
NA JENNIFER ULLEMBO
KOCHA mkuu wa timu ya Yanga, Marcio Maximo, ametuma maombi kwa uongozi wa klabu hiyo kumtafutia michezo miwili zaidi ya kimataifa kabla ya kuivaa Azam FC Septemba 13 jijini Dar es Salaam, katika mechi ya Ngao ya Hisani.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto alithibitisha kutumwa maombi hayo kwa uongozi.
Kiziguto alisema mchezo wa kwanza wa kimataifa, utachezwa kesho dhidi ya Thika United kutoka nchini Kenya, huku mchezo wa pili ukitarajiwa kucheza Jumapili ijayo.
“Kocha anahitaji mechi mbili zaidi za kimataifa, awali ilikuwa ni mechi moja lakini sasa amebadilisha na uongozi umeanza kushugulikia,” alisema Kizuguto.
“Sijajua tutacheza na timu gani mechi mbili za ziada, lakini kocha amesisitiza zifuatane yaani ikimalizika ya Jumapili nyingine ifanyike wiki inayokuja,” alisema Kizuguto.
Alisema uongozi unatambua mchezo huo wa Ngao ya Hisani ni muhimu kwa timu, ndiyo maana umekubaliana na mapendekezo ya kocha.
Maximo ameonyesha kujipanga zaidi kuelekea katika mchezo na Azam FC, ambapo mbali na kuhitaji mechi za ziada ameanza kurudia mazoezi aliyowapa wachezaji wake visiwani Zanzibar.