26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Jiji la Mwanza latenga maeneo zaidi ya 48 kwa ajili ya machinga

Na Clara Matimo, Mwanza

Katika kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuwataka Wakuu wa Wilaya na mikoa kuwatambua na kuwawekea mazingira wezeshi  wafanyabiashara wadogo (machinga) ya kufanyia biashara,  halmashauri ya jiji la Mwanza imetenga maeneo zaidi ya 48 kwa ajili yao.

Hayo yamebainishwa jijini Mwanza leo Alhamisi Septemba 23, 2021 na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi,  wakati akizungumza na machinga wa   jiji hilo kwa nyakati tofauti katika maeneo mbalimbali alipokuwa kwenye ziara ya kuongea nao iliyolenga kuwapa elimu kwa nini wametengewa maeneo hayo.

Amesema zoezi la kuwatengea maeneo linaenda sambamba na kuwatambua ambapo kila machinga atatakiwa kujaza fomu lengo ni serikali iwe na takwimu sahihi ya wafanyabiashara wanaolipa kodi hali itakayoweiwezesha kukusanya mapato, kuzidi kuimarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao, tunzaji wa mazingira na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, wakati na wakubwa kuongeza kipato.

Amefafanua kwamba  ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa  wameunda kamati  mbalimbali ikiwemo ya kutoa elimu kwa machinga, kuwatambua ili wajue idadi yao na kutambua maeneo ambayo  watapelekwa maana  wanahitaji wenye sifa ya kuendelea kuwa machinga waendee ambao  mitaji yao imekuwa kuaniza  Sh 4,000,000  wanafaa kuwa wafanyabiashara wa kati  wakate leseni wapewe maeneo ambayo yana mazingira wezeshi.

“Kuna watu wanapita na kuwalaghai msijaze fomu naomba niwaambie msiwasikilize mnachotakiwa ni kuiamini serikali yenu hao wanaowadanganya hawana nia njema na nyie, tutakapoanza kugawa maeneo tutagawa kwa waliojaza fomu tu na hakutakuwa na ukilitimba wa aina yoyote tena siku hiyo kila machinga atapata eneo lake kwa kuchagua mwenyewe karatasi iliyoandikwa aende eneo gani maana tutaweka vikaratasi kwenye pipa kila mtu atachagua.

“Fomu hizo zitatusaidia kujua tunao machinga wangapi ili tunapotenga maeneo tutenge kulingana na idadi yenu vile vile itatusaidia kujua aina ya biashara ambayo mnaifanya iwe rahisi kila mfanyabiashara  kupagwa eneo ambalo linaendana na aina ya biashara yake maana tumelenga kila biashara iwe na eneo maalum lakini kwa sababu mama lishe inatakiwa wawepo kila sehemu tunataka tuwapange  vizuri ili wasiweze kuleta madhara ya moto hatuwezi kuwa na eneo moja ambalo linauza bidhaa zote.

“Nawaomba mnisikilize mimi ndiye mkuu wenu wa wilaya siwezi kuwaangamiza, lengo la kiongozi yeyote ni kuweka mazingira bora kwa watu wake na hiyo ndiyo nia ya Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan, ametuagiza sisi wasaidizi wake tuifanye kazi hiyo, huko tutakakowapeleka tutakuwa tumepawekea miundombinu mizuri kabisa,”amesisitiza Makilagi.

Kwa mujibu wa Makilagi zoezi la kuwatambua machinga limeanza Septemba 20  litakamili mwezi huu  tarehe 26 lakini hadi jana septemba 22 zaidi ya machinga 3,800 walikuwa wameishajiandikisha ambapo amebainisha kwamba jiji hilo linakadiriwa kuwa na machinga 15, 000 kwa mujibu wa vitambulisho vya taifa.

“Naupongeza uongozi wa machinga wilaya na mkoa  wameamua kujitoa kwa ajili ya nchi yao, tumekuwa tukishirikiana nao katika kamati zote nilizozitaja ili kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa kuna baadhi ya watu wanafanya upotoshaji kwamba wamelipwa na serikali naomba waelewe hawajalipwa hata senti moja, harusi huwa inaandaliwa na watu wachache tu ambayo ni kamati lakini siku ya kusherekea wanasherekea wengi.

Amesema Wilaya ya Nyamagana ndiyo kitovu cha biashara kwa sababu kuna mzunguko wa pesa hata wafanyabiashara wakubwa wanaopata fedha wilaya na mikoa mingine wanahamia humo hivyo wamedhamiria iwe eneo la mfano hasa ukizingatia makao makuu ya machinga nchini yapo wilayani humo.

Mwenyekiti wa Muungano wa machinga Mkoa wa Mwanza, Said Tembo, amesema ziara hiyo ya mkuu wa wilayaya imesaidia kuwatoa wasiwasi machinga maana walikuwa na hofu kwamba ndiyo mwisho wa biashara zao  kwa hiyo elimu waliyopewa imesaidia kuondoa maneno ya uzushi wanayoambiwa kuhusu zoezi la kuwatambua.

“Tunamshukuru sana mkuu wetu wa wilaya kwa ziara hii iliyolenga kutupa elimu maana wanachama wetu walikuwa na hofu kwamba tutaondolewa bila kupewa maeneo mengine, nawaomba watulie wajaze fomu ili watambuliwe watakapoanza kugawa maeneo kila mtu apate. Serikali yetu inatujali tumeambiwa hata maeneo ambayo hayana vituo vya daladala vitawekwa tuseme nini zaidi ya kushukuru,” alisema Tembo.

AMINA: Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, akizungumza na machinga wa wilaya hiyo wanaofanya biashara katika mtaa wa barabara ya Nyarere lengo likiwa ni kuwapa elimu ya kwa nini wanatengewa maeneo kwa ajili ya kufanyia biashara zao. Picha na Clara Matimo.

AMINAA: Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, akizungumza na machinga wa wilaya hiyo  wanaofanya biashara katika mtaa wa barabara ya Nyarere lengo likiwa ni kuwapa elimu ya kwa nini wanatengewa maeneo kwa ajili ya kufanyia biashara zao. Picha na Clara Matimo.

MAKILAGI: : Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, akizungumza na machinga wa wilaya hiyo wanaofanya biashara katika mtaa wa barabara ya Nyarere lengo likiwa ni kuwapa elimu ya kwa nini wanatengewa maeneo kwa ajili ya kufanyia biashara zao. Picha na Clara Matimo.

WANANCHI :Baadhi ya machinga wanaofanya biashara  Wilaya ya Nyamagana katika mtaa wa barabara ya Nyerere wakimsikiliza Mkuu wa wilaya hiyo, Amina Makilagi alipofika kuwapa elimu ya kwa nini wanatengewa maeneo kwa ajili ya kufanyia biashara zao. Picha na Clara Matimo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles