Na Muhammed Khamis (UoI) Iringa,
UCHAKAVU wa mabomba ya kusambazia maji safi na salama yaliyowekwa miaka ya 1960 katika Tarafa ya Isimani, Wilaya ya Iringa Vijijini, wana changamoto kubwa ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu kwa miaka 20 sasa.
Uwepo wa changamoto hiyo unawalazimu wananchi wa eneo hilo kutumia maji yenye chumvi kwa mahitaji yao ya kila siku na hivyo kujiweka katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza.
Mkazi wa tarafa hiyo, Letisia Kalinga, alisema changamoto ya maji katika eneo lao ni ya muda mrefu, huku mabomba ya maji yakibaki kama maonyesho.
Alisema hali hiyo inawaletea usumbufu mkubwa wananchi, hususani kina mama kwani hulazimika kufuata maji maeneo ya mbali zaidi, huku yakiwa si mazuri kwa kutumia.
“Iwapo unataka maji mazuri, ni lazima ununue kwa gharama ya Sh 500 kwa dumu moja jambo ambalo ni changamoto kubwa kwa maisha ya kijijini kuweza kumudu,” alisema.
Kwa upande wake, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Isimani, Gogfrey Kinyoya, alisema ukosefu wa maji katika eneo hilo ni changamoto pia kwa wanafunzi wa bweni shuleni kwao.
Alisema imefika wakati sasa Serikali kuingilia kati jambo hilo kutokana na umuhimu wa huduma hiyo kwa wananchi, ukizingatia tarafa ya Isimani imezungukwa na vianzio vingi vya maji akitolea mfano Mto Ruaha.
Mkazi mwingine wa eneo hilo, Maimuna Lumato, alisema kuwa wanawake ndio wamekuwa waathirika wakubwa wa kadhia hiyo ya ukosefu wa maji safi na salama kwa miaka mingi sasa, huku akiwatupia lawama viongozi wao kwa kushindwa kuwaondolea kero hiyo.
Alisema tangu wamchague Wiliam Lukuvi ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa mbunge wao, hajawahi kufika kutaka kujua changamoto zinazowakabili wananchi wa eneo hilo.
“Viongozi wetu wamekuwa na ahadi nyingi wakati wa mchakato wa kuomba kura, lakini mara baada ya kuchaguliwa wanasahau wajibu wao kwa wananchi waliowachagua.
“Hebu angalia eneo letu hili la Isimani limezungukwa na vyanzo vikubwa vya maji, kwa mfano Mto Ruaha ambao upo karibu na hapa, lakini tumekosa kufaidika na rasilimali hiyo,” alisema Maimuna.
Mwenyekiti wa kijiji katika Tarafa ya Isimani, Daudi Kombora, alikiri kwamba kero ya maji katika eneo hilo ni ya miaka mingi na hadi sasa bado hakuna ufumbuzi wowote.