue hali ya hewa baada ya kuwataka Ukawa warudi bungeni wakati mazungumzo hayo yakiendelea.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kauli hiyo ilionekana kuwakera baadhi ya wajumbe wa Ukawa wakiwamo Profesa Lipumba na Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya ambao walilazimika kumpinga wazi wazi.
Wakati wa mijadala ya vikao hivyo, CCM waliwakilishwa na Kinana na Mangula. Chadema waliwakilishwa na Dk. Slaa pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu. Kwa upande wa NCCR-Mageuzi, alikuwapo Mbatia na Katibu mkuu wake, Mosena Nyambabe wakati CUF waliwakilishwa na Profesa Lipumba pamoja na Sakaya.
Chama cha UDP kiliwakilishwa na mwenyekiti wake, John Cheyo akiwa na mdogo wake Isack Cheyo. TLP alikuwapo Mwenyekiti wa chama hicho, Augustine Mrema na Fahmi Dovutwa aliviwakilisha vyama visivyokuwa na wabunge bungeni.
mimi naona tu watu waondoe ubinafsi katiba mpya itapatikana
Dalili zote zinaonyesha katiba mpya ni mpaka 2018/2019 rais ajaye atafanikisha, ni bahati mbaya wanasheria waliopo serikali wakiongozwa na mwanasheria mkuu wa serikali wameshindwa kumshauri Rais vizuri kama kwamba wanasheria wote wazuri wako nje ya mfumo wa serikali kama mawakili binafsi, kwenye mashirika ya umma,vyama vya upinzani au katika makampuni ya kimataifa. Lazima warudi kwenye Rasimu halisi(original) na siyo maoni yanaendelea sasa hivi kwenye bunge la katiba linaloendelea.
Cha muhimu ni kuwepo muafaka unaokubalika na pande zote mbili kinzani ndani ya Bunge la Katiba kuhusu njia bora ya kuhakikisha watanzania wote wanashiriki au kuwakilishwa kwenye utunzi wa Katiba mpya itakayokubalika na wote. Itakuwa jambo jema kusitisha zoezi ili kuwezesha maandalizi mazuri zaidi yaweze kufanywa kwenye kuhakikisha uwepo wa taratibu nzuri zaidi zitakazopelekea upatikanaji wa Katiba mpya isyokuwa pendeleo kwa kundi lolote au mshirika yoyote na inayokubalika na wengi (kama sio wote) ndani ya pande mbili husika kwenye Muungano Tanzania. Muafaka kwenye Muundo wa Serikali ya Muungano ndio msingi madhubuti wa Katiba mpya tarajiwa na ni kura ya maoni pekee itakayowezesha wavisiwani na wabara kuamua Muundo huo muafaka utakaokubalika na wengi ndani ya pande zote mbili za Muungano. Awamu ya Kwanza na muhimu zaidi ni kura ya maoni kuhusu Muundo wa Serikali ya Muungano. Awamu ya pili ni ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya na utunzi wa Rasimu ya Katiba. Awamu ya tatu ni uboreshaji wa Rasimu ya Katiba mpya ndani ya Bunge la Katiba. Awamu ya nne iwe kura ya maoni ya watanzania kuikubali au kuikataa rasimu ya Katiba mpya. Muungano utakaodumu na kunufaisha watanzania wa pande zote za Muungano ni ule ulio muafaka wa wengi ndfani ya pande zote husika. Wanasiasa wakitoa fursa kwa watanzania waamue muundo wa Serikali na Katiba ya Muungano wanaotaka watakuwa wametekeleza vizuri majukumu yao kama wanasiasa.